Upload
others
View
10
Download
0
Embed Size (px)
Citation preview
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Wizara ya Fedha
Dar es Salaam
Aprili, 2011
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
1
Dibaji
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilizinduliwa rasmi tarehe 26 Machi, 1999 kuwa Wakala wa Serikali
(Executive Agency) kwa mujibu wa Sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997.
Kabla ya Uhuru, Takwimu zilikuwa zinakusanywa kwa kutumia sheria ya Takwimu ya mwaka
1949 (Statistics Ordinance of 1949 – chapter 443). Sheria hii ilikuwa inatumika katika nchi za
kikoloni za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Uganda na Tanganyika. Kupitia sheria hii, Idara ya
Takwimu ya Afrika Mashariki ilipewa mamlaka ya kuratibu mfumo (Muundo) wa takwimu za
uchumi na jamii wa nchi tatu.
Baada ya Uhuru mwaka 1961, mamlaka ya kukusanya, kuhifadhi na kuchapisha takwimu
yalitokana na sheria ya Takwimu Na. 33 ya mwaka 1961; Sheria ambayo nayo ilifutwa kwa Sheria
ya Takwimu Na. 1 ya mwaka 2002. Kutokana na Sheria hiyo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu imepewa
majukumu ya kuendesha, kusimamia na kuratibu shughuli zote za kitakwimu Tanzania Bara. Hivi
sasa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ipo kwenye mchakato wa kupata sheria mpya ikiwa ni sehemu ya
Mpango Mkakati wa Kuboresha na kuimarisha Takwimu Tanzania.
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kamati ndogo iliyoundwa kutayarisha kitabu hiki.
Dkt. Albina A. Chuwa
MKURUGENZI MKUU
OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
2
1. Utangulizi
Tanzania ilianza kuwa na Ofisi ya Takwimu mara tu baada ya Uhuru mwaka 1961. Kabla ya
Uhuru Ofisi hii ilikuwa Nairobi, Kenya. Ofisi ya Takwimu ilipitia mabadiliko mengi hadi
kufikia kuitwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (National Bureau of Statistics - NBS) iliyozinduliwa
rasmi tarehe 26 Machi, 1999 kuwa Wakala wa Serikali (Executive Agency) kwa mujibu wa
Sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997. Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikiwa chini
ya Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango iliundwa kutokana na iliyokuwa Idara Kuu ya Takwimu
(Central Bureau of Statistics) ambayo ilikuwa inafanya kazi chini ya Sheria ya Takwimu Na.
33 ya mwaka 1961 (Statistics Ordinance No. 33 of 1961), Sheria ambayo nayo ilifutwa kwa
Sheria ya Takwimu Na. 1 ya mwaka 2002.
2. Historia ya Takwimu Kabla ya Uhuru ( mwaka 1946 - 1961)
Historia ya Takwimu Tanzania Bara ilianza toka wakati wa Wakoloni walipokuwa
wakitutawala. Kwa bahati mbaya taarifa za wakati huo hazikuweza kuhifadhiwa na hivyo
hatujui ni namna gani waliendesha shughuli za kitakwimu hapa nchini. Lakini kutokana na
uwekaji wa kumbukumbu za kihistoria kama nyingine zilivyo, hili limekuwa ni pengo kubwa
ambalo linahitaji kuzibwa. Kitengo cha Takwimu kilianzishwa mwaka 1946 chini ya “East
African Governors‟ Conference” na ofisi yake ilikuwa na makao yake huko Nairobi, Kenya.
Katika kipindi hicho takwimu zilikuwa zikikusanywa na wataalam kutoka Nairobi na
uchambuzi wake ulifanyika huko huko. Baada ya kuanzishwa kwa “East African High
Commission”, kitengo hiki kilibadilishwa jina na kuitwa “East African Statistical Department”.
Idara hii ilikuwa inawajibika kwa kazi zifuatazo:
Kuhakikisha wanatoa machapisho ya kitakwimu kama Serikali za Kikoloni za
Wajerumani na Waingereza walivyokuwa wanatoa siku za nyuma,
Kufanya uchambuzi wa matokeo ya Sensa na tafiti mbalimbali ambazo ziliandaliwa na
„East African Statistical Department‟, na
Kuandaa mfumo wa takwimu.
Ili kuhakikisha shughuli za kitakwimu zinaendelea vizuri hapa Tanganyika, ilibidi kufunguliwa
ofisi mwezi Januari, 1949 hapa Dar es Salaam, ingawa Ofisi ya Nairobi bado ilikuwepo.
Mnamo mwaka 1954/55, Ofisi ya Dar es Salaam ilibadilishwa jina na kuitwa „Tanganyika
Unit‟. Kuanzia wakati huo ofisi hii iliongezewa majukumu mbalimbali ya ukusanyaji na
uchambuzi wa takwimu.
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
3
3.0 Historia ya Takwimu Baada ya Uhuru
3.1 Muundo wa Taasisi Ulivyobadilika Tangu Mwaka 1961
Baada ya kupata Uhuru mwaka 1961, Kitengo hiki kilianzishwa chini ya Hazina kutoka
iliyokuwa “Tanganyika Unit of East African Statistical Department, Nairobi” na kuwa
„Statistics Division‟ chini ya Hazina na ofisi zake zilikuwa katika jengo hilohilo la Hazina.
Baada ya mabadiliko hayo, Mtakwimu Mkuu wa kwanza alikuwa raia wa Uingereza
aitwaye Nd. D.C. Upton, na aliongoza ofisi hii mpaka mwaka 1964. Hata hivyo, mnamo
mwaka 1962, jina la ofisi hii lilibadilishwa na kuwa Maktaba ya Takwimu „Central
Statistical Bureau (CSB)‟. Nd. C. Patel, ndiye aliyeiongoza CSB kuanzia mwaka 1964 hadi
mwaka 1966 na baadae Nd. D.D. Johnson alikaimu kama Mtakwimu wa Serikali. Ofisi hii
CSB ilibaki kuwa chini ya Hazina mpaka mwaka 1964, ambapo ilihamishiwa chini ya Ofisi
ya Rais na Baraza la Mawaziri. Baada ya uhamisho huo, Ofisi hii ilihamia jengo la
Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Mtaa wa Kivukoni Front, ghorofa ya kwanza.
Mnamo mwaka 1966, CSB ilibadilishwa jina na kuitwa „Central Bureau of Statistics
(CBS)‟, na kuwa chini ya Wizara ya Uchumi na Mipango. Baada ya mabadiliko hayo Ofisi
hii ilihama toka jengo la “Exchequer and Audit Department” na kuhamia jengo la Lehman
ghorofa ya kwanza katika jengo la Clock Tower, kwenye makutano ya Samora Avenue na
Mission Street. Dkt. G. Jacobsson, raia wa Sweden ndie alikuwa anaongoza CBS kama
Mtakwimu wa Serikali.
Mwaka 1967, kulifanyika sensa ya watu ya kwanza baada ya Uhuru kwa maana hiyo
kulihitajika nafasi ya kutosha kwa ajili ya kazi ya uchambuzi wa Sensa ya Watu ya mwaka
1967. Hivyo, Kitengo cha Sensa ya watu kilihamia Mtaa wa Mkwepu No. 9 na mpaka leo
bado jengo hilo linatumika na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Kuanzia mwaka 1970 mpaka 1973, Ndugu Joshua J. Mpogolo
alikuwa Msimamizi Mkuu wa tatu tokea tulipopata Uhuru mwaka
1961 na kuwa na cheo kilichoitwa Mkurugenzi wa Takwimu. Yeye
ndie alikuwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hii. Mnamo
mwaka 1974, jina la CBS lilibadilishwa na kuwa „Bureau of
Statistics (BOS)‟.
Ndugu Joshua J. Mpogolo
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
4
Mwaka 1974/75 Wizara ya Uchumi na Mipango iliunganishwa na Wizara ya Fedha na BOS ikawa Idara
katika Wizara ya Fedha na Mipango. Ofisi zake zilikuwa jengo la Casino, Mtaa wa Kivukoni na cheo cha
Ndugu J. J. Mpogolo kilibadilishwa na kuwa Kamishina wa Takwimu. Kuanzia mwaka 1980 mpaka 1986,
Idara hii ilihamishiwa tena Wizara ya Mipango na Uchumi baada ya mabadiliko ya wizara hizi kati ya
mwaka 1986 – 1989 na baadae tena ikawa chini ya Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango.
Kuanzia mwaka 1990, BOS ilikuwa chini ya Tume ya Mipango. Mnamo
mwaka 1980 mpaka 1998, BOS iliendelea kutumia majengo ya Casino
ambapo Ndugu Nathanael K. Mbalilaki alikuwa Msimamizi Mkuu wa
nne kama Mtakwimu Mkuu wa Serikali.
Mnamo Machi, 1999, baada ya BOS kuwa Wakala wa Serikali,
jina la ofisi hii lilibadilishwa na kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS), ikiongozwa na Ndugu Cletus P.B. Mkai kama Mkurugenzi
Mkuu kuanzia mwaka 1998. Ofisi zake ziliendelea kuwepo jengo
la Casino na kuwa chini ya Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Ndugu C. P. B. Mkai alistaafu mwaka 2007 na Dkt. Albina A.
Chuwa alichukua nafasi yake na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu.
Dkt. Albina A. Chuwa amekuwa ni mwanamke wa kwanza
kushika cheo hiki tangu kuanzishwa kwa Ofisi hii mwaka 1949.
Kabla ya mwaka 1980, Idara zilikuwa zikiongozwa na Wakuu wa
Idara bila kuwa na muundo maalum. Muundo rasmi ulianza
mwaka 1980 wakati walipoteuliwa wakuu wa Idara na kuitwa
Watakwimu Wakuu wa Serikali Wasaidizi (Assistant Government
Statisticians). Muundo huu uliendelea kutumika hadi ilipoanzishwa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Ndugu Nathanael K. Mbalilaki
Ndugu Cletus P. B. Mkai
Dkt. Albina A. Chuwa
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
5
Muundo mpya wa NBS ulipitishwa na Idara Kuu ya Utumishi mwaka 1999 wakati NBS
inaanzishwa kuwa Wakala wa Serikali. Muundo huu una ngazi kuu tatu za uongozi kama
ifuatavyo:
i) Ngazi ya Kwanza ni MKURUGENZI MKUU,
ii) Ngazi ya Pili ni WAKURUGENZI ambapo kuna Wakurugenzi wanne kama
ifuatavyo;
a) Mkurugenzi wa Fedha, Utawala na Masoko,
b) Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii,
c) Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, na
d) Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu.
iii) Ngazi ya Tatu ni WAKUU WA IDARA (MAMENEJA). Wakati NBS inaanza kama
Wakala ilikuwa na Idara 10 na baadae kufikia Idara 13 hadi sasa kama
inavyoonyeshwa hapa chini:
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
6
Idara ya Takwimu
za Viwanda na Ujenzi
Idara ya Takwimu
za Biashara, Usafirishaji, Utalii na
Uhamiaji
Idara ya Teknolojia
ya Habari na Masoko
Idara ya Shughuli za Kitakwimu
Idara ya Uratibu, Viwango na Mbinu za
Kitakwimu
Mkurugenzi Mkuu
Idara ya Utumishi
na Utawala
Idara ya Takwimu
za Ajira na Bei
Kurugenzi ya Fedha Utawala, na Masoko
Idara ya Takwimu za Kilimo
MUUNDO WA UONGOZI WA NBS KWA SASA
Idara ya Takwimu za Mazingira na
Uchambuzi wa Takwimu
Idara ya Takwimu za Kodi
Idara ya Fedha
Mkaguzi wa Ndani
Kurugenzi ya Sensa ya Watu na Takwimu za
Jamii
Kurugenzi ya Takwimu
za Uchumi
Kurugenzi ya Uendeshaji Shughuli za Kitakwimu
Idara ya Takwimu za Jamii
Idara ya Takwimu za Pato la Taifa
Mwanasheria
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
7
MUUNDO WA UONGOZI WA NBS KWA SASA
Dr. Albina Chuwa
Mkurugenzi Mkuu
WAKURUGENZI
Stanley Mahembe
Kurugenzi ya Fedha Utawala, na Masoko
Ephraim Kwesigabo Kurugenzi ya Sensa ya
Watu na Takwimu za Jamii
Morrice Oyuke
Kurugenzi ya Takwimu za Uchumi
Radegunda Maro Kurugenzi ya Uendeshaji
Shughuli za Kitakwimu
MAMENEJA
Lilian Karumna
Idara ya Fedha
Aldegunda Komba Idara ya Takwimu za Jamii
Daniel Masolwa
Kaimu Idara ya Takwimu za Pato la Taifa
Ahmed Makbel Idara ya Uratibu, Viwango
na Mbinu za Kitakwimu
Gabriel G. Madembwe
Idara ya Utumishi na
Utawala
Irenius Ruyobya
Idara ya Takwimu
za Ajira na Bei
Said Aboud
Idara ya Takwimu za Kilimo
Wilfred Mwingira
Idara ya Shughuli za Kitakwimu
Mwanaidi Mahiza
Idara ya Teknolojia ya
Habari na Masoko
Mathias Masuka Idara ya Takwimu
za Kodi
Joy Sawe
Idara ya Takwimu za
Viwanda na Ujenzi
Valerian Tesha
Idara ya Takwimu za Biashara, Uusafiri Usafirishaji, Utalii na Uhamiaji
Sango Simba Idara ya Takwimu za Mazingira na
Uchambuzi wa Takwimu
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
8
3.2 Sheria za Kuendesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu Zilizokuwepo Tangu Uhuru Hadi Sasa
Kabla ya Uhuru, Takwimu zilikuwa zinakusanywa kwa kutumia sheria ya Takwimu ya mwaka
1949 (Statistics Ordinance of 1949 – chapter 443). Sheria hii ilikuwa inatumika katika nchi za
kikoloni za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Uganda na Tanganyika. Kupitia sheria hii,
Idara ya Takwimu ya Afrika Mashariki ilipewa mamlaka ya kuratibu mfumo (Muundo) wa
takwimu za uchumi na jamii wa nchi tatu.
Baada ya uhuru mwaka 1961, Mamlaka ya kukusanya, kuhifadhi na kuchapisha takwimu
yalitokana na sheria ya Takwimu Na. 33 ya mwaka 1961. Kupitia sheria hii, Ofisi ilipewa
majukumu yafuatayo;-
(i) Kufanya sensa ya watu,
(ii) Kukusanya, kuhifadhi, kuchambua na kuchapisha takwimu zinazohusiana na
uchumi, jamii na utamaduni, na
(iii) Kuratibu mfumo wa takwimu za kiuchumi na kijamii.
Mwaka 1997, Serikali ilitunga sheria ya Wakala wa Serikali Namba 30 ya mwaka 1997. Lengo
la Serikali lilikuwa ni kuziwezesha Wizara kuunda wakala zitakazotoa huduma kwa ufanisi
zaidi kwa wateja wake na umma kwa ujumla kwa kutumia mbinu mpya za kiutendaji. Tarehe
26 Machi 1999, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilizinduliwa rasmi kuwa Wakala wa Serikali.
Baada ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuwa wakala, mchakato ulianza wa kutunga sheria mpya
ya Takwimu Na. 1 ya mwaka 2002 ambayo iliifuta sheria ya Takwimu ya mwaka 1961.
4. Majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Kutokana na Sheria ya Takwimu Namba 1 (Statistics Act) ya mwaka 2002, Ofisi ya Taifa ya
Takwimu imepewa majukumu ya kuendesha, kusimamia na kuratibu shughuli zote za
kitakwimu Tanzania Bara. Majukumu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kama yalivyoainishwa
kwenye kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Takwimu, Na. 1 ya mwaka 2002 ni kama ifuatavyo:
a. Kuendesha Sensa ya Watu na Makazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
b. Kuandaa mpango wa kitaifa wa takwimu kwa ajili ya utoaji wa takwimu rasmi za
Serikali na kuuhuisha mara kwa mara,
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
9
c. Kuandaa viwango vya kitakwimu na kuhakikisha vinatumika na wazalishaji wote wa
takwimu rasmi nchini ili kuleta uwiano na ulinganifu wa takwimu zinazozalishwa ndani
ya nchi na kimataifa,
d. Kuratibu shughuli zote za kitakwimu nchini,
e. Kukusanya na kusambaza takwimu na taarifa zinazohusiana nazo,
f. Kuwa kitovu cha utunzaji wa takwimu zote rasmi katika nchi,
g. Kuwasaidia watumiaji wa takwimu katika kupata takwimu za kimataifa,
h. Kutoa huduma ya kitakwimu na msaada wa kitaalamu kwa asasi mbalimbali na umma
kwa ujumla, na
i. Kuwa kitovu cha rejea kwa Mashirika ya Kimataifa na makampuni ya kigeni
yanayohitaji taarifa za kitakwimu kuhusu Tanzania.
5. Sensa, Tafiti na Matukio Muhimu Yaliyofanyika Tangu Mwaka 1961
Tangu baada ya Uhuru mwaka 1961 NBS imeweza kufanya sensa, tafiti na kushiriki katika
warsha na mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Mafanikio makubwa yalipatikana
baada ya NBS kuanzishwa na kuweza kutoa takwimu na viashiria mbalimbali vya kiuchumi na
kijamii vilivyoiwezesha Serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kitaifa. Sensa,
tafiti na matukio hayo ni kama ifuatavyo:
a. Sensa ya Watu na Makazi 1967, 1978, 1988 na 2002,
b. Utafiti wa Mapato na Matumizi wa Kaya Binafsi tangu ikiitwa „The family Budget
Survey 1963, HBS 1969, HBS 1976/77, 1991/1992, 2001 na HBS 2007‟,
c. Hali ya Uchumi wa Tanzania 1966/67, 1968/69, 1970/71, 1972/73, 1981, 1989, 1991,
1997, 1999 mpaka 2009,
d. Sensa ya Kilimo 1971/1972, 1993/95, 2002/03 na 2007/2008,
e. Utafiti wa Afya ya Mama na Mtoto (DHS) 1991/92, 1994, 1996, 2004/05 na 2010,
f. Utafiti wa Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi 2000/01 na 2006,
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
10
g. HIV/AIDS 2003/04,
h. HIV/AIDS na Malaria 2007,
i. Utafiti wa Wenye Ulemavu 2008,
j. National Panel Survey 2008/09,
k. Tanzania Social Economic Database (TSED),
l. Statistical Abstract,
m. Kusimamia kikamilifu Chama cha Watakwimu Tanzania (TASTA),
n. Kuandaa na kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika kila mwaka,
o. Kushiriki kwa mara ya kwanza kuadhimisha Siku ya Takwimu Duniani ambayo ilianza
mwaka 2010,
p. Kushiriki katika kuweka takwimu za Tanzania kwenye mtandao wa IMF zikielezea
mbinu zitumikazo katika kutoa takwimu mbalimbali za nchi yetu (General Data
Dissemination System) - (GDDS) kuanzia Julai, 2001, na
q. Kushiriki katika kuandaa na kuboresha takwimu za Jumuiya ya Afrika Mashariki
ikiwemo kuandaa, kuboresha na kuweka takwimu katika „database‟ ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
6. Mafanikio na changamoto zilizopatikana tangu mwaka 1961
A. Mafanikio
i) Kuanzishwa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Kuimarisha na Kuboresha Takwimu
Tanzania. Maeneo makuu matano ambayo Mpango huu umejikita ni kama
ifuatavyo:
1. Uboreshaji wa miundo ya taasisi na sheria ya takwimu,
2. Uendelezaji na uboreshaji raslimali watu,
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
11
3. Uimarishaji wa miongozo ya ukusanyaji takwimu,
4. Kuimarisha upatikanaji na usambaji wa takwimu,
5. Upatikanaji wa majengo ya ofisi na vitendea kazi.
ii) Kuongeza ubora na kupanua wigo wa uzalishaji wa takwimu za msingi (core
statistics) kama vile Pato la Taifa, Mfumuko wa Bei, takwimu za viashiria
mbalimbali vya kijamii na kiuchumi,
iii) Kuaminika kimataifa katika utoaji takwimu, ambapo Tanzania imechaguliwa kuwa
mjumbe kwenye Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UN Statistical
Commission) kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2011 hadi 2015.
iv) Kuimarika kwa ushirikiano na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kwa kuendelea kufanya vikao vya pamoja kila baada ya miezi mitatu
kwa lengo la kujadili maendeleo ya takwimu nchini.
v) Kuwasilisha majedwali ya Hali ya Uchumi kwa Wizara yenye dhamana na takwimu
kila ifikapo tarehe 31 Machi ya kila mwaka ili kuiwezesha Serikali kupanga
mipango yake inavyostahili,
vi) Kuanzisha mfumo endelevu wa kijiografia wa ukusanyaji, utunzaji na usambazaji
wa takwimu na taarifa nchini,
vii) Katika kuendeleza na kuboresha nyanja za uchambuzi na usambazaji wa takwimu za
uchumi na kijamii kwa ajili ya ulinganisho na nchi nyingine duniani, NBS
imeendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa, kama vile:
- Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN),
- Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),
- Benki ya Dunia (WB),
- Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB),
- Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID),
- Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID)
- Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA)
- Idara ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UNSD), n.k.
viii) Kwa upande wa rasilimali watu kwa kipindi cha miaka 5 iliyopita, NBS imeongeza
watumishi wake kutoka 138 mwaka 2006/7 hadi kufikia 182 mwaka 2010/11.
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
12
Sanjari na hilo, NBS inao wataalam 125 wenye shahada mbalimbali ambao ni
asilimia 69 ya watumishi wote,
ix) Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya NBS kutoka Tshs 2.6 bilioni mwaka 2004/05
hadi Tshs 8.0 bilioni mwaka 2010/11 kwa ajili ya kufanikisha majukumu ya Taasisi
hii.
x) Kutoa viashiria na taarifa mbalimbali za kitakwimu zinazohitajika katika kutathmini
utekelezaji wa mikakati na mipango mbalimbali ya maendeleo katika kuisaidia
serikali kutoa maamuzi sahihi – mfano MKUKUTA kwa Tanzania Bara, MKUZA
kwa Tanzania Zanzibar, Malengo ya Milenia ya mwaka 2015, na Dira ya Maendeleo
ya Taifa ya mwaka 2025 kwa Tanzania Bara na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya
mwaka 2020 kwa Tanzania Zanzibar.
xi) Kuzindua na kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa Huduma Bora kwa Mteja wa
mwaka 2010.
xii) Kuongezeka kwa matumizi ya takwimu kutokana na uhamasishaji unaofanyika
kupitia vipindi vya redio, luninga, magazeti na uzinduzi mbalimbali wa makala.
xiii) Kuongezeka kwa ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi ya maamuzi kutoka
asilimia sifuri mwaka 1999 hadi asilimia 40 mwaka 2011.
B. Changamoto
i. Katika miaka ya 1980 - 1998 kulikuwa na ukosefu wa fedha, fedha zilikuwa
zinatolewa kwa ajili ya mishahara tu, fedha za vitendea kazi na ukusanyaji wa
takwimu hazikutolewa hivyo „administrative records data‟ ndio zilizokuwa
zinatumika,
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
13
ii. Fani ya Takwimu kwa muda mrefu haikupewa kipaumbele hasa katika
kupandishwa vyeo (promotions) ikilinganishwa na Wachumi ambao wao
walikuwa wanapata vyeo kwa mtiririko kila mwaka,
iii. Serikali ilisitisha ajira mpya kwa kipindi kirefu katika miaka ya 1980 na hii
ilisababisha upungufu mkubwa wa rasilimali watu katika fani ya takwimu,
iv. Mapungufu ya Sheria ya Takwimu Na. 1 ya 2002 kutotoa uhuru (professional
autonomy) na fursa ya NBS kuelekeza Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kuhusu
njia bora ya kukusanya, kuchambua na kuziwasilisha takwimu kwa usahihi kwa
kutumia viwango vya takwimu vilivyokubalika kitaifa na kimataifa. Hali
kadhalika, Mfumo wa Taifa wa Kutoa na Kusambaza Takwimu nchini (National
Statistical System – NSS) kutotambuliwa na Sheria hii,
v. Kuboresha maslahi ya watumishi ili kuhimili ushindani katika soko la ajira,
vi. Ufinyu wa bajeti ya kujenga uwezo wa Watakwimu hasa katika shughuli za
kuboresha utoaji wa takwimu za msingi zinazohitajika na Serikali ikiwa na pamoja
na kufungua Ofisi za Takwimu za Wilaya ili kuendana na Sera ya Serikali ya
ugatuaji madaraka kwa wananchi,
vii. Ukosefu wa majengo ya uhakika kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu makao makuu na
mikoani pia,
viii. Uhaba wa vitendea kazi hasa wakati wa ukusanyaji wa takwimu na uchambuzi
kwa mfano magari, kompyuta na kadhalika,
ix. Kutokidhi mahitaji ya wateja kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya takwimu
nchini hali iliyotokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii duniani,
x. Upungufu wa wanawake katika fani ya Takwimu,
xi. Kutokuwepo kwa sera ya Utoaji na Uhamasishaji wa utumiaji wa Takwimu toka
Taifa hadi ngazi ya Vijiji,
xii. Ukosefu wa taarifa sahihi za uzalishaji bidhaa na huduma kwa wakati kutoka
katika vyanzo vya Takwimu, na
xiii. Ufinyu wa bajeti unaosababisha kutotolewa kwa viashiria muhimu kama vya
kupima hali ya uchumi katika ngazi ya wilaya na mikoa.
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
14
C. Namna ya Kukabiliana na Changamoto Hizi
i. Kwa kuwa hivi sasa kuna mkakati unaoendelea wa Kitaifa wa
kuboresha na kuimarisha Takwimu Tanzania, suala la sheria ya
Takwimu kubadilishwa litashughulikiwa katika zoezi hili ambalo
limeishaanza na linategemewa kumalizika mwaka 2016,
ii. Vitendea kazi vinatarajiwa kuongezwa kutoka serikalini, wadau wa maendeleo na
kupitia Mpango Kabambe wa Kuimarisha na Kuboresha Takwimu (Tanzania
Statistical Master Plan - TSMP),
iii. Katika kuongeza ubora wa takwimu zinazokusanywa, Ofisi itaendelea kufanya
ukaguzi mikoani mara kwa mara kuhakikisha takwimu zinazokusanywa zina ubora
unaokubalika,
iv. Kuhusu ukosefu wa wanawake katika fani hii ya takwimu, Ofisi inakusudia
kufanya uhamasishaji kwa wanafunzi wa kike wanaosoma sekondari ili waweze
kusoma hesabu na hatimaye kuingia katika fani hii,
v. Katika kuboresha maslahi ya Watumishi, Ofisi inatarajia kutumia taarifa
itakayotolewa na Mtaalam Mshauri kupitia TSMP, mapendekezo ya kuboresha
maslahi ya watumishi yatawasilishwa Serikalini baada ya kufanya upembuzi
unaostahili,
vi. Kuhusu upatikanaji na usambazaji duni wa takwimu katika ngazi mbalimbali,
Ofisi itaendelea na jitihada za kuhakikisha Takwimu zinapatikana na kusambazwa
katika ngazi ya taifa hadi vijijini kwa kupitia mikutano, machapisho, warsha ,
vipindi vya redio na luninga ili wadau waweze kutumia takwimu hizi kwa kupanga
mipango ya maendeleo na sio kukisia/kukadiria tu,
vii. Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa Ofisi, NBS kwa kupitia Mpango wa
TSMP iko kwenye mchakato wa kufanya tathmini ya mazingira (Environmental
Impact Assessment) kupitia Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo
la Makao Makuu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
viii. Kuhusu ufinyu wa Bajeti, Ofisi itaendelea kufanya majadiliano na Serikali pamoja
na wadau wa maendeleo kuhusu uwezekano wa kuongeza bajeti ya NBS ili
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
15
takwimu na viashiria mbalimbali ziweze kutolewa hadi ngazi ya mikoa na wilaya,
na
ix. Kuhusu ukosefu wa taarifa sahihi kutoka vyanzo vya takwimu, Ofisi itaendelea
kuielimisha umma na wadau wa takwimu umuhimu wa kutoa taarifa sahihi na kwa
wakati.
7. Mwelekeo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika miaka 50 ijayo
a. Uboreshaji wa Ukusanyaji wa Takwimu
i. Majengo na vitendea kazi
Ukuaji wa shughuli za kitakwimu kunaenda sanjari na mahitaji ya majengo ya Ofisi
ya Taifa ya Takwimu ikiwemo Ofisi za Mikoa pamoja na vitendea kazi kama magari
na vinginevyo. Aidha, ukuaji huu unahusisha pia kuendela kuboresha utumiaji wa
vifaa vya ”teknohama” pamoja na programu za uchambuzi wa takwimu kwa ajili ya
kuboresha upatikanaji wa takwimu kwa wadau mbalimbali. Mipango ya baadae ni
kuhakikisha vituo vya uchambuzi wa takwimu vinaanzishwa katika mikoa sanjari na
uimarishwaji wa Chuo Cha Takwimu cha Afrika Mashariki.
Mpaka sasa NBS bado inatumia majengo ya kukodi kwa baadhi ya Idara zake,
mkakati uliopo ni kujenga jengo la takwimu (Takwimu House) kupitia Mpango
Kabambe wa Koboresha Takwimu.
ii. Mafunzo
Uendelezaji wa raslimali watu utafanywa kwa kujenga uwezo wa watumishi kwa
kuwaongezea ujuzi na maarifa ya ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa takwimu
zinazoonyesha hali halisi. Mafunzo hayo yatakuwa ya muda mfupi na mrefu kwa
mujibu wa mahitaji,
iii. Uimarishaji wa Miongozo ya Ukusanyaji wa Takwimu
Kutaundwa miongozo ya ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu itayokubalika
kimataifa, kuwa na matumizi sahihi ya misamiati, tafsiri, mbinu nzuri katika
ukusanyaji takwimu pamoja na kuwa na mihimili imara ya sampuli kwa tafiti za
kiuchumi na kijamii. Aidha, mfumo wa kijiografia (Geographical Information System)
utaimarishwa ili kuongeza matumizi ya takwimu kwa sababu hufikisha ujumbe kwa
haraka zaidi unapotumika.
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
16
iv. Kuongeza mahusiano na nchi za nje na ofisi za kimataifa kuhusu uboreshaji, ukusanyaji,
uchambuzi na usambazaji wa takwimu.
b. Uboreshaji wa Bajeti ya NBS
i. Ni matarajio ya NBS kuwa Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya NBS ili
takwimu na viashiria mbalimbali ziweze kutolewa kwa watumiaji wa ndani na
nje,
ii. Serikali itaendelea kuipa uwezo NBS kifedha ili kuboresha mafungu ya fedha
ziendazo Ofisi za Taifa za Takwimu mikoani kwa ajili ya kazi za ukusanyaji wa
takwimu maana mahitaji ya takwimu yameongezeka katika ngazi zote za
utawala na wadau kwa ujumla.
c. Maboresho Mengine ya Takwimu
Ofisi ya Taifa ya Takwimu inatarajia kufanya yafuatayo kwa miaka ijayo:
i. NBS itaendelea kuboresha Vizio katika utoaji wa GDP na CPI kwa kutumia
Utafiti wa Mapato na Matumizi katika Kaya Binafsi (HBS) na vyanzo na tafiti
nyingine,
ii. Kuboresha muundo wa Taasisi na Sheria ya Takwimu,
iii. Kuendelea kupanua wigo kwa kufanya tafiti mbalimbali kupitia “Commissioned
Work” ili kuongeza mapato,
iv. Kuendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa TSMP katika Wizara, Idara na
Taasisi mbalimbali za Serikali,
v. Kuendelea na maandalizi ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya 2012, zoezi
hili litaendelea kwa kufanya kazi za uchambuzi, usambazaji na utunzaji wa
takwimu hadi mwaka 2015. Kuanzia mwaka 2016 maandalizi ya Sensa ya Watu
na Makazi ya mwaka 2022 yataanza, na
vi. Katika kuboresha fani ya takwimu nchini, NBS itaendelea na juhudi za kufufua
na kuimarisha Chama cha Watakwimu Tanzania (Tanzania Statistical
Association - TASTA).
Miaka 50 Ya Uhuru wa Tanzania Bara, Makala ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu
17
8. Hitimisho
Pamoja na changamoto zinazoikabili Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika suala zima la
maandalizi ya Sensa, juhudi zimewekwa ili kuhakikisha kuwa maandalizi yanakamilika
ipasavyo. Sensa ijayo ina umuhimu wa kipekee kwani ndiyo itakuwa chanzo kikuu cha
takwimu zitakazotumika kupima ni kwa kiasi gani Tanzania imefanikiwa katika kutekeleza
Malengo ya Milenia ya mwaka 2015 pamoja na programu nyingine za maendeleo
zilizowekwa na Serikali.
Vilevile, Ofisi ya Taifa ya Takwimu itaendelea kutoa Takwimu za Pato la Taifa kwa kila
mwaka, Mchango wa shughuli za Kiuchumi kwa mwaka, Wastani wa Pato la Mtanzania
kwa mwaka na kutayarisha Takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka.
Moja ya lengo la Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu ni
kuwa na mfumo imara na bora wa kitaifa wa kuratibu, kukusanya, kuhifadhi na kusambaza
takwimu rasmi hapa nchini. Kwa maana hiyo, utekelezaji wa Mpango huu utaboresha
upatikanaji wa takwimu bora, sahihi na kwa wakati ambazo zitasaidia Serikali na Taasisi
mbalimbali kufanya maamuzi sahihi ya kisera na pia kupima viashiria muhimu vya
kutathmini utekelezaji wa MKUKUTA/MKUZA, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania
Bara ya mwaka 2025 na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania Zanzibar ya mwaka
2020.
Aidha, kupitia Mpango huu vitengo vya takwimu katika ngazi mbalimbali za Serikali
vitaanzishwa au kuboreshwa ili uzalishaji wa takwimu uweze kukidhi mahitaji ya wadau
mbalimbali.
OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU
Dira
Dira ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ni kuwa chanzo cha kuaminika katika kutoa takwimu rasmi
nchini.
Dhamira
Dhamira ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ni kuuwezesha mchakato wa kufanya maamuzi kwa kutoa
takwimu bora na zinazokubalika kwa wakati, kuratibu shughuli za kitakwimu na kuhamasisha
utumiaji wa methodolojia na mbinu za kitakwimu.