8
Taarifa kwa Vyombo vya Habari, 22 Machi 2015 SERIKALI INAPASWA KUMALIZA TATIZO SUGU LA UKOSEFU WA DAMU SALAMA NCHINI Sikika inasikitishwa na taarifa za kukosekana kwa damu salama katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Damu salama ni moja kati ya dawa muhimu kwa kuwa inakidhi vipaumbele vya afya katika jamii kama ilivyobainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Ni dawa muhimu na ya kipekee kwa kuwa pindi inapohitajika kutumika hakuna mbadala wala haiwezi kutengenezwa kiwandani. Hivyo, uwepo wa damu salama katika hospitali zetu ni jambo la lazima. Nchini Tanzania, Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) uliopo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, una wajibu wa kuhamasisha watu ili kujitolea damu. Vile vile, mpango huu una wajibu wa kuhakikisha kuwa damu salama pamoja na bidhaa zitokanazo na damu zinapatikana katika vituo vyenye dhamana ya kutoa huduma za damu. 1

Sikika- Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Embed Size (px)

DESCRIPTION

SERIKALI MALIZA TATIZO LA UKOSEFU WA DAMU SALAMA NCHINI

Citation preview

Page 1: Sikika- Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Taarifa kwa Vyombo vya Habari, 22 Machi 2015

SERIKALI INAPASWA KUMALIZA TATIZO SUGU LA

UKOSEFU WA DAMU SALAMA NCHINI

Sikika inasikitishwa na taarifa za kukosekana kwa damu salama katika vituo

vya kutolea huduma za afya nchini. Damu salama ni moja kati ya dawa

muhimu kwa kuwa inakidhi vipaumbele vya afya katika  jamii kama

ilivyobainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Ni dawa muhimu na ya

kipekee kwa kuwa pindi inapohitajika kutumika hakuna mbadala wala haiwezi

kutengenezwa kiwandani. Hivyo, uwepo wa damu salama katika hospitali zetu

ni jambo la lazima.

Nchini Tanzania, Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) uliopo chini ya

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, una wajibu wa kuhamasisha watu ili

kujitolea damu. Vile vile, mpango huu una wajibu wa kuhakikisha kuwa damu

salama pamoja na bidhaa zitokanazo na damu zinapatikana katika vituo

vyenye dhamana ya kutoa huduma za damu.

                                  

Ijapokuwa NBTS imeweza  kuongeza upatikanaji wa damu salama kutoka

chupa 12,500 (2005) hadi chupa 160,000 (2013) kwa mwaka, hata hivyo,

ukusanyaji wa damu bado upo chini ya mahitaji halisi ya nchi ambayo ni kati

ya chupa 400,000 hadi 450,000 kwa mwaka kwa mujibu wa Shirika la Afya

duniani. NBTS imekuwa ikikusanya takribani asilimia 38 tu ya mahitaji ya

damu salama nchini kwa mwaka, hivyo kusababisha upungufu wa kudumu wa

damu salama katika vituo vyenye dhamana ya kutoa huduma za damu nchini.

1

Page 2: Sikika- Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Kumekuwepo na taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kwa majuma

kadhaa sasa, kuhusu upungufu mkubwa wa damu katika vituo vyenye

dhamana ya kutoa huduma za damu nchini. Uhitaji wa damu salama nchini ni

mkubwa kutokana na kuongezeka kwa tatizo la upungufu wa damu mwilini

unaosababishwa na malaria na matatizo ya uzazi hasa wakati wa ujauzito na

kujifungua. Tanzania ni moja kati ya nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara

zenye idadi kubwa ya vifo vya watoto na wanawake. Inakadiriwa kuwa karibu

asilimia 28-30 ya vifo vya kina mama vinatokana na upungufu wa damu

mwilini. Hii inaweza kuonekana katika matumizi ya damu salama nchini

ambayo karibu asilimia 80 ya damu inayokusanywa inatumika kwa wanawake

na watoto, wakati asilimia 20 inatumika kwa matumizi mengine kama

upasuaji, ugonjwa wa selimundu (sickle cell anaemia) na tiba ya saratani. Kwa

hiyo upatikanaji wa damu salama kwa wakati unazuia kuongezeka kwa

ugonjwa na hata vifo na hivyo kuboresha afya za wananchi.

Ni kutokana na umuhimu huu wa damu salama, Sikika iliamua kuangalia kwa

undani ukubwa wa tatizo hili, sababu na namna linavyoweza kutatuliwa ili

kuboresha upatikanaji wa damu salama nchini.

Katika utafiti wetu tulibaini kuwa, kuna upungufu mkubwa wa damu salama

katika vituo vingi vya kutolea huduma hiyo. Kwa mfano katika wilaya ya

Simanjiro, mahitaji ya damu salama kwa mwaka ni chupa 145 hata hivyo

wamekuwa wakipokea chini ya nusu ya mahitaji yao. Mwaka 2013 walipokea

chupa  74 tu, na kati ya mwezi Februari na Machi mwaka huu hawakuwa na

akiba kabisa kwani mara ya mwisho kupokea damu ilikuwa mwezi Septemba

mwaka 2014.

2

Page 3: Sikika- Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Hali hiyo pia ilionekana katika wilaya ya Mpwapwa, ambapo kati ya mwezi

Februari na Machi 2015 hawakuwa na akiba ya damu salama. Mahitaji yao

kwa mwaka ni chupa 1,400, hata hivyo wamekuwa wakipokea wastani wa

chupa 20 kwa mwezi ambazo ni sawa na chupa  240 tu kwa mwaka ikiwa ni

mara 6 pungufu ya mahitaji yao.

Kwa  mkoa wa Dar es salaam, hali ni kama ilivyo katika mikoa mingine

ambapo, vituo vyote vilivyotembelewa vilikutwa na upungufu mkubwa wa

damu salama kutokana na kupatiwa damu pungufu na NBTS. Kwa mfano,

hospitali ya Wilaya ya Temeke imekuwa ikipokea  damu salama inayokidhi

mahitaji ya hospitali kwa asilimia 20% tu kwa mwaka, huku hospitali ya

Amana ikiwa inapatiwa asilimia 40% tu ya mahitaji yake.  Hospitali ya Taifa

Muhimbili, ambayo imekuwa ikishugulikia mgonjwa  makubwa na sugu, nayo

imekuwa  ikipatiwa damu salama kwa takribani asilimia 50 - 60 ya mahitaji

yake. Uhaba wa damu salama umekuwa sugu nchini kote kutokana na kuwa

vituo vyote vinategemea NBTS katika kupatiwa bidhaa hiyo.

Sikika inatambua na inaamini  Serikali inatambua kuwa, chanzo kikubwa cha

uhaba sugu wa damu salama nchini ni upungufu wa fedha unaoikabili NBTS.

Hii inasababisha NBTS kushindwa kutekeleza majukumu yake muhimu kama

vile kufanya kampeni za kuhamasisha wananchi kuchangia damu kwa hiari

pamoja na kununua vitendanishi vya kutosha kwa ajili ya kupima, kuhifadhi

na kutengeneza bidhaa zingine zitokanazo na damu salama. Kwa takribani

miaka 10,  bajeti ya NBTS kwa  zaidi ya asilimia 80% imekuwa ikitoka kwa

wafadhili, hususani Serikali ya Marekani, kupitia Mpango wa dharura wa

UKIMWI (PEPFAR) ambao wamekuwa wakipunguza ufadhili wao unaofikia

kikomo mwaka huu 2015. Serikali imekuwa ikichangia asilimia 20 tu ya bajeti

3

Page 4: Sikika- Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

ya NBTS  huku ikishindwa kuziba pengo lililokuwa linaachwa na wafadhili,

jambo ambalo ndio chanzo kikubwa cha NBTS kushindwa kukusanya damu

salama ya kutosha nchini. Kwa mfano, Mahitaji ya damu salama nchini ni

chupa 100,000 hadi 112,000 kwa muhula kiasi ambacho NBTS imeshindwa

kukusanya hata nusu ya kiasi hicho. Mathalani, katika kipindi cha mihula

miwili iliyopita (Oktoba – Disemba 2014 na Januari – Machi 2015), NBTS

imeweza kukusanya kiasi cha chupa 34,000 tu ambacho ni sawa na asilimia 17

ya mahitaji ya damu salama kwa kipindi hicho.

Kushindwa kwa NBTS kukusanya damu salama ya kutosha, kumepelekea

baadhi ya vituo vya huduma kutumia damu wanayoikusanya kutoka kwa

familia, ndugu na jamaa za wagonjwa badala ya kuipeleka katika vituo vya

kanda au taifa kwa ajili ya kupima, kuhifadhi na kutengeneza bidhaa zingine

zitokanazo na damu salama. Hii ni hatari kiafya, kwani huweza kusababisha

maambukizi ya magonjwa na pia kuchangia matumizi mabaya ya damu kwa

kuwa vituo vya huduma havina mashine na utaalamu wa kutosha hususani

katika kutengeneza bidhaa zingine zitokanazo na damu.

Kama ilivyo kwa bidhaa zingine,  uhaba wa damu salama kwa kiasi kikubwa

umekuwa ukisababisha baadhi ya watoa huduma za afya kujihusisha na

vitendo vya rushwa - ‘’kuuza damu kwa wagonjwa’’ kutokana na ongezeko la

mahitaji ya damu huku upatikanaji wake ukiwa ni mdogo.

Sikika, tumefurahishwa na tunapongeza jitihada za wadau mbalimbali kama

taasisi za kidini na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuandaa kampeni

za kukusanya damu. Jitihada hizi ni nzuri katika kutatua tatizo kwa muda

4

Page 5: Sikika- Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

mfupi lakini kunahitajika mpango endelevu ambao utaiwezesha NBTS

kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Tunaitaka Serikali kuwajibika katika kutatua tatizo la damu salama nchini. Ni

jukumu la Serikali kuiwezesha NBTS kifedha badala ya  kutegemea wafadhili

na watu binafsi. Serikali ipange bajeti inayotosha pamoja na kutoa fedha kwa

wakati kwa Mpango huu ili kuuwezesha kukusanya na kusambaza damu

salama inayokidhi mahitaji ya nchi. Tunaamini kuwa, iwapo Mpango wa

Taifa wa Damu Salama utakuwa na fedha za kutosha na zinazotolewa kwa

wakati hakutakuwa na Upungufu wa damu salama nchini.  

Mr. Irenei Kiria, Mkurugenzi wa Sikika, S.L.P 12183 Dar es Salaam,Simu: +255 222 666355/57, Nukushi: 2668015, Barua pepe: [email protected],

Twitter: @sikika1, Facebook: Sikika Tanzania, Tovuti: www.sikika.or.tz

5