26
MKANGANYIKO WA DHANA ZA MZIZI, KIINI NA SHINA KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI Joash Johannes Gambarage Ikisiri Kwa mwanazuoni yeyote ambaye anafahamikiwa na dhana za kimofolojia hakosi kuwa amewahi kuzitumia au kuzisoma au hata kuzieleza dhana za kiini, shina na mzizi. Mbali na matumizi ya dhana hizi ni ukweli usiopingika kwamba dhana hizi zimekuwa zikitumika katika kufasili dhana nyingine pia. Uambishaji, kwa mfano, ni dhana ijumuishayo dhana za kiini, shina na mzizi. Katika-Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha (2004: 23) Massamba anaieleza dhana ya uambishaji kuwa ni utaratibu wa kuweka kiambishi kabla, kati na baada ya mzizi. Katika fasili hii dhana ya mzizi imetajwa tayari. Hii ni kusema kuwa ni vigumu kukwepa matumizi ya dhana ya shina na mzizi katika mofolojia ya Kiswahili. Wataalamu wengine, kwa sababu ya kutokuwepo ubayana wa dhana hizi, hutumia dhana ya mzizi sawa na dhana ya shina (taz. Johannes, 2007). Hata hivyo, maswali yanabaki kuwa: Je, nini maana ya kiini, mzizi na shina? Je, dhana hizi zinafanana au zinatofautina vipi kimawanda katika sarufi ya Kiswahili? Nini mpaka unaotenganisha dhana hizi? Haya ni baadhi ya maswali ambayo wengi wetu tumewahi kujiuliza. Makala haya yatazamia fasili za dhana hizi. Yataanza kwanza kueleza mtazamo wa kimapokeo wa dhana zenyewe, kisha kutoa mjadala wa kiuhakiki kabla ya kuhitimisha kwa kutoa mtazamo binafsi. 1.0 Mtazamo wa Kimapokeo juu ya Kiini, Shina na Mzizi Kwa kuwa tutapitia pia maandishi yaliyoandikwa kwa Kiingereza ni vizuri tukipata tafsiri ya dhana hizi kwa Kiingereza. Kwa mujibu wa Kamusi ya TUKI (1990) istilahi hizi zimetafsiriwa hivi: ‘Base’ kiini/umbo msingi (taz. TUKI, 1990:8); ‘root’ mzizi (taz. TUKI, 1990: 50); na ‘stem’ shina (taz. TUKI, 1990: 53). Kabla hatujaingia katika kiini cha mjadala ni vema kwanza tukajaribu kuelewa dhana hizi zilivyowahi kuelezwa kimapokeo. Maelezo ya awali tuliyoweza kuyapata katika stadi za lugha za Kibantu juu ya dhana hizi ni yale ya Meeussen, 1967) ambaye, pamoja na mambo mengine, anagusia dhana

mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

  • Upload
    others

  • View
    1

  • Download
    0

Embed Size (px)

Citation preview

Page 1: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

MKANGANYIKO WA DHANA ZA MZIZI, KIININA SHINA KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI

Joash Johannes Gambarage

Ikisiri

Kwa mwanazuoni yeyote ambaye anafahamikiwa na dhana za kimofolojia hakosi kuwa amewahi kuzitumia au kuzisoma au hata kuzieleza dhana za kiini, shina na mzizi. Mbali na matumizi ya dhana hizi ni ukweli usiopingika kwamba dhana hizi zimekuwa zikitumika katika kufasili dhana nyingine pia. Uambishaji, kwa mfano, ni dhana ijumuishayo dhana za kiini, shina na mzizi. Katika-Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha (2004: 23) Massamba anaieleza dhana ya uambishaji kuwa ni utaratibu wa kuweka kiambishi kabla, kati na baada ya mzizi. Katika fasili hii dhana ya mzizi imetajwa tayari. Hii ni kusema kuwa ni vigumu kukwepa matumizi ya dhana ya shina na mzizi katika mofolojia ya Kiswahili.

Wataalamu wengine, kwa sababu ya kutokuwepo ubayana wa dhana hizi, hutumia dhana ya mzizi sawa na dhana ya shina (taz. Johannes, 2007). Hata hivyo, maswali yanabaki kuwa: Je, nini maana ya kiini, mzizi na shina? Je, dhana hizi zinafanana au zinatofautina vipi kimawanda katika sarufi ya Kiswahili? Nini mpaka unaotenganisha dhana hizi? Haya ni baadhi ya maswali ambayo wengi wetu tumewahi kujiuliza. Makala haya yatazamia fasili za dhana hizi. Yataanza kwanza kueleza mtazamo wa kimapokeo wa dhana zenyewe, kisha kutoa mjadala wa kiuhakiki kabla ya kuhitimisha kwa kutoa mtazamo binafsi.

1.0 Mtazamo wa Kimapokeo juu ya Kiini, Shina na MziziKwa kuwa tutapitia pia maandishi yaliyoandikwa kwa Kiingereza ni vizuri tukipata tafsiri ya dhana hizi kwa Kiingereza. Kwa mujibu wa Kamusi ya TUKI (1990) istilahi hizi zimetafsiriwa hivi: ‘Base’ kiini/umbo msingi (taz. TUKI, 1990:8); ‘root’ mzizi (taz. TUKI, 1990: 50); na ‘stem’ shina (taz. TUKI, 1990: 53). Kabla hatujaingia katika kiini cha mjadala ni vema kwanza tukajaribu kuelewa dhana hizi zilivyowahi kuelezwa kimapokeo. Maelezo ya awali tuliyoweza kuyapata katika stadi za lugha za Kibantu juu ya dhana hizi ni yale ya Meeussen, 1967) ambaye, pamoja na mambo mengine, anagusia dhana hizi tatu. Meeussen, 1967: 97; taz. pia Good, 2005) anatumia mchoro ufuatao (taz. Kielelezo 1) kuonesha vipashio vya shina katika Mame-Bantu [tafsiri ya kielelezo ni yangu]:

Page 2: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

MKANGANYIKO WA DHANA ZA MZIZI, KIINI NA SHINA KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI 13

Shina

Kiini Dhamira

Mzizi-mnyambuliko Kaulitndwa

Mzizi Viambishi vya kaulitndsh, tndea, tndana

Kielelezo 1: Mchoro uoneshao vipashio ya shina

Katika kielelezo hiki ni wazi kwamba mtazamo wa Meeussen ni kuwa shina linajumuisha kiini cha neno, mzizi na viambishi vya dhamira. Mizizi ya neno, kwa mujibu wa Meeussen, ni ya aina mbili: aina ya kwanza ni mzizi wa mnyambuliko (extended root) - ule unaoundwa na baadhi ya viambishi vya kauli kama usababishi, utendea na utendana. Aina ya pili ni mzizi usioundwa na viambishi vyovyote. Katika aina hii ya pili ya mzizi hapana shaka kwamba ni mzizi unaobaki baada ya viambishi vyote kuwa vimeondolewa. Kiini cha neno, kwa mtazamo wa Meeussen, kinaweza kuundwa na aina mbili za mizizi zilizotajwa hapo juu na viambishi vya kauli mbalimbali. Kama tutakavyoona katika sehemu zinazofuata za makala haya mtazamo huu wa Meeussen unatofautina kwa kiasi kikubwa na mitazamo ya wataalamu kama Hartman (1972), Bauer (1983), Good (2005), Mgullu (1999), Kiango (2000), kwa kuwataja wachache tu.

2.0 Mapitio ya Fasili MatumiziBaada ya kupitia mtazamo huu wa kimapokeo ni vizuri kwanza tukajaribu kuzitalii fasili matumizi mbalimbali na kuchunguza undani wake:

Mohamed (1993: 56) ana haya ya kusema kuhusu mzizi:

Page 3: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

14 KISWAHILI JUZ. 74

Mzizi ni kiini cha kitenzi kinachobeba maana ya kitendo. Pia, inaweza kutafsiriwa [kufasiliwa]1 kwamba mzizi ni ile sehemu ya neno inayobaki baada ya kuondolewa viambishi vyote, yaani maana na vijenzi.

Fasili hii ya Mohammed inataja mambo ya msingi yafuatavyo: Mzizi ndiyo kiini cha neno (taz. pia Mgullu, 1999: 100). Hivyo ni sehemu ya msingi ya neno ambayo ina taarifa ya kileksika na ya kisarufi (taz. Hartman, 1972). Vilevile fasili hii inataja kwamba mzizi wa neno ni ile sehemu ya neno inayobaki baada ya viambishi vyote kuwa vimeondolewa. Fasili hii tunaafikiana nayo kwa kiasi kikubwa ingawa tunapaswa kuzingatia kuwa mzizi/kiini ni dhana inayohusu kategoria zote za maneno na siyo kitenzi tu.

Hata hivyo, fasili hii ya mzizi inatatizwa na maelezo ya baadae ya Mohamed anapofafanua aina za mizizi. Kwa mujibu wa Mohamed (1993: 57) kuna aina mbili za mizizi: (i) Mzizi asilia: huu ni ule unaobaki baada ya viambishi vyote kuondolewa. Kwa mfano, pik- katika pika, na lim- katika lima; (ii) Mzizi wa mnyambuliko: hujengwa na mzizi asilia pamoja na viambishi tamati vijenzi. Kwa mfano, limi-a, pigan-a. Ni wazi kuwa fasili hii inashabihiana sana na mtazamo wa Meeussen kuhusu mzizi wa mnyambuliko kama tulivyoona katika 1.1 hapo juu. Pamoja na kushabihiana huku bado kuna kauli mbili kinzani katika dhana hii ya mzizi. Ukinzani unajitokeza pale Mohamed anaposema kuwa mzizi hubaki baada ya viambishi vyote kuwa vimeondolewa na wakati huohuo anasema mzizi una viambishi vya kauli. Hapa inadhihirika kwamba maelezo haya ya Mohamed yana ukinzani wa kiwango cha juu. Ni vizuri pia kutanabahisha kuwa baadhi ya mizizi, ya maneno huru kama ‘baba’, ‘samaki’, kwa mfano, huwa haiambishwi. Kwa hiyo dhana ya uambishaji haihusu maneno yote katika lugha.

Ilivyo ni kwamba wakati shina ni muungano wa mzizi na viambishi kama vile vya kauli na/au irabu tamati, mzizi wa neno huru hauwezi kuchanganuliwa zaidi; kwa maana hiyo viambishi vya aina yoyote haviwezi kuwa sehemu ya mzizi wa neno huru. Halikadhalika wakati mwingine ‘amba’ kiini cha neno, kama kinavyojipambanua katika lugha ya Kiswahili kwa baadhi ya maneno ndio mzizi pia. Kama tutakavyoona katika sehemu inayofuata hii si mara ya kwanza, katika isimu ya lugha ya Kiswahili, kupambanua dhana ya kiini kuwa ndiyo mzizi.

Wakuza mitaala Taasisi ya Elimu (TE) (1996: 18-22) wanaitumia dhana ya kiini kumaanisha mzizi. Angalia baadhi ya mifano waitoayo katika (1):

1Msisitizo ulio katika mabano mraba ni wa mwandishi. Anataka kuonesha kuwa neno tafsiri linatumika kama uhawilishaji wa mawazo yaliyo katika maandishi toka lugha moja kwenda nyingine (taz. Mwansoko, 2006); wakati kutafasili ni kutoa maana ya neno.

Page 4: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

MKANGANYIKO WA DHANA ZA MZIZI, KIINI NA SHINA KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI 15

1. Maneno Kiini Maneno Kiinianaezeka ezek- Mageuzi geu- [geuz-]uongozi ongoz- tunamwende shea ende- [end-]ondoa ond- [ondo-]2 elekeza elek- [eleke-]piga pig- matembezi temb- [tembe-]hilo, hicho, hiyohi- matamshi am- [tamsh-]

Katika (1) baada ya kuhakiki ugawanyaji neno kimofolojia, inaonesha wazi kuwa dhana ya kiini na dhana ya mzizi ni dhana ile ile moja. Tazama mifano zaidi katika TE (1996: 22) na jinsi wanavyotofautisha dhana ya kiini (mzizi) na shina katika (2)

2. Maneno Kiini Shinashikishana shik- shikish-elekeza elek- [eleke] elekez-shikilia shik- shikili-

Ni wazi kuwa katika mifano ya (2) kiini kimetofautishwa na shina. Kwa maana hiyo kwa mujibu wa TE, shina linaweza kujumuisha mzizi na viambishi tamati vya baadhi tu ya kauli, na siyo vyote. Kwa mifano michache waliyoitoa katika (2) ni wazi kuwa baadhi ya viambishi vya kauli vinavyoungana na mzizi kuunda shina ni kama vile kauli ya udumishaji (katika neno shik-ili-a), kauli ya usababishi (katika maneno shik-ish-a na eleke-z-a). Hata hivyo inafaa kuweka bayana kuwa tunaweza kupata mashina ya vitenzi yaliyoundwa na kauli mbalimbali, kwa mfano, utendana, utendwa n.k. Maelezo yetu katika sentensi iliyotangulia yanashabihiana na maelezo ya Good (2007: 2) anayeeleza kuwa katika lugha za Kibantu mashina huundwa na viambishi lakini si mizizi. Jambo jingine la msingi linalofaa kusisitiza hapa ni kuwa, viambishi tamati kama vile irabu ishilizi na dhamira mbalimbali vinahusika pia kuunda mashina ya maneno.

Kihore na wenzake (2004) wanakubaliana na Crystal (1987) kuwa mzizi ni umbo-msingi la neno ambalo haliwezi kuchanganuliwa tena katika sehemu nyingine ndogo bila kupoteza (uamilifu na) utambulisho wake wa kisemantiki. Fasili hii inajitosheleza. Hata hivyo maelezo kuwa mzizi unahusiana na dhana ya uundaji wa neno jipya yatachunguzwa zaidi wakati wa mjadala juu ya mpaka wa shina na mzizi katika §.4.0.

Kihore na wenzake (2004: 63) wanaeleza kuwa kuna aina mbili za mizizi: funge, yaani, ile isiyoweza kusimama yenyewe kama neno na ile isimamayo yenyewe kama neno, yaani mizizi huru. Hapana shaka pia ugawaji huu wa mizizi ni wa kimofo-semantiki. Hii ni kusema umezingatia kigezo cha kimaumbo na cha kimaana.

2Msisitizo katika mabano unaonesha usahihi wa mizizi/viini. Hivyo, katika neno ‘ondoa’ kiini ni ondo- na siyo ond- kama wasemavyo TE. Halikadhalika katika neno ‘mageuzi’ kiini ni geuz- na siyo geu, katika neno‘tunamwendeshea’ kiini ni end- na siyo ende-, katika neno matembezi ni tembe- badala ya temb-. Kiini cha neno matamshi ni tamsh- ambacho umbo lake la ndani ni tamk-. Kilichotokea hapa ni mchakato wa kimofofonolojia kuwa /k/

[∫]/- i, (taz. pia Schadeberg, 1995; na Kahigi, 2003).

Page 5: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

16 KISWAHILI JUZ. 74

Juu ya dhana ya shina, Kihore na wenzake (weshatajwa) wanarejelea TUKI (1990: 53) kuwa shina ni sehemu ya neno yenye mzizi na viambishi. Fasili hii pia ni sahihi ingawa tutahitaji kuweka mkazo kuwa shina linaweza kuwa na kiambishi hata kimoja tu au zaidi. Maelezo ya Kihore na wenzake yanayohusisha dhana kuwa shina haliundi neno jipya tutayajadili tutakapokuwa tunaeleza suala la mpaka wa dhana hizi katika kipengee cha 4.0.

3.0 Dhana ya ‘Base’ na dhana ya ‘kiini’Baada ya kupitia maandishi ya wataalamu mbalimbali (Bauer, 1983; Crystal, 1987; Katamba, 1993; Good, 2005; Kiango, 2000) walioandika juu ya dhana ya ‘base’ katika lugha ya Kiingereza tutaona kuwa dhana hii inatofautishwa na mzizi ‘root’ na shina ‘stem’. Je, dhana ya ‘Base’ katika lugha ya Kiingereza ni sawa na dhana ya Kiini/mzizi/umbo msingi katika Kiswahili? Swali hili litakuwa limejibiwa baada ya kuwasoma watalaamu wafuatao: Bauer (1983: 21) anaweka bayana kama ifuatavyo:

“ a base is any form to which affixes of any kind can be added. This means that any root or any stem can be termed a base...”.

“kiini? cha neno ni umbo lolote la neno ambalo viambishi vya aina yoyote vyaweza kupachikwa. Mzizi wowote au shina lolote la neno laweza kuitwa kuwa ni kiini...” [tafsiri yangu].

Fasili hii ya Bauer inataja jambo la pekee kuwa kiini cha neno huweza kuambishwa. Fasili hii ya Bauer ina maana kuwa mzizi au shina la neno laweza kuitwa kiini cha neno. Kiango (2000) anakubaliana na fasili hii ya Bauer iliyotolewa hapo juu. Ili tuweze kuelewa vizuri kinachosemwa tutazame mifano kutoka katika lugha ya Kiingereza katika (3) na (4) kama ilivyotolewa na Kiango (2000: 77):

3. Base Neno lililoundwa na Base Ka+Mzizi+Kt(a) touchable un-touch-able(b) passable im-pass-able(c) guided mis-guide-ed(d) intergrated dis-integrate-ed(e) fulfillmentself-fulfill-ment

Base Neno lililoundwa na Base (Mzizi+Kt)4. (a) microscope (micro+scope) microscope+ic

(b) photograph (photo+graph) photograph+ic(c) photostat (photo+stat photostat+ic(d) telegraph (tele+graph) telegraph+ic

Tukiisoma kwa makini mifano katika (3) na (4) tutabaini kwa urahisi kabisa kuwa dhana ya ‘base’ inavyotumika hapa ni tofauti na ambavyo imeelezwa na wataalamu tuliowaeleza katika §. 2.1 na 2.2. Katika mifano 3 (a-d) tunaona dhana ya kiini katika lugha ya Kiingereza inapambanuliwa kuwa ni mizizi ambayo imeambikwa kauli. Ni wazi kuwa katika sarufi ya Kiswahili mzizi unaoambatana na viambishi

Page 6: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

MKANGANYIKO WA DHANA ZA MZIZI, KIINI NA SHINA KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI 17

vya mnyambuliko huitwa shina na siyo kiini. Mifano katika 3 (e) ni nomino ambayo imeundwa na mzizi wa kitenzi na kiambishi tamati-kijenzi. Kwa upande wa kulia wa mifano hiyo, ni maneno ya mnyambuliko yaliyoundwa kutokana na viambishi awali na viini. Mifano katika 4(a-d) inaonesha muundo wa kiini ambao ni muambatano wa mizizi. Kwa ujumla, pamoja na Kiswahili kuwa lugha ambishi-bainishi na Kiingereza kuwa lugha tenganishi (taz. Katamba, 1993: 60), tunaona kuwa mifano katika (3), katika sarufi ya Kiswahili ingeelezwa kuwa inahusu shina na siyo kiini/mzizi na mifano katika (4) inahusu mzizi/kiini.

Katika ufafanuzi wa hapo juu tumeona wazi kuwa, kwa mujibu wa Katamba, katika mifano (3) na (4) kiini kinaundwa na muambatano wa mzizi wa viambishi, hususani vya kauli na viambishi tamati ambavyo ni vijenzi. Maelezo haya ya Bauer (1983) na Kiango (2000) juu ya kiini hayatofautiani na maelezo ya Katamba (1993:45) ambaye anaeleza pia kuwa dhana ya ‘base’ inaweza kuambishwa na viambishi vya mnyambuliko au vya uambatishi3. Anaendelea kueleza kuwa mizizi yote ni viini lakini mashina yanaweza kuwa kiini endapo tu yanatumika katika muktadha wa uambatishi. Ili kuifafanua dhana ya kiini, Katamba (1993: 46) naye anatoa mifano ifuatayo katika lugha ya Kiingereza katika (5) na ambayo inatupatia mizizi, shina na viini katika (6) hapa chini:

5. faiths frogmarchedfaithfully bookshopsunfaithful window-cleanersfaithfulness hardships

6. Mzizi (root) Shina (stem) Kiini (base) [Tafsiri yangu](a) faith faithful faiths(b) frog frogmarch frogmarch(c) book bookshop bookshops(d) clean windowcleaner window-cleaner(e) hard hardship hardhip(f) window window-clean

Katika mifano (6) Katamba amebainisha mizizi, mashina na viini. Mizizi katika data yake imeainishwa kwa usahihi. Kinachoonekana ni kuwa neno ‘faith’ linajitokeza kama mzizi, kama shina na kama kiini. Maneno mengine katika 6(b)-(g) yanajitokeza katika miktadha tofauti. Kwa mujibu wa Katamba neno ‘faith’ linakuwa mzizi kwa sababu linaweza kuunda neno jipya; mfano ‘faithful’, faithfulness n.k. Na neno hilohilo pia linakuwa shina kwa sababu linaweza kuambikwa viambishi vya uambatishi kama -s katika wingi na kuwa “faiths”. Kuwa na neno moja linalotumika kama mfano wa dhana zote tatu kunatufanya tuzidi kuhoji

3Dhana ya uambatishi hapa inatumika kama tafsiri ya inflection, yaani uambikaji wa viambishi katika mzizi au shina la neno bila neno hilo kubadili kategoria ya neno au mwelekeo wa maana katika neno.

Page 7: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

18 KISWAHILI JUZ. 74

zaidi juu ya mpaka wa dhana hizi. Katika data hii maneno ‘frogmarch’, ‘bookshop’, ‘windowcleaner’ na ‘hardship’ yanajitokeza kama mashina na kama viini pia. Hata hivyo tunazidi kusisitiza kuwa dhana ya ‘base’ inavyotumika katika uchambuzi wa sarufi ya Kiingereza ni tofauti kabisa na dhana hiyo inavyoweza kutumika katika lugha ya Kiswahili. Tunasisitiza kuwa katika sarufi ya Kiswahili dhana ya kiini ni sawa na dhana ya mzizi; kitu ambacho sivyo katika lugha ya Kiingereza. Kwa kuwa katika ufafanuzi huu tumegusia dhana ya mpaka baina ya dhana hizi ni vema sasa katika sehemu inayofuata tuingie katika mjadala mwingine ambao unahusu mpaka baina ya mzizi/kiini na shina.

4.0 Mpaka baina ya Shina na MziziKuna fasili kadha wa kadha za shina na mzizi ambazo tukizichunguza kwa undani tutagundua kwamba zinajaribu kuweka mpaka baina ya dhana hizi mbili. Miongoni mwa fasili, au tuseme sifa pambanuzi, za dhana hizi ni kama ifuatavyo:

4.1 Hoja pambanuzi za Mzizi:(1) Ni sehemu ya neno ambayo huhusika na uundaji wa neno jipya.(2) Ni kiini cha neno ambacho hupambanuliwa na mofolojia

ya mnyambuliko.(3) Ni ni kiini cha neno kinachoishia na konsonanti.(4) Ni ni sehemu ya neno isiyobadilika.(5) Ni sehemu ya neno isiyoweza kuchanganuliwa zaidi.

4.2 Hoja pambanuzi za shina:(1) Ni sehemu ya neno ambayo haiwezi kuunda neno jipya.(2) Ni umbo la neno ambalo hupambanuliwa na mofolojia ya uambatishi.(3) Ni kiini cha neno kinachoishia na irabu.(4) Ni umbo la neno lenye mzizi na angalau kiambishi kimoja.

Tuanze mjadala wetu kwa kujadili kwa pamoja hoja za pande mbili lakini zinazoendana. Tuanze na hoja katika kipengee cha 4.1.1 na 4.1.2 zilizojumuishwa kama ifuatavyo:

4.1.1/2 Mzizi huunda neno jipya na hupambanuliwa na mofolojia ya mnyambuliko4.2.1/2 Shina haliwezi kuunda neno jipya na hupambanuliwa na

mofolojia ya uambatishi.

Mofolojia kama taaluma inayohusu uchanganuzi wa maumbo ya maneno na ufafanuzi wa maana ya kisarufi ya maumbo hayo, imethibitika kuwa na matawi mawili (taz. Mgullu, 1999; Kihore na wenzie, 2004) ambayo yameainishwa kwa vigezo tofautitofauti.

Tukianza na Mgullu (1999: 96) anaeleza kuwa kuna mofolojia ya mnyambuliko wa maneno ambayo anasema tafsiri yake kwa Kiingereza ndiyo

Page 8: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

MKANGANYIKO WA DHANA ZA MZIZI, KIINI NA SHINA KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI 19

‘inflectional morphology’ na mofolojia ya uundaji wa maneno aiitayo ‘derivational morphology’. Tukichunguza kwa makini fasili hii ya Mgullu tutagundua kuwa inaeleza aina moja tu ya mofolojia ambayo ni mofolojia ya mnyambuliko. Hii ni kwa sababu mofolojia ya mnyambuliko ni tawi ambalo huhusu uundaji wa maneno mapya, yaani kwa neno kubadili kategoria yake ya awali au kwa kubadili maana ya awali hata kama ni kimwelekeo tu (taz. Lyons, 1968; Rugemalira, 1998; Kahigi, 2003; na wengineo). Ni wazi pia kuwa tawi la ‘inflectional morphology’ ambalo hapa tutaliita ‘mofolojia ya uambatishi’ halihusu uundaji wowote wa neno. Tawi hili huhusu uambishaji wa maneno kwa kuweka viambishi mbalimbali kama vile vya idadi (number), uhusika4 (case), jinsi (gender), njeo (tense), hali (mood), n.k katika kiini cha neno (Ling. Lyons, 1968).

Aidha, kuhusu dhana ya shina Mgullu (1999: 104), naamini amepotoshwa katika fasili yake ya shina, anaeleza kuwa: “shina ni sehemu ya neno ambayo hutumiwa kuundia neno jipya”. Anatoa mifano ifuatayo ya shina:

7. Neno shinautotoni {toto}kuimba {imb}wapiganaji {pig}

Fasili hii na mifano yake inapaswa kukaziwa macho. Ni wazi kuwa Mgullu anachojaribu kueleza hapa kinaihusu dhana ya mzizi na sio shina kama anavyodai.

Naye Kihore na wenzie (2004: 89-93) wanaeleza kuwa kuna matawi mawili ya uambishaji au mofolojia ambayo ni uambishaji-nyambulishi (derivational) na uambishaji-kisarufi (inflectional). Kati ya haya, ni tawi la uambishaji-nyambulishi ndilo huhusishwa na kuunda neno jipya. Hivyo wanalihusisha na dhana ya mzizi. Kwa maelezo yao ni kuwa uambishaji-kisarufi hauundi neno jipya na huhusu sana dhana ya shina. Aidha, wanaeleza kuwa wataalamu wa isimu wanaelekea kukubaliana kuwa dhana za shina na mzizi zinaweza kutofautishwa kwa utaratibu wa uambishaji ambao ama unaweza kuunda au kutounda neno jipya.

Hebu tupitie mifano mbalimbali inayotolewa na Kihore na wenzie katika kushadidia hoja yao. Wanatoa mifano ifuatayo kutofautisha dhana ya shina na mzizi:

8. (a)(b)

walkkick

- walks - kicks

- walked- kicked

(c) show- shows - showed(d)(e)

killnation

- kills-

- killed- nations (uk. 84)

4Viambishi kama uhusika na jinsi havimo katika lugha ya Kiswahili. Hivi vinapatikana katika lugha za Ulaya Magharibi na Ulaya-Mashariki na Kati. Ingawa wanaisimu kama Guthrie (1970) walijaribu kuhusisha dhana ya jinsi na ngeli za majina ni bayana kuwa kidhima dhana hizi ni tofauti sana (ling. Johannes, 2007).

Page 9: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

20 KISWAHILI JUZ. 74

Kwa mujibu wa Kihore na wenzie kikoa cha kwanza cha maneno katika 8(a-e) ni shina la vikoa vinavyofuata; sababu inayotolewa hapa ni kuwa maana ya msingi ni ileile hivyo hakuna neno jipya lililoundwa. Tunakubaliana na hoja hii katika mahali pa kwanza. Hata hivyo tukipanua data hiyo na kuwa na maneno kama ‘walker’, ‘killer’ n.k tunaona kuwa, pia kulingana na maelezo ya Kihore na wenzie, hapa neno ‘kill’ na ‘walk’ yanabadilisha uamilifu wake wa kisarufi kuwa ni mzizi kwa sababu yamebadili kategoria ya neno kutoka kitenzi kuwa nomino. Swali la msingi hapa ni kuwa mbona neno lilelile, ‘kill’ au ‘walk’ liwe na sifa ya kuwa mzizi na shina? Swali hili ndilo hasa kiini cha mjadala wa mpaka baina ya dhana hizi mbili. Tuangalie mkanganyiko mwingine unaojitokeza katika data (9):

9. (a)(d)

pigaa-ta-pig-a

(b) pig-w-a (e) a-li-pig-a

(c) a-ta-pig-a(uk. 84)

Kwa mujibu wa Kihore na wenzie umbo piga katika (9) ni shina. Hiyo ni sahihi tu katika 9 (a), (c)-(e) kwa sababu 9 (b) imebadili mwelekeo wa maana kutoka kuzungumzia mtenda kwenda kwa mtendwa japo kategoria ya neno ni ileile. Hivyo 9(b) haikupaswa kuwepo katika data hii inayoeleza piga kama shina wakati kuna kiambishi –w- cha utendwa kati ya konsonanti ya mwisho ya mzizi na irabu ishilizi. Kwa kuongezea zaidi, neno pig-w-a halihusiani na uambishaji wa kisarufi (inflectional) walioueleza au kwa maneno mengine halijaundwa na shina piga bali mzizi pig-. Viambishi vyote vya kauli vinahusiana na mofolojia ya mnyambuliko/uambishaji-nyambulishi wa vitenzi (verb to verb derivation). Hii ni kusema kuwa viambishi vya kauli hubadili mwelekeo wa maana ya msingi ya neno tofauti na mofolojia ya uambatishi (ling. Polomé, 1967; Kahigi, 2003; Rugemalira, 2005).

Matatizo ya mpaka wa uchanganyaji aina za mofolojia yanajitokeza tena katika mifano ya Kihore na wenzie (2004: 84):

10. (a) godoro (e) ma-taifa(b) ma-godoro (f) vi-taifa(c) kijigodoro (g) ji-taifa

(d) taifa

Kihore na wenzie wanaona kuwa maumbo godoro na taifa ni mashina kwa sababu tu kategoria ya neno imebaki kuwa ileile na pia maana ya msingi ni ileile. Ili kujibu madai haya tupanue data mojawapo walau ya umbo taifa, ili kuona ukweli wa madai yao:

11. (a) taifa (e) ji-taifa(b) ma-taifa (f) u-taifa(c) vi-taifa (g) u-taif-ish-a-ji(d) ki-taifa

Page 10: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

MKANGANYIKO WA DHANA ZA MZIZI, KIINI NA SHINA KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI 21

Tukichunguza data yetu katika 11(a-g) tutaona wazi kuwa mifano hii inahusu nomino. Ingawa kategoria haijabadilika lakini tutakubaliana kuwa umbo taifa, kama ilivyo kwa godoro katika 10 (a-c) ni mzizi na siyo shina. Sababu moja inayothibitisha kuwa ni mzizi ni kuwa maumbo godoro na taifa katika mifano 10 na 11 yanahusiana na mofolojia ya mnyambuliko (Noun to Noun derivation/ derivation by noun class changing, ling. Katamba, 1993; Kiango, 2000; Kahigi, 2003). Hivyo basi taifa >vi-taifa>u-taifa>u-taifisha-ji ni ngeli tofauti za majina. Halikadhalika kwa godoro>vi-ji-godoro. Sababu ya pili ni kuwa maneno yote mawili, tukiondoa mfano wa 11(g), hayawezi kuchanganuliwa zaidi. Kwa kuwa nomino taifa na kitenzi taifisha yameingizwa kama vidahizo tofauti kabisa katika kamusi (taz. TUKI-Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza) jambo linalotupa mashaka kuendelea kudhani kitenzi taifisha kinatokana na nomino taifa ingawa ni kweli maneno yote yana asili moja ya Kiarabu. Kuna haja ya kuchunguza zaidi juu ya tafsiri sahihi ya neno taifisha kuwa ni ‘nationalize’ au ‘confiscate’. Hoja yetu inafaulu kwa mfano rahisi wa siasa za wazalendo na wapinzani wa Mugabe kule Zimbabwe. Mashamba ya wazungu yaliyochukuliwa na serikali na kugawiwa wazawa hayafanywi kuwa mali ya taifa ‘nationalized’ bali ‘yametaifishwa ‘confiscated’ na kugawiwa wazawa na si mali ya serikali tena.

Hoja nyingine tunayoitoa kuhusu neno taifisha kwamba linapaswa kuwa katika ruwaza nyingine ni kwamba kitenzi ‘taifisha’ kiko katika kauli ya utenda kama vilivyo vitenzi, ‘tundika’, ‘fundisha’3 n.k. Vitenzi vya jinsi hii, (yaani taifisha, na fundisha) katika mizania ya lugha za Kibantu (ling. Good, 2007), vinarejelewa kuwa vina usababishi-hadai (pseudo-causative) maana yake ni kwamba vinadhaniwa kuwa vina kiambishi cha kauli ya utendesha na kuwa viko katika utendesha kumbe siyo! Kwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala ya u-taif-ish-a-ji.

Mkanganyiko wa mpaka baina ya aina mbili za mofolojia tuliouona hapo juu unaongeza utata zaidi katika mjadala wa mpaka wa dhana za shina na mzizi. Ni wazi kuwa hatuwezi kukubali moja kwa moja hoja kwamba mashina yote katika lugha ya Kiswahili hayawezi kuundia neno jipya na tena kwamba mizizi yote inaweza kuunda maneno mapya. Tuchunguze data ifuatayo katika (12) na (13) ili kubaini tunachosema:

12. Shina (T) Neno jipya (N)(a) chunga wa-chunga-ji(b) cheza wa-cheza-ji(c) soma m-soma-ji(d) imba w-imba-ji(e) ziba mki-zib-o

3Hapa nachukulia kuwa kitenzi “fundisha” pia kiko katika kauli ya kutenda na hakitokani na kitenzi ‘funda’. Vitenzi ‘funda’ na ‘fundisha’ vinaingizwa kama vidahizo viwili tofauti, taz. TUKI (1990).

Page 11: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

22 KISWAHILI JUZ. 74

(f) hama ma-ham-e(g) langua m-langu-zi(h) shinda u-shind-i(i) sifu sif-a

13. (a) mama(b) homa(c) i-pi(d) ki-le

Katika mifano 12(a-d) maumbo yaliyokolezwa wino ni mashina na katika 12(e-i) maumbo yaliyokolezwa wino ni mizizi. Tofauti na inavyodaiwa, mifano katika 12(a-d) inadhihirisha wazi kuwa mashina ya vitenzi yanaweza kuambikwa vijenzi (mofu –ji) na kuunda neno jipya ambalo ni la kategoria ya nomino. Hali kadhalika uundaji huu wa maneno mapya kwa njia ya mashina ya vitenzi unahusu mofolojia ya mnyambuliko na siyo uambatishi. Mifano katika 13(a-d) nayo inapingana wazi na dhana kuwa mizizi yote ina uwezo wa kuunda neno jipya na kuwa inahusu mofolojia ya mnyambuliko tu. Ni bayana pia kwamba mifano katika 13(c-d) ni mizizi inayohusiana na dhana ya uambishaji wa kisarufi (uambatishi).

4.1.3 Mzizi ni kiini cha neno kinachoishia na konsonanti4.2.3 Shina ni kiini cha neno kinachoishia na irabuHoja ya umbo la mzizi inapaswa kuchunguzwa kwa jicho angavu. Sababu ni kwamba hoja yenyewe kwa upande mmoja ni sahihi na kwa upande mwingine siyo sahihi. Ni sahihi kwa sababu ni kweli kuwa mizizi mingi ya vitenzi vya Kiswahili huishia na konsonanti. Hata hivyo si kweli kuwa wakati wote mizizi huishia na konsonanti na mashina huishia na irabu. Tuangalie mifano katika (14) ili kuthibitisha hoja hii:

14. (a) hubiri (T) wa-hubiri (N)(b) sinzi-a (T) u-sin-gi-zi?(N) u-sinzi-a-ji(c) tembea (T) ma-tembe-zi(d) kimbia (T) m-kimbi-zi/ m-kimbi-a-ji(e) wewe (W)(f) lazima (Ts)

Mifano katika 14(a-f) inatuthibitishia kuwa ipo mizizi mingi katika lugha ya Kiswahili inayoishia na irabu. Kuhusu hoja ya umbo la shina ni wazi kuwa shina linaweza pia kuishia na konsonanti kama inavyooneshwa katika 15(a)-(d):

15. (a) shikish - katika shikisha(b) pigw- katika pigwa(c) kimbiz - katika kimbiza(d) kalik - katika kalika

Page 12: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

MKANGANYIKO WA DHANA ZA MZIZI, KIINI NA SHINA KATIKA MOFOLOJIA YA KISWAHILI 23

Ikumbukwe kwamba mashina katika 15(a)-(d) yanaundwa na mzizi na kiambishi kimoja cha kauli. Kwa mfano, katika (15) mizizi ni shik-, pig-, kimbi-, na ka-mtawalia. Ni wazi kuwa si mashina yote huishia na irabu kama tuonavyo hapo juu. Tunapaswa kuzingatia kuwa mashina yanaweza kuundwa pia na miambatano ya mizizi (taz. Katamba, 1993; Kiango, 2000; Kihore na wenzie, 2004).

4.1.4 Mzizi ni sehemu ya neno isiyobadilika

Kwa mwanaisimu yeyote anayeifahamu vizuri sarufi ya Kiswahili akiulizwa kuthibitisha ukweli wa hoja katika § 4.1.4 atajibu ndio na hapana kwa wakati mmoja. Ili tufahamikiwe vizuri juu ya hoja hii tuabiri mifano katika (16) na (17):

16. (a) chez-a chez-e-a(b) za-a za-li-a(c) samba-asamba-z-i-a

17. (a) pend-a m-penz-i(b) Pand-am-panz-i(c) lind-a m-linz-i(d) suk-a m-sus-i(e) chek-a m-chesh-i(f) pik-a -pish-i

chez-esh-aza-lish-asamba-z-a

Mifano katika 16 (a-c) inathibitisha upande mmoja wa hoja kuwa kuna maneno ya Kiswahili ambayo mizizi yake haibadiliki. Lakini mifano katika 17(a-f) inathibitisha hoja kwa upande mwingine kuwa kupitia michakato ya kimofofonolojia mizizi huweza kuathiriwa na kuchukua umbo jingine ambalo ni la nje (ling. Katamba, 1993, Kahigi, 2003; Schadeberg, 2005; Massamba, 2004).

5.0 HitimishoTunaweza kuhitimisha hoja yetu kwa kukubaliana kuwa hoja na 4.1.5 ni sahihi zaidi katika kueleza dhana ya mzizi na shina. Ni ukweli usiopingika kuwa mzizi ni kiini cha neno ambacho hakiwezi kuchanganuliwa zaidi bila kupoteza uamilifu wake kisarufi. Kuhusu fasili ya shina tunaweza kusema kuwa shina ni sehemu ya neno ambayo inaundwa na mzizi na kiambishi angalau kimoja au na muambatano wa mizizi katika maneno ambatani.

Page 13: mwalimuwakiswahili.co.tz  · Web viewKwa maelezo hayo tunahitimisha hoja yetu kwa kuligawa neno hili kimofolojia kama u-taifish-a-ji (Kiambishi awali-mzizi-viambishi fuatishi) badala

24 KISWAHILI JUZ. 74

MAREJEO

Bauer, L. (1983). English Word-Formation. Cambridge . Cambridge University Press. Good, J. (2005) “Reconstructing morpheme order in Bantu: The case of

causativization and applicativization”. Katika Diachronica 22.3–57.Good, J. (2007). “Slouching towards deponency: A family of mismatches in the Bantu verb

stem”. Proceedings of the British Academy, Volume 145.Hartman, R. (1972). Dictionary of Language and Linguistics. London. Applied Science

Publishers.Johannes, J.G. (2007). “The Ki-Nata Noun Structure”. Unpublished M.A Dissertation.

University of Dar es Salaam

Kahigi, K. K. (2003). “The Sisumbwa Noun: Its Classes and Derivation”. In Occasional Papers in Linguistics. No.1. pp.1-86. University of Dar es Salaam: LOT Publications.

Katamba, F. (1993). Morphology. Macmillan Press Limited. London.Kihore na wenzake (2004) Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu. TUKI. Dar es Salaam. Kiango, J.G. (2000). Bantu Lexicography: a Critical Survey of the Principles and Process of

Constructing Dictionary Entries. Institute for the Study of Languages and Cultures of Asia and AfricaTokyo University of Foreign Studies. Japan.

Lyons, J. (1968). Introduction to Theoretical Linguistics. Cambridge. Cambridge University Press. United Kingdom.

Massamba D.P.B. (2004). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. TUKI, Dar es Salaam.-------------------- (1996) Phonological Theory: History and Development. Dar

es Salaam: Dar es Salaam University Press.Meeussen, A.E. (1967). Bantu grammatical reconstructions. Tervuren: Tervuren.Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili.

Longhorn Publishers, Nairobi.Mohamed, M.A. (1993). Sarufi Mpya. Press and Publicity Centre. Dar es Salaam.

Mwansoko, J.M. (2006). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. TUKI.Dar es Salaam.

Polomé. E. C. (1967). Swahili Language Handbook. 1717 Massachusetts Avenue: Centre for Applied Linguistics.

Rugemarila, J. M. (2005). A Grammar of Runyambo. Dar es Salaam: Languages of Tanzania (LOT).

Schadeberg T. C. (1995). “Spirantization and the 7-to-5 Vowel Merger in Bantu” katika Belgian Journal of Linguistics. Vol. 9. pp. 73-84

Taasisi ya Elimu (1996). Kiswahili Kidato Cha Pili. Oxford University Press. Tanzania. TUKI (1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Dar es

Salaam