Upload
shafii-muhudi
View
470
Download
0
Embed Size (px)
DESCRIPTION
HOJA YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MUUNDO WA SERIKALI MBILI (Kiswalili)
Citation preview
1
HOJA YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MUUNDO
WAKE WA SERIKALI MBILI
(Omar R. Mapuri)
UTANGULIZI
Hoja ya Muungano wa Tanzania inasimama juu ya msingi wa sera ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM). Sera ya CCM kuhusu Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kuwa Tanzania ina ncha mbili; yaani kuulinda na
kuudumisha Muungano wenyewe kwa upande mmoja na muundo wa
Muungano huo kuwa wa Serikali mbili kwa upande wa pili.
CCM inaushabikia Muungano na kupania kuulinda na kuudumisha kwa
sababu kwanza inaamini kuwa Muungano huu ni wa watu wenyewe na pili,
uliasisiwa na vyama wazazi wake, yaani TANU na ASP. Zaidi ya hivyo,
CCM yenyewe ni matokeo ya Muungano huo na chachu ya kuziimarisha
kwani tendo la kuviunganisha vyama vya TANU na ASP kuunda CCM
lilitokana na utashi wa kukamilisha hatua za kuunda Muungano.
CCM inaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali mbili kwa sababu
kwanza ndio ulioamuliwa na waasisi wa Muungano, Marehemu Baba wa
Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume, na pili
2
umezingatia vya kutosha uhalisi wa mambo wa nchi kubwa na ndogo
kuungana. Muundo huo ndio unaohakikisha umadhubuti wa Muungano
wenyewe bila ya nchi ndogo (Zanzibar kwa muktadha huu) kumezwa na
nchi kubwa (Tanganyika).
CCM inajivunia Muungano huu na muundo wake wa Serikali mbili kwani
hata baada ya miaka 40 ya kuundwa kwake bado ndio mfano pekee wa
Muungano uliofanikiwa wa nchi huru zilizoungana katika Bara la Afrika.
Zaidi ya yote, Muungano huu umeweza kuhimili misukosuko yote ya ndani
uliyokumbana nayo ambayo ingeweza kuudhofisha au hata kuuvunja.
Pamoja na makelele mengi ya kisiasa yenye kuulalamikia, Muungano huu na
muundo wake wa Serikali mbili unaungwa mkono na Watanzania walio
wengi. Ushahidi wa kitakwimu utatolewa katika makala haya kwamba
muundo wa Serikali mbili ndio unaotakiwa na Watanzania walio wengi, na
muundo wa Serikali tatu unaopigiwa debe sana na vyama vya upinzani na
baadhi ya wasomi ndio unaokataliwa na Watanzania wengi kuliko muundo
mwingine wowote.
Kabla ya kuendelea na hoja, inafaa katika hatua hii kutazama maandiko
rasmi ya kisera ya CCM kuhusu Muungano na muundo wake, kama yalivyo
katika Ilani za Uchaguzi za CCM za 1995 na 2000.
Ibara ya 47 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 1995 inasomeka ifuatavyo:
47. Sera ya Kuimarisha Muungano
3
Muundo wa Muungano, ambao unakubaliwa na CCM, ni
Muungano wenye Serikali mbili: Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Sera hii imethibitishwa mwaka 1994 wakati wanachama wetu
walio wengi walioshiriki katika kura za maoni kote nchini
walitaka sera hii iendelee. Katika kipindi cha miaka mitano
ijayo, CCM itaendelea kudumisha Muungano wa Tanzania
katika muundo wa Serikali mbili.
Kwa upande wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2000, ibara
zinazozungumzia kuimarisha Muungano ni za 116 na 117 ambazo
zinasomeka ifuatavyo:-
116. Umoja wa kitaifa wa Watanzania ambao umedumu kwa kipindi
kisichopungua miaka 36 unatokana na Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ambao ulizaa Tanzania. Katika
kipindi chote hicho muundo wa muungano ambao umeendelea
kukubaliwa na Chama Cha Mapinduzi ni muungano wenye
Serikali mbili: Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Sera hii imeendelea
kuthibitishwa na wanachama wa CCM na wananchi kwa jumla.
117. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2000 2005) Chama
Cha Mapinduzi kitaendelea kuhakikisha kuwa mafanikio
yaliyorithiwa kutoka kwa Waasisi wa taifa letu Baba wa Taifa,
Mwalimu J.K. Nyerere na Makamu wake wa Kwanza Sheikh
Abeid Aman Karume yanaendelezwa na kulindwa kwa
4
kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa huru, Taifa lenye
Umoja, Udugu na Mshikamano na nchi yenye amani na utulivu.
Aidha, muundo wa Muungano utaendelea kuwa wa Serikali
mbili: yaani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar.
Hivyo ndivyo inavyosema Sera ya CCM kuhusu Muungano na muundo
wake. Ni muhimu hili kuwekwa sawa kwani wapinzani wa CCM, hasa kule
Zanzibar, hupenda kujichukulia uhuru wasiopewa wa kuisemea CCM
wapendavyo wao. Hupenda sana kuipotosha sera hii kwa kuinukuu kilaghai
kwamba eti ni ya Serikali mbili kuelekea moja. Kauli hiyo imewahi
kutoka katika vikao vya CCM kama kauli nyingi nyenginezo zilivyowahi
kutoka. Kwa mfano, Bunge, likiwa na Wabunge wa CCM watupu liliwahi
kupitisha azimio la kutaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya
Muungano. Lakini baada ya yote hayo na kauli zote zilizosemwa na/au
kuandikwa, ulipofika wakati wa kutunga sera rasmi, Chama kiliamua bila ya
kigugumizi kuendelea na sera ya Muungano wa Serikali mbili na kuiweka
kwa uwazi na bila ubabaishaji katika Ilani za Uchaguzi.
NGUZO ZA MUUNGANO
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulijengwa juu ya msingi wa
kijiografia na kihistoria uliowafanya watu wa maeneo haya kuwa wamoja,
ndugu, wenye tamaduni zilizoingiliana na hata wenye utashi wa kisiasa
uliofanana.
5
Juu ya msingi huo, zimesimama nguzo nne zinazouhimili Muungano huo.
Nguzo ya kwanza ambayo imejengeka kwa muda mrefu katika historia ni
kwamba Muungano huu ni wa watu wenyewe. Nguzo hii inaupa Muungano
uhalali wa kijamii na hata wa kisiasa. Nguzo ya pili ni msukumo wa
kujenga umoja wa Afrika. Nguzo hii inaupa Muungano uhalali wa kisiasa
za kimataifa. Nguzo ya tatu ni Hati ya Muungano ambayo iliujengea
Muungano uhalali wa kisheria ambao unaendelezwa na Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na Katiba ya Zanzibar ya 1984. Nguzo
ya nne inayouhimili Muungano na ambayo inaendelea kujengeka ni ya
uendelevu wa Muungano wenyewe. Muungano wa Tanzania umeshatimiza
miaka 40 ukiendelea kuimarika. Umeweza na unaendelea kuhimili
misukosuko mingi, ambapo kila unapoingia kwenye tanuri la misukosuko,
unaibuka ukiwa imara zaidi. Nguzo hii inaupa Muungano uhalali wa kisiasa
za ndani.
Sasa tuzitazame nguzo hizi moja moja.
Nguzo Ya Umoja wa Watu Wenyewe
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umejengeka kutokana na mahusiano
ya dahari na karne baina ya watu wa visiwa vya Zanzibar na mwambao wa
Afrika ya Mashariki, hasa Mrima ambayo ni sehemu kubwa ya Tanzania
Bara ya sasa.
6
Kabla ya Kuja Kwa Wageni Toka Nje ya Afrika
Wanahistoria (mfano Ingrams) wakijenga hoja kutokana na maandiko ya
kale ya Periplus (karne ya kwanza AD) na ngano za watu wa kale,
wanakubaliana kwamba watu wa kwanza kabisa kufika katika visiwa vya
Zanzibar ni Waafrika kutoka Mrima katika harakati za uvuvi. Ushahidi wa
kiakiolojia wa hivi karibuni umethibitisha usahihi wa imani hiyo.
Wakati wa Himaya ya Zenj
Lakini hata baada ya kuja kwa wageni kutoka nje ya Afrika, mahusiano ya
watu wa pande hizi mbili siyo tu yaliendelea, bali yalizidi kuimarika hasa
kutokana na kuongezeka kwa ubora wa teknolojia ya usafiri wa baharini.
Himaya ya Waajemi (Washirazi) katika eneo hili ambayo baadhi ya
wanahistoria wanaiita Himaya ya Zenj (Zenj Empire) ilipojengeka kutokana
na ujio wa wale Ndugu saba wa El-Hasa mnamo karne ya 13 ambao
walianzisha tawala katika vituo mbali mbali vya mwambao wa Afrika
Mashariki (mfano Kilwa, Barawa, Lamu, Unguja, Pemba, n.k.), maingiliano
ya watu wa maeneo haya yaliendelea bila ya vikwazo.
Wakati wa Himaya ya Biashara ya Zanzibar
Mnamo karne za 16 hadi katikati ya 19, ilijengeka Himaya ya Kibiashara
ambayo kitovu chake kilikuwa Zanzibar. Himaya hiyo iliyojumuisha
biashara ya watumwa, vipusa na viungo, ilienea hadi maeneo ya Maziwa
Makuu kwa upande wa Kaskazini Magharibi na maeneo ya Ziwa Nyasa na
Mto Ruvuma kwa upande wa Kusini mwa Tanzania ya leo. Katika kitabu
7
chake cha Slaves, Spices & Ivory in Zanzibar Profesa Abdul Sheriff
anazungumzia dhana ya Bara ya Zanzibar (The Hinterland of Zanzibar)
akiwa na maana ya eneo la Bara lililokuwa chini ya ushawishi wa Zanzibar
(bila shaka na Sultani wake), ambalo kwa kiasi kikubwa ni hili hili eneo la
Tanzania Bara ya leo. Dhana hiyo ilipewa methali maarufu ya: Inapopigwa
ngoma Zanzibar, wanacheza katika Maziwa Makuu.
Maelezo haya yanajaribu kujenga hoja kwamba eneo ambalo leo linaitwa
Tanzania, kwa kiasi kikubwa ndilo lililokuwa Himaya ya Kibiashara ya
Zanzibar ya enzi hizo. Kwa maneno mengine nchi hii ilikuwa moja toka
enzi hizo ingawa yenye mipaka hafifu. Watu wa eneo lote hili
waliunganishwa na harakati za biashara. Biashara ya utumwa iliwafanya wa
huku waende kule na wa kule waje huku, ingawa katika mazingira ya
uchungu. Watumwa walichukuliwa Bara na kupelekwa visiwani Zanzibar
ambako vizazi vyao vimeendelea hadi leo na kufanya sehemu kubwa ya
Wazanzibari. Kwa upande mwengine, wako wafanyabiashara ya watumwa
walioanzia Zanzibar na kuhamia Bara na kufanya maskani yao huko. Vizazi
vyao vinaendelea hadi leo na wamekuwa sehemu ya jamii ya Watanzania
Bara. Hivi sasa, katika mazingira ya uhuru, watu wa kila upande kati ya
pande mbili hizi wanaendelea kuhamia na kuweka maskani katika upande
wa pili bila ya vikwazo.
Utenganishi wa Wakoloni wa Kizungu
Kitendo kilichowatenganisha watu wa pande hizi ni kile cha wakoloni
kutoka Ulaya (Wazungu) kugawana makoloni katika Bara la Afrika, katika
nusu ya pili ya karne ya 19. Baada ya kinyanganyiro baina yao, wakoloni
8
hao walikutana katika Mkutano wa Berlin wa 1887 ambapo waligawana
Afrika. Katika mgao huo, sehemu ya Bara (ukiondoa ukanda wa mwambao
wa pwani ulioitwa Mrima) walipewa Wajerumani. Koloni hilo ambalo
lilijumuisha Burundi na Rwanda ya sasa liliitwa Deutsche Ost Afrika (yaani
Afrika Mashariki ya Wajerumani). Sultani wa Zanzibar aliachiwa visiwa
vya Unguja, Pemba na Mafia na ukanda wa Mrima. Miaka mitatu baadae,
chini ya Mkataba wa Heligoland wa 1890, Sultani alilazimishwa kuuza kwa
Wajerumani ukanda wa Mrima na kisiwa cha Mafia, na hivyo kubakiwa na
visiwa vya Unguja na Pemba tu, na yeye mwenyewe kuwekwa chini ya
Himaya ya Mwingereza. Watu wa Bara na Visiwani wakawa
wametenganishwa.
Kuanza Kurejeana
Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1915 1919), majaaliwa
yalianza kuwakurubisha tena watu wa pande hizi mbili. Kufuatia kushindwa
kwa Wajerumani katika vita hivyo, Rwanda na Burundi walipewa Wabelgiji
na sehemu iliyobaki ya Deutsch Ost Afrika iliitwa Tanganyika Territory na
kupewa Waingereza. Kwa hivyo watu wa Zanzibar na Tanganyika ingawa
waliendelea kuwa na nchi mbili tofauti, lakini angalau wakawa chini ya
mkoloni mmoja.
Hali hiyo ilijenga mazingira ya kuweza kurejea kwa mawasiliano baina ya
watu wa Bara na wa Visiwani ambayo yalikuwa yameathirika vibaya kwa
kipindi cha kiasi cha miaka 30. Mwamko wa kudai uhuru wa kijamii na
baadae wa kisiasa ulipoanza kujengeka, watu wa pande hizi mbili, hususan
9
wenyeji wa asli (yaani Waafrika) hawakusita kuitumia fursa hiyo
kushirikiana na kusaidiana katika azma hiyo.
Mwaka 1927, Waafrika wa Dar es Salaam walianzisha jumuiya yao
iliyoitwa African Association kwa ajili ya kupigania maslahi yao ya
kijamii. Mwaka 1934, Waafrika wa Zanzibar nao walianzisha African
Association yao, pengine kutokana na ushawishi wa ndugu zao wa Dar es
Salaam. Nao Waafrika wa Zanzibar wakawashawishi wale wa Dodoma na
kupelekea kuundwa kwa African Association ya Dodoma. Jumuiya tatu
hizi zilijenga umoja wa kufanya mikutano mikuu ya pamoja ya mwaka kwa
zamu baina ya miji hiyo, na zilikuwa chachu ya kufunguliwa kwa matawi ya
African Association katika miji mbali mbali Tanganyika na Zanzibar.
Ziara za Michezo
Sambamba na ushirikiano huo wa kijamii, wananchi wa Tanganyika na
Zanzibar walianzisha utamaduni wa kubadilishana ziara za kimichezo. Ziara
hizo zilikuwa zikifanyika wakati wa mapumziko ya Pasaka, kwa utaratibu
wa zamu ambapo kama mwaka huu wanamichezo wa Zanzibar wanakwenda
Tanganyika, mwaka ujao wa Tanganyika watakwenda Zanzibar. Utamaduni
huo unaendelea hadi leo na umezidi kupanuka kwa kujumuisha wasanii na
hata wananchi tu wa kawaida.
Ushirikiano wa Kisiasa
Upepo wa harakati za kudai uhuru kutoka kwa wakoloni ulipofika maeneo
haya, watu wa Tanganyika na Zanzibar walihamasishana, kushirikiana na
10
kusaidiana katika jukumu hilo la kudai na kupigania uhuru wa nchi zao.
Mwaka 1954, chama cha Tanganyika African National Union (TANU)
kilianzishwa Tanganyika kutokana na Tanganyika African Association, kwa
ajili ya kudai uhuru wa Tanganyika. Zanzibar nako mwaka 1957
ilianzishwa Afro-Shirazi Party (ASP) kutokana na kuungana kwa African
Association na Shirazi Association (iliyokuwa imeundwa 1938). Kuundwa
kwa ASP kulishuhudiwa na Rais wa TANU, Mwalimu Julius K. Nyerere.
Ushirikiano wa TANU na ASP katika mapambano ya kudai uhuru hadi
ulipopatikana Uhuru wa Tanganyika Disemba 9, 1961 na kufanikiwa kwa
Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964 unajulikana na hauna haja ya
kuufafanua hapa. Dhamira angalau ya ASP (wakati wa kupigania uhuru) ya
kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika baada ya uhuru haikuwa siri. Hiyo
inadhihirishwa na maelezo yafuatayo ya Marehemu Sheikh Thabit Kombo
kama yalivyonukuliwa na Rais Benjamin Mkapa katika hotuba yake ya
kihistoria aliyoitoa Zanzibar kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya
Muungano tarehe 26 Aprili, 2004:-
Mafisadi wanalalamika, kwa nini muungano umefanyika haraka
haraka; Mapinduzi Januari na Muungano Aprili, miezi mitatu tu!
Wako wanaodhani kuwa Mwalimu Nyerere ndiye aliyelazimisha
Muungano.
Wazo la Muungano ni wazo la Afro-Shirazi tokea mwanzo.
Utakumbuka katika Manifesto yetu tulisema kuwa tukipata Uhuru
azma ya ASP ni kuona kuwa Afrika yote inakuwa moja yenye nguvu.
Lakini kwa Tanganyika na Zanzibar ahadi ya muungano ni ahadi ya
11
wanachama wenyewe waliyokuwa wanaitoa katika mikutano yao
yote Watu wa Tanganyika na watu wa Zanzibar ni wale wale,
tofauti ni sisi wa Zanzibar kutawaliwa na Sultani. Mazungumzo
yalikuwa mafupi sana, yalichukua siku moja tu; maana hakukuwa na
swali kama tuungane au tusiungane. Hoja ilikuwa tu muungano wetu
uwe na sura gani..
Muungano Kama Tukio la Kimantiki
Kutokana na ukweli huo wa kihistoria wa umoja, udugu na ushirikiano wa
muda mrefu baina ya watu wa pande hizi, na kufuatia TANU na ASP
kushika madaraka baada ya Uhuru na Mapinduzi, Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar kuwa Tanzania uliokamilishwa rasmi tarehe 26 Aprili, 1964
lilikuwa ni tukio la kimantiki na halipaswi kuwa la kushangaza.
Ni ukweli wa kihistoria kwamba pamoja na kwamba watu wa Tanganyika na
Zanzibar wamekuwa wamoja katika zama zote za kihistoria, lakini
Tanganyika na Zanzibar hazikuwa nchi tulizoziunda. Ziliundwa na
wakoloni na mipaka yake ilikuwa ikipangwa na kupanguliwa na wakoloni
kwa maslahi yao. Tanganyika na Zanzibar pamoja na mipaka yake tuliirithi
tu kutoka kwa wakoloni baada ya uhuru. Lakini Tanzania tumeiunda
wenyewe.. Katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya
Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere anasisitiza kwa fahari: Tanzania ni
lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru. Nchi nyingine zote ni za
kurithi kutoka katika Ukoloni. Tanzania ni ya kuundwa na sisi wenyewe,
kwa hiari yetu wenyewe, baada ya kukomboa sehemu zake mbili kutoka
katika Ukoloni. (uk.57).
12
Pamoja na hayo, kama itakavyofafanuliwa baadae, wapo watu
wanaoshangaa na kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
kwa hoja kwamba eti hayakutafutwa maoni ya wananchi kwanza. Katika
kuwabeza watu hao, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake hicho hicho cha
Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania anasema ifuatavyo kwa kejeli:-
Pwani ya Tanganyika na Zanzibar ya sasa zilikuwa pamoja kwa muda
mrefu sana kabla ya kutengwa na Wakoloni Waingereza na
Wajerumani. Kama zingebaki zimetengana, kwa wazalendo hao
hiyo ingekuwa ni halali, maana zilitengwa kwa hila na mitutu ya
bunduki za Mabwana. Lakini uamuzi wa Tanganyika huru na Zanzibr
huru kuungana, na hivyo kuwaunganisha tena ndugu waliokuwa
wametengwa na Mabeberu, tendo hilo kuna wanaosema kuwa
halikuwa halali. Hatukutafuta maoni ya watu kwa njia ya demokrasia
wanayoijua wao. Wajerumani na Waingereza walitafuta maoni ya
wazee wetu kwa mtutu wa bunduki! Hiyo ilikuwa halali. Nchi
walizounda kwa njia hizo zilikuwa halali. Tunatakiwa tujivunie
Utanganyika na Uzanzibari uliopatikana kwa njia hizo; lakini tuuonee
haya Utanzania, tunda la uhuru wetu wenyewe. Sikuamini kuwa
Wakoloni walifaulu kiasi hiki katika kuzinywesha kasumba na
kuzitawala akili za baadhi yetu!. (uk.58).
Tarehe 5 Februari, 1977 vyama vya TANU na ASP viliungana na kufanya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika tukio ambalo lilikuwa na maana ya
kuzidi kuuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Tena kuundwa
kwa CCM kulitanguliwa na mashauriano ya kutosha. Aidha, ilifanywa kura
13
ya maoni ya wanachama ambayo matokeo yake yalikuwa kama
yanavyoonekana katika Jedwali Na. 1 na 2 hapa chini:-
JEDWALI Na. 1: MATOKEO YA MAONI YA WANACHAMA WA
TANU KUHUSU KUUNGANISHWA TANU NA ASP
Matawi Idadi Asilimia
Idadi ya Matawi Yote ya TANU 6,639 100.00
Yaliyokutana 6,427 96.81
Yasiyokutana 212 3.19
Yaliyokubali 5,424 99.95
Yaliyokataa 3 0.05
Idadi ya Matawi Madogo ya TANU 38 100,00
Yaliyokutana 38 100.00
Yaliyokubali 38 100.00
Yaliyokataa 0 0.00
Chanzo: Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, 1977 1997
JEDWALI Na. 2: MATOKEO YA VIKAO NA WANACHAMA WA
ASP KUHUSU MAONI YA KUUNGANISHWA TANU NA ASP
Matawi Idadi Asilimia
Idadi ya Matawi ya ASP 257 100.00
Yaliyokubali 257 100.00
Yaliyokataa 0 0.00
Idadi ya Wanachama Wote Walioshiriki 103,983 100.00
Waliokubali 103,574 99.06
Waliokataa 409 0.04
Chanzo: Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, 1977 1997.
14
Yaani wanachama wa TANU katika katika 99.95 ya matawi yao yaliyotoa
maoni na matawi yote madogo waliafiki chama chao kuunganishwa na ASP.
Kwa upande wa Zanzibar, wanachama wa ASP katika matawi yao yote
waliafiki chama chao kiunganishwe na TANU. Na kwa wanachama mmoja
mmoja walioshiriki katika kura hiyo ya maoni, ni 409 tu kati ya wote
103,983, yaani sawa na asilimia 0.04 tu ndio waliokataa.
Huu ulikuwa ni ushahidi madhubuti usio shaka wa kitakwimu wa imani ya
wananchi kwa Muungano. Kwa kura hiyo, watu wa Tanganyika na Zanzibar
kupitia vyama vyao vya TANU na ASP ambavyo vilikuwa pekee wakati
huo, waliuthibitishia Ulimwengu kwamba Muungano ni wao na haukuwa wa
viongozi tu kama inavyodaiwa na wapinzani wachache wa Muungano.
Kabla ya kuunganishwa kwa TANU na ASP, Katiba ya Muda ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliitaja Jamhuri hiyo kuwa ni ya
mfumo wa chama kimoja ambapo kwa Tanganyika Chama hicho ni TANU
na kwa Zanzibar chama hicho ni ASP. Kwa maneno mengine, Jamhuri
ilikuwa chini ya chama kimoja kwa viwili, jambo ambalo lilileta dosari
kubwa katika uimara wa Muungano. Baada ya TANU na ASP kuungana na
kuwa CCM, dosari hiyo iliondolewa na hivyo kikawa ni kitendo cha
kuimarisha Muungano. Zaidi ya yote, tukio hilo ndilo lililochochea
kutungwa rasmi kwa Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya 1977.
Kwa hivyo, kwa majumuisho, inasisitizwa tena kwamba Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ni wa watu wenyewe. Waasisi wa Muungano huo,
15
yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume
kupitia Serikali zao, waliwezesha tu kufikiwa kwa matarajio ya wananchi
wenyewe. Mzee Karume alilielezea tukio hilo kwa maneno yafuatayo kama
alivyonukuliwa na Rais Benjamin Mkapa katika hotuba yake ya tarehe 26
Aprili, 2004:-
Napenda mfahamu wananchi wote, kazi hii si kazi ya Abeid Karume.
Jambo hili, jambo la wenyewe Waafrika wote. Mwalimu Julius
Nyerere na Abeid Karume wao ni watumishi wa wenyewe wana wa
nchi, na sisi tumekubali kuwatumikia wenyewe wananchi.
Tunawatumikia wananchi kwa utumishi wao maalum, ule walioona
wao wenyewe bora. Basi jambo hili la kufanya Union, Tanganyika na
Zanzibar, ni jambo ambalo lililofikiriwa na wenyewe wananchi wa
Tanganyika na Zanzibar
Hatimaye, mwaka 1977, watu wenyewe, kupitia vyama vyao waliithibitisha
hatua ya Waasisi ya kuunganisha Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Hiki ni kielelezo cha wazi cha umadhubuti wa nguzo hii ya Muungano ya
kwamba Muungano ni wa watu wenyewe, na jinsi nguzo hii inavyoupa
uhalali wa kijamii na hata wa kisiasa Muungano wetu.
Nguzo Ya Msukumo wa Kujenga Umoja wa Afrika
Nguzo ya pili inayouhimili Muungano ni utashi wa kujenga umoja wa
Afrika. Manifesto (Ilani za Uchaguzi) za TANU na ASP toka enzi za
mapambano ya kudai uhuru zilikuwa na vipengele vya kutaka umoja wa
16
Afrika. Aidha, vyama vyote vilishiriki kikamilifu katika majukwaa yote
yaliyowaunganisha Waafrika wa nchi mbali mbali katika kudai uhuru kwa
lengo la kuja kuziunganisha nchi hizo baada ya uhuru. Kwa mfano, TANU
na ASP zilikuwa wanachama wa PAFMECA na baadae PAFMECSA,
vyombo ambavyo viliviweka pamoja vyama vilivyokuwa vikidai uhuru
kutoka nchi mbali mbali za eneo la Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.
Katika hili, hata Chama cha Hizbu (ZNP) cha Zanzibar kilikuwa kikishiriki.
Katika jitihada za kufikia ndoto hiyo ya umoja wa Afrika, nchi za Afrika
Mashariki (yaani Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar) zilijaribu
kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki baada ya uhuru wa nchi hizo. Baada
ya kuona dalili za kukawia kufikiwa kwa lengo hilo katika upeo wa Afrika
Mashariki, Rais Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais Karume wa
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar walikubaliana zianze Tanganyika na Zanzibar
ili kuonyesha njia na kuendeleza shauku ya kutafuta umoja wa Afrika.
Dhamira hiyo inajieleza katika maneno ya Mwalimu Nyerere katika hotuba
yake katika Mkutano Maalumu wa Bunge la Tanganyika, tarehe 25 Aprili,
1964, lililoitishwa kujadili na kuridhia Hati ya Muungano. Mwalimu
anajinukuu katika kitabu chake cha Uhuru na Umoja kama ifuatavyo:-
Ikiwa, basi, nchi ambazo ni marafiki na ni jirani, na hasa zile ambazo
zilipata kuwa moja bali zikagawanywa na wakoloni wapya; ikiwa hizo
zitashindwa kuungana, kushindwa huko kunaweza kukaleta wasi wasi
katika bara letu la Afrika na shauku yake ya Umoja. Bali ikiwa nchi
hizo zaweza kuungana, muungano huo waweza ukawa ni thibitisho la
vitendo kwamba matumaini ya bara letu si ya bure. (uk.292).
17
Miaka miwili baadae, wakati wa sherehe za Muungano kutimiza miaka
miwili zilizofanyika Dar es Salaam mwaka 1966, Mzee Karume naye
aliithibitisha dhamira hiyo. Kama alivyonukuliwa na Rais Benjamin Mkapa
katika hotuba yake ya kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano
tarehe 26 Aprili, 2004 mjini Zanzibar, Mzee Karume alisema yafuatayo:-
Muungano wa Tanzania unaonyesha mithali katika Afrika. Mithali
yenyewe (ni) kuthibitisha nini viongozi wa Kiafrika kabla ya
hawajapata independence walikuwa wakisema. Neno lililokuwa
likisemwa ni hili hapa Tanzania (Muungano). Ya kwamba kila
mmoja akijitapa, mara tu nikipata Serikali yangu katika nchi yangu
lazima nilete uhusiano na Muungano wa Uafrika, tuzidi kuendelea
kwa maendeleo yaliyo bora. Lakini si bahati mbaya (kuwa
hawajatekeleza). Watanzania mjue kuwa si bahati mbaya. Bahati
nzuri, Muungano ndiyo huu hapa. Watanzania tena mnataka nini?
Muungano wa Tanzania ndiyo hatua ya mwanzo. Na msife moyo
wananchi wa Tanzania. Wenzetu wako jirani watakuja unga.
Muungano wa Tanzania ni kani inayoendeleza uhai wa dhamira ya
kuwaunganisha Waafrika na hivyo umeijengea heshima kubwa nchi yetu.
Uhai wa dhamira hiyo inayopata msukumo kutokana na Muungano wetu,
unajidhihirisha katika kuingia hatua ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika
(African Union) wenye nguvu zaidi kutoka hatua ya uliokuwa Umoja wa
Nchi Huru za Kiafrika (OAU). Na katika eneo letu la Afrika Mashariki,
hatua za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki zimefufuliwa kutokana na
uhai wa dhamira hiyo.
18
Kwa hivyo, nguzo hii ya msukumo wa kujenga umoja wa Afrika imeupa pia
Muungano wetu uhalali wa siasa za kimataifa, hasa Barani Afrika.
Watanzania wanajivunia heshima hii na wanapenda iendelee. Heshima hiyo
itaendelea tu kwa kuudumisha Muungano na kamwe si kwa kuudhofisha au
kuuvunja.
Nguzo ya Kisheria
Nguzo ya tatu inayouhimili na kuupa uhalali Muungano wa Tanzania ni
ukweli kwamba Muungano huo umesimama juu ya msingi wa sheria za nchi
na za kimataifa. Ulijadiliwa, ukatungiwa mkataba wa kimataifa (Hati ya
Muungano) ambao ulitiwa saini tarehe 22 Aprili, 1964 na Wakuu wa Nchi
(Marais Nyerere na Karume) na hatimae kuridhiwa na Mabaraza ya kutunga
sheria ya nchi zote mbili (yaani Bunge la Tanganyika na Baraza la
Mapinduzi la Zanzibar) kwa niaba ya wananchi wao.
Kama itavyoonekana baadae, wapo waliowahi kudhani kwamba kwa upande
wa Zanzibar, hatua za kuuhalalisha Muungano kisheria hazikutimia kwa
madai eti kwamba Hati ya Muungano haikuridhiwa na baraza la kutunga
sheria kwa niaba ya wananchi. Lakini hoja yao ilinyauka pale
walipozinduliwa kwamba wasilitazame Baraza la Mapinduzi kwa sura yake
ya Baraza la Mawaziri tu, bali walione pia katika sura yake ya pili
liliyokuwa nayo wakati huo ya Baraza la Kutunga Sheria.
19
Nguzo ya Uendelevu
Nguzo ya nne inayouhimili na kuupa uhalali wa kisiasa Muungano wa
Tanzania na ambayo inaendelea kuimarika kila kukicha, ni uendelevu wa
Muungano wenyewe. Hadi sasa, miaka arobaini baada ya kuasisiwa kwake,
Muungano huu unabaki kuwa mfano pekee Barani Afrika wa muungano wa
nchi zilizo huru uliodumu. Kama ilivyokwishagusiwa kabla, juhudi za
kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki mara tu baada ya uhuru, zilivia.
Ulijaribiwa pia Muungano wa Misri, Libya na Syria (ulioitwa Jamhuri ya
Umoja wa Kiarabu) katika miaka ya sitini, lakini haukufika mbali. Senegal
na Gambia nazo zilijaribu Senegambia katika miaka ya themanini lakini bila
ya mafanikio.
Kama itavyofafanuliwa baadae, Muungano wa Tanzania umefaulu majaribu
mengi. Badala ya kuudhofisha, majaribu hayo yamekuwa yakiuimarisha
zaidi. Muungano ulianza na mambo 11 tu katika orodha ya mambo ya
Muungano, lakini hivi sasa yamefikia 22. Wasioutakia mema Muungano
wamekuwa wakidai kwamba eti mambo yaliyoongezwa yaliingizwa
kinyemela na kwa kuiburuza Zanzibar. Lakini madai kama hayo ambayo
hayana chembe ya ukweli, mara nyingine yamekuwa yakiambatana na
unafiki. Kwa mfano, waliosimamia na kuhakikisha Usalama wa Taifa wa
Zanzibar unawekwa chini ya Serikali ya Muungano mwaka 1984, ndio hao
hao sasa wanaoongoza kampeni ya kutaka Watanzania na hasa Wazanzibari
waamini kwamba eti mambo yanaingizwa kiholela tu na kwa kuwaburuza
Wabunge wa Zanzibar kutokana na uchache wao Bungeni.
20
Ukweli ni kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayalinda vya kutosha
maslahi ya Zanzibar kwani inatamka wazi kwamba hakuna jambo
litaloongezwa au kupunguzwa katika orodha ya mambo ya Zanzibar ila kwa
thuluthi mbili ya kura za Wabunge wanaotoka Zanzibar na thuluthi mbili za
Wabunge kutoka Bara. Kwa hivyo, wingi wa Wabunge wa Bara hauna
nafasi ya kuwaburuza wenzao wa Zanzibar.
Itoshe tu kusisitiza kwamba uendelevu wa Muungano ni nguzo madhubuti
ya kuuhimili Muungano huu ambayo pia inaupa uhalali wa kisiasa za ndani.
Katika sehemu hii, zimezungumziwa nguzo nne zinazouhimili
Muungano wa Tanzania na hata kuupa sura mbali mbali za uhalali. Ni
kutokana na umadhubuti wa nguzo hizo ndiyo maana umehimili na
unaendelea kuhimili misukosuko mbali mbali kama itavyofafanuliwa
baadae. Katika hotuba yake ya kuliaga Bunge tarehe 28 Julai, 1995,
Rais Ali Hassan Mwinyi ambae alikuwa anastaafu wakati huo alisema
kwa fahari kubwa:-
Katika kipindi hiki Muungano wetu umepita katika tanuri la moto
na kutokea upande wa pili ukiwa bado imara na wenye nguvu.
Matatizo yaliyojitokeza yalishughulikiwa kwa ukamilifu na katika
hali ya maelewano baina ya pande zote mbili. Tumefanya pia
marekebisho katika Katiba ambayo nina imani yatazidi kuimarisha
Muungano wetu katika kipindi hiki cha mageuzi ya kisiasa na
kiuchumi.
21
SABABU ZA MUUNGANO
Kwa kadiri CCM inavyohusika, sababu kubwa na za msingi zilizowaongoza
Waasisi wa Muungano katika kuuanzisha ni hizi tatu zifuatazo:-
1. Kuurejesha na kuuthitibisha umoja wa watu waliokuwa
wametenganishwa.
2. Kutekeleza azma ya kujenga umoja wa Afrika.
3. Kulinda Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar.
Sababu mbili za kwanza zimekwishajadiliwa kwa kina hapo kabla na hivyo
hapana haja ya kuurejea mjadala huo. Kwa sababu ya tatu, ufafanuzi
unapatikana kutokana na maelezo ya Sheikh Thabit Kombo kama
alivyonukuliwa na Rais Mkapa katika hotuba yake ya maadhimisho ya
miaka 40 ya Muungano. Maelezo hayo yaliyotolewa kama faida ya
Muungano ni kama yafuatavyo:-
Matumaini ya kudumu kwa amani na usalama yamekuwa
makubwa kwa nchi zote mbili; wasiwasi mwingi wa usalama
umeondoka. Fikiri mwenyewe kusingekuwako muungano, na maadui
wa Zanzibar wakazidisha vitimbi vyao, kusingekuwako usalama wala
amani; si Bara wala si hapa Zanzibar. Lakini kwa nguvu za
muungano wakorofi wanasita kidogo
Lakini usingekuwako muungano tungekuwa na hasara kubwa, kwa
Tanganyika na kwa Zanzibar pia. Zanzibar pamoja na mapinduzi
yake, ingedumu katika wasiwasi kwamba mbinu zingeweza kutumika
kumrudisha Sultani. Na Tanganyika nayo pamoja na ukubwa wake,
isingekuwa salama kabisa kama kungekuwako vurugu visiwani hapa.
22
Maadui wangeweza kuitumia Zanzibar kuihujumu Tanganyika kwa
urahisi sana
Pamoja na kwamba kauli hiyo ya hadharani ilitoka muda mrefu baada ya
Mapinduzi, ipo kila sababu ya kuamini kwamba suala la usalama wa
Mapinduzi ya Zanzibar na hata Uhuru wa Tanganyika ni miongoni mwa
mambo yaliyozingatiwa wakati wa mazungumzo ya Muungano. Na pengine
ndilo lililochangia katika kuharakisha Muungano hasa ikizingatiwa ukweli
kwamba watawala waliopinduliwa Zanzibar walikuwa wamekimbilia nje
ambako wangeweza kupanga mbinu za kujaribu kurudisha utawala wao.
Hao ni maadui wa Mapindizi ambao wasingeweza kupuuzwa. Na hofu hiyo
ilithibitishwa na majaribio 17 ya mapinduzi yaliyofanywa bila ya mafanikio
na maadui wa Mapinduzi ya 1964. Muungano bila shaka una mchango
wake katika kuyaviza majaribio hayo.
Kumekuwa pia na hoja kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ulipata msukumo kutokana na vita baridi vya wakati huo kati ya Marekani
na Urusi na kambi zao. Hoja ni kwamba eti Marekani ndiyo iliyoshawishi
ufanyike Muungano kwa lengo la kuidhibiti Zanzibar eti isiwe Cuba ya
Afrika. Wana-CCM hawaafikiani na hoja hiyo. Mtazamo wao ni kwamba
kama kweli Wamarekani walikuwa na mawazo hayo, hawakwenda zaidi ya
kuomba Mungu tu tukio hilo litokee. Lakini wenyewe Watanganyika na
Wazanzibari waliungana kwa utashi wao na kwa maslahi yao. Hawakuwa
na habari na ndoto za Marekani na maslahi yake.
Katika hili, Rais Mkapa alitoa msisitizo ufuatao katika hotuba yake ya
maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano:-
23
wapo wanaodhani Muungano wetu ulikuwa lazima wakati ule kwa
sababu tu ya vita baridi duniani, na mapambano ya mataifa makubwa
kutafuta himaya barani Afrika. Swali linabaki. Vita baridi
vilikwisha, na harakati za wakubwa kujenga himaya Afrika nazo
zimekwisha. Lakini Muungano unaendelea, kwa nini? Kwa sababu
msingi wa Muungano haukuwa vita baridi, bali shauku kubwa
iliyozuiliwa na wakoloni kwa miaka mingi ya watu wa Tanganyika
na Zanzibar kuungana kama walivyokuwa zamani.
KWA NINI SERIKALI MBILI?
Muundo wa Muungano wa Tanzania ni wa Serikali mbili; yaani Serikali ya
Jamhuri ya Muungano ambayo inashughulikia mambo ya Muungano na
mambo yote ya Tanzania Bara (baada ya Serikali ya Tanganyika kufa) na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoshughulikia mambo yasiyokuwa ya
Muungano kwa upande wa Zanzibar.
Muundo huu umekuwa jambo la mjadala mkubwa na wenye kuendelea
miongoni mwa Watanzania. Wapo wanaouona muundo huu kuwa haufai
kwa kuwa ni tofauti na miungano mingine inayojulikana duniani. Wapo
wanaoamini kuwa unasababisha kero nyingi na hivyo haukidhi matarajio ya
Watanzania. Wapo wanaoamini kuwa haupendwi na Watanzania. Wapo pia
waliojaribu kujenga hoja kwamba eti Waasisi wa Muungano walipokuwa
wanaunganisha nchi hizi mbili, lengo lao la baadae lilikuwa ni muungano
wa Serikali moja na kwamba huu wa Serikali mbili ulikusudiwa uwe wa
muda tu. Wapo wengine waliojaribu kujenga hoja kwamba eti Waasisi hao
24
walichounda ni Shirikisho la Serikali tatu ambapo Serikali ya Tanganyika
imefichwa ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
CCM inatofautiana na mawazo yote hayo. Kufaa au kutokufaa na
kukubalika au kutokubalika kwa muundo huu kwa Watanzania kutajadiliwa
baadae chini ya Misukosuko Iliyohimiliwa Na Muungano.
Katika sehemu hii, inatazamwa dhamira halisi ya Waasisi katika kufikia
uamuzi wa Muundo huu. CCM inaamini kwamba Waasisi walikusudia
muundo wa Serikali mbili na walikuwa wanakijua walichokuwa wanafanya.
Wao wenyewe ndio walioijua zaidi dhamira yao kuliko wale wanaojaribu
kuitafsiri.
Kwa mnasaba huo, tunaanza na kuwanukuu kauli zao kama walivyosema
wenyewe.
Katika Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Mwalimu Nyerere
anaifichua dhamira yao na sababu za kuamua muundo wa Serikali mbili
kama ifuatavyo:-
Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi Moja mifumo ya kawaida ya
miundo ya Katiba ni miwili: Muungano wa Serikali Moja, au
Shirikisho la Serikali Tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta
Serikali yake, na Nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni Nchi Moja yenye
Serikali Moja. Katika mfumo wa pili kila Nchi itajivua madaraka
fulani ambayo yatashikwa na Serikali ya Shirikisho, na itakuwa
Serikali ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki.
25
Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja,
tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini
tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na
ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000)
na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano
wa Serikali Moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza
Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika;
hatukutaka tudhaniwe, hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha
ubeberu mpya. Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja.
Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa
Tanganyika. Zanzibar ingeendesha Serikali yake na kuchangia
gharama za kuendesha serikali ya Shirikisho; na Tanganyika
ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa
Tanganyika ndio hasa ungeendesha Serikali yake ya watu 12,000,000
na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya
Shirikisho la watu 12,300,000. Ni watu wanaofikiri kwa ndimi zao
wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa
ndogo. Gharama ya Serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo,
(waulizeni Wazanzibari) na wala Serikali ya Shirikisho isingekuwa
ndogo, hata bila gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na
gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.
Kwa hiyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika
gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya
Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na
Serikali yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni
26
kwamba tukiwa na Serikali Moja Tanganyika itaonekana kuwa
imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute muundo ambao utaiondolea
Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa
kuendesha Serikali mbili zenye uzito unaolingana.
Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa
Muungano wa Serikali Mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo
kama wapumbavu, tulitazama hali halisi yetu ilivyokuwa na tukabuni
mfumo utakaotufaa zaidi. ( uk.15 16).
Mzee Abeid Amani Karume kwa upande wake aliielezea kwa ushupavu
zaidi dhamira ya kuunda Muungano kwa kutumia neno la Kiingereza la
Union ili kuziba mwanya wa kubabaisha na shirikisho. Katika hotuba yake
ya maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano, Rais Mkapa alimnukuu Mzee
Karume kutokana na hotuba yake maarufu aliyoitoa siku za mwanzoni za
Muungano ambayo husikika sana katika redio. Katika nukuu hiyo Mzee
Karume alitamka yafuatayo:-
Leo tumekuja kuonana na nyinyi wananchi wote. Na ikiwezekana
kuusia mambo. Sababu baadhi ya watu wengi, wanataka kufahamu
(kuhakikishiwa kwamba) Serikali ya Unguja (kwa maana ya
Zanzibar) na Serikali ya Tanganyika zimechanganyika, zimekuwa
Union moja tu.
Kwa hivyo, ni dhahiri kabisa kwamba walipoamua muundo huo wa
Muungano walikuwa wanajua walichokuwa wanakifanya na walichokuwa
wanakitaka. Na wala haina maana kwamba labda walipoamua muundo huo
27
walidhani hautokuwa na matatizo. Matatizo walijua yatakuwepo lakini
waliamua kwa makusudi wakabiliane nayo ndani ya Muungano badala ya
kusubiri yamalizike kwanza ndio waunganishe nchi. Ukweli huo
unadhihirishwa katika kitabu cha ASP cha Maendeleo ya Mapinduzi ya
Afro-Shirazi Party 1964 1974 kama ifuatavyo:-
Nchi mbili huru, kama zilivyokuwa Zanzibar na Tanganyika,
zinapoungana, kuna njia mbili za kuunganisha. Njia ya kwanza ni
kuungana kwa yale wanayokubaliana, hata yakiwa ni machache,
madamu tu nia ipo, ni kuitekeleza ile nia na halafu zikaendelea
kutanzua matatizo yao na kujenga juu ya ile nia iliyokwisha
kutekelezwa. Njia ya pili ni kukaa na kutanzua matatizo kwa
makubaliano mpaka kifikilie kima cha makubaliano kiwezacho kuleta
muungano. Zote hizi njia mbili si rahisi na kila moja ina matatizo
yake yanayoweza kuchukua muda mrefu kutanzuliwa. Tanganyika na
Zanzibar zilichukua njia ya kwanza, siyo kwamba ndiyo iliyokuwa
rahisi, bali kwa sababu nchi mbili hizi zilikubaliana na kutekeleza nia
yao ya kuungana na kutanzua matatizo yaliyosalia ya muungano huku
zimo katika Muungano. (uk.33).
Kwa hivyo, matatizo ambayo yamekuwa yakiukabili Muungano ambayo
mengine yamefikia kuutia katika misukosuko mikubwa hayawezi yakawa ni
kioja, kwani yalitabiriwa. Hata hivyo, kuendelea kuimarika kwa Muungano
ndani ya mazingira ya matatizo hayo, ni kielelezo cha udhati wa nia ya
kuungana na usahihi wa uamuzi wa kuteua muundo wa Serikali mbili.
28
Katika hotuba yake ya kihistoria iliyoimarisha hoja ya Muungano tarehe 26
Aprili, 2004 kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya Muungano,
Rais Mkapa alitoa majumuisho mazuri ya suala hili kama ifuatavyo:-
Muungano wetu umefikisha miaka 40, na upo imara. Nguvu yake ni
Watanzania wenyewe, wengi wao asilimia 84.8 wakiwa hawajui
uraia mwingine isipokuwa Utanzania. Watanzania hawa waliozaliwa
mwaka 1964 na kuendelea, ambao leo wana umri wa miaka 40 au
chini zaidi, hawana uzoefu wa kuwa kitu kingine isipokuwa kuwa
Watanzania.
Na hawajui mfumo mwingine wa Muungano isipokuwa mfumo wa
Serikali mbili, wenye manufaa mawili makubwa ambayo ni sehemu ya
msingi wa Muungano wetu. Kwanza, mfumo huu unadhihirisha
kuwa kweli sisi tumeungana, serikali yetu ni muungano, si
shirikisho. Na, muungano ni imara kuliko shirikisho.
Msingi wa pili ni madaraka kamili ya Zanzibar kwa mambo ambayo
si ya muungano. Madaraka hayo yanasaidia kuhakikisha kuwa
Zanzibar inahifadhi utambulisho wake na haimezwi na Tanzania
Bara. Wapo wanaoamini kuwa mfumo huu hauna haiba nzuri; ati
haupendezi. Kwao napenda kusema kuwa jambo muhimu kuliko yote
katika msingi wa nyumba si sura yake, muhimu zaidi ni uimara wake.
Na mimi nakuhakikishieni, Ndugu Wananchi, kuwa mfumo wa Serikali
mbili ndicho chombo imara kilichotuvusha salama katika bahari ya
miaka 40 iliyopita, na Inshallah, ndicho kitatuvusha salama katika
miaka ijayo.
29
MISUKOSUKO ILIYOHIMILIWA NA MUUNGANO
Kama ilivyokwishaelezewa, Muungano umeweza na unaendelea kuhimili
misukosuko mingi. Misukosuko hiyo imekuwa ni changamoto
inayouwezesha kujidhatiti zaidi, kwani kila unapoishinda changamoto moja,
unaibuka imara zaidi. Hii ni kwa sababu changamoto hizo huwafanya
wahusika, hasa Serikali zote mbili, kutoa ufafanuzi kusafisha upotoshaji
unaotolewa au kuyafanyia kazi na kuyapatia ufumbuzi matatizo
yanayojitokeza ambayo hutumiwa kuutia misukosuko Muungano.
Awali, misukosuko ilijikita zaidi katika kuhoji uhalali wa Muungano
wenyewe. Baadae, baada ya shaka kuondolewa kuhusu uhalali wake,
misukosuko imeelekea zaidi katika kuhoji muundo wa Serikali mbili.
Kuhoji Muungano Wenyewe
Hoja ya kwamba Muungano haukuwa halali kwa sababu eti haukupata
ridhaa ya wananchi na haukukamilisha taratibu za kisheria zilianza kusikika
hadharani Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya themanini. Seif Sharif Hamad
na wenzake ambao baadae walikiri kuwa walikuwa wapinzani ndani ya
CCM na Serikali, waliitumia fursa iliyotolewa kwa nia njema na CCM ya
kuanzisha mjadala wa kitaifa wa marekebisho ya Katiba kutaka kuudhofisha
au hata kuuvunja Muungano. Watu hao hao ni wale wale ambao baada ya
kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi waliunda chama chao cha CUF
katika miaka ya tisini.
30
Kipindi hicho cha msukosuko wa kwanza mkubwa kuutikisa Muungano
kilikuwa baina ya 1983 na 1984 na kinajulikana kwa umaarufu wa
kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar. Madai yaliyokuwa
yameshika nguvu wakati huo ni ya kudai kura ya maoni ya wananchi ili eti
kuupa uhalali Muungano huo na kukamilisha hatua za kisheria.
Imekwishaelezewa kwa kina katika sehemu ya Nguzo za Muungano jinsi
Muungano ulivyo na uhalali unaotokana na watu wenyewe, na kwamba
umekidhi matakwa ya sheria.
Mtazamo wa CCM kuhusu kura za maoni ni kwamba si jambo la lazima na
wala si njia pekee ya kupima utashi wa wananchi. Hadi wakati Tanganyika
na Zanzibar zinaungana hakukuwa na nchi duniani zilizokuwa zimeungana
baada ya kuitishwa kura za maoni. Miungano mikubwa mikubwa iliyodumu
na iliyo madhubuti kabisa kama ile ya Marekani (USA) na Uingereza (UK)
haikuanzishwa kwa kura za maoni. Na wala hadi leo haikupigiwa kura za
maoni za kuithibitisha. Kinyume chake,Marekani iliwahi kuingia katika vita
vya wenyewe kwa wenyewe kuulinda Muungano baada ya majimbo ya
Kusini kutaka kujitoa. Wanaolalamikia Muungano hupenda kutaja mifano
ya nje kuzipa nguvu hoja zao, lakini mifano hii ya Marekani na Uingereza
hawaitaji katika muktadha huu. Kwa mazingira ya wakati ule na hasa
kuzingatia usalama wa Mapinduzi ya Zanzibar, isingeweza kutumika njia
nyengine zaidi ya iliyotumika. Hata hivyo, suala hili la kura ya maoni
lilikuwa agenda kuu ya uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa
1990 ambapo Dr. Salmin Amour alichaguliwa kuwa Rais wa tano wa
Zanzibar. Uchaguzi huo uliambatana na kampeni kubwa ya chini kwa chini
iliyowataka watu waususie hadi kwanza itapoitishwa kura ya maoni.
31
Inasadikiwa katika CCM kwamba kampeni hiyo iliongozwa na kundi la
wanasiasa chini ya uongozi wa Seif Sharif Hamad waliokuwa wamefukuzwa
kutoka CCM kwa sababu za usaliti. Ni watu hao hao ndio wanasadikiwa pia
kuongoza kampeni ya chini kwa chini ya kutaka Sheikh Idris Abdul-Wakil
apigiwe kura za HAPANA wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 1985.
Kampeni zote hizo hazikufanikiwa. Kushindwa kwa kampeni ya 1990
iliyotaka kura za maoni kuliidhoofisha kwa kiasi kikubwa hoja ya kwamba
Muungano eti Wazanzibari hawakuwa wameuridhia. Kujitokeza kwa wingi
kwa wananchi kupiga kura na kumchagua Dr. Salmin Amour ambae
kampeni yake na ya CCM ilikuwa ya kupinga kura za maoni ulikuwa
ushahidi wa kutosha kwamba Wazanzibari hawakuwa na tatizo na
Muungano.
Kwa upande wa uhalali wa kisheria, kitendawili kiliteguliwa na Tume ya
Chama Kimoja au Vyama Vingi (maarufu Tume ya Nyalali) katika miaka ya
tisini. Tume hiyo ilijiridhisha kwamba Baraza la Mapinduzi la Zanzibar
likikaa kama Baraza la Kutunga Sheria, liliiridhia Hati ya Muungano kama
lilivyofanya Bunge la Tanganyika, na hivyo kukamilisha taratibu za
kisheria.Profesa Haroub Othman katika makala yake ya Forty Years of the
Union: Is It Withering Away? naye kwa njia zake amejiridhisha hivyo.
Ugunduzi huu ukawa umeimaliza kabisa hoja dhidi ya uhalali wa
Muungano. Kilichoendelea kutokea baada ya wakati huo katika mjadala wa
Muungano yakawa ni masuala ya muundo na kero za Muungano tu.
32
Kuhoji Muundo wa Serikali Mbili
Baada ya uhalali wa Muungano kuthibitika bila ya chembe ya shaka, sasa
hoja zimehamia kwenye muundo, labda na kero za Muungano.
Kabla ya kuendelea na uchambuzi, kwanza tuwatazame hao wanaouandama
Muungano, hasa upande wa Zanzibar. Vitimbi vya wasaliti wa Chama
wakati wa Chaguzi Kuu za 1985 na 1990 vimekwishaelezwa. Lakini ni
kundi hilo hilo ndilo lililokuwa mapema zaidi (mwaka 1984) limemfitini
katika Chama (CCM) Rais wa pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe
kwamba alikuwa anataka kuvunja Muungano kwa azma yake ya kutaka
kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Ni kutokana na fitina hizo ndio
akalazimika kujiuzulu. Wakati huo walijifanya wapenzi wakubwa wa
Muungano na wenye uchungu mkubwa nao. Lakini kufikia 1990, wakautilia
shaka kiasi cha kutaka kuuitishia kura za maoni. Kufikia 1992, waliunda
chama chao cha CUF na sera yao ya Muungano ikawa ya Serikali tatu. La
kujiuliza ni jee, inakuwaje sera ya Serikali tatu ya Jumbe iwe ya
kuvunja Muungano lakini sera ya Serikali tatu ya CUF isiwe ya
kuvunja Muungano? Pamojawapo lazima pana unafiki. Ili kupabaini,
tutazame historia kidogo.
Kwamba muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilikuwa sera ya ASP toka
wakati wa kudai uhuru, hapana ubishi. Sheikh Thabit Kombo amethibitisha
hivyo kwa uwazi. Lakini kwa upande wa pili, inajulikana pia kwamba
chama cha Hizbu kilikuwa kinaipinga vikali sera hiyo. Kauli mbiu ya
chama hicho ilikuwa ASP itaiuza Zanzibar kwa Nyerere. Aidha, Hizbu
ilijenga chuki dhidi ya watu wenye asili ya Bara na kuna wakati kwa
33
ushawishi wake, Sultani alitoa meli ya kuwarejesha kwao Wabara. Hata
hivyo wito huo haukuitikiwa vyema kwani hao Wabara walijua kwamba
Zanzibar walikuwa kwao.
CCM inaamini kwamba waliokuja unda CUF wana mnasaba na Hizbu, na
zaidi, CUF iliundwa kutokana na ushawishi wa waliokuwa viongozi wa
Hizbu. Kama Hizbu haikutaka Muungano, hapawezi kuwa na taabu sana
kuamini kwamba na CUF iliyochipua kutoka kisiki chake haijaukinai
kikweli Muungano. Ikumbukwe kwamba Ilani ya Kwanza ya Uchaguzi ya
CUF ilizungumzia kuirejesha Zanzibar ya zamani. Kwa hivyo, madai ya
kura ya maoni na sera ya Serikali tatu ni visingizio tu vya kilaghai
vinavyoficha nia ya CUF ya kuvunja Muungano. Halikadhalika, Wana-
CCM wengi hawaamini kwamba ile fitina dhidi ya Jumbe waliyoifanya
viongozi wa sasa wa CUF walipokuwa ndani ya CCM na Serikali ilikuwa
kielelezo sahihi na cha kweli cha imani yao kwa Muungano.
Ni kutokana na mtazamo huo ndio maana CCM inaamini kwamba CUF
hawautaki Muungano, lakini maadam hawawezi kusema hivyo bayana
kutokana na kuujua ukweli kwamba Muungano umekwishajikita ndani ya
nyoyo za Wazanzibari na Watanzania kwa jumla walio wengi, jitihada
wanazofanya ni kutafuta fursa za kuutia misukosuko kwa lengo la
kuudhoofisha au hata kuuvunja. Ndio hizo kelele za kura ya maoni na sera
ya Serikali tatu.
Vyama vingine vya upinzani ambavyo nguvu zake ziko zaidi Bara navyo
vina sera ya Serikali tatu. Lakini kwao wao Sera hii inaelekea kuchochewa
zaidi na hasira tu ya Zanzibar kujiunga na OIC; hasira waliyoidaka kutokana
34
na kundi la Wabunge wa CCM (maarufu G 55) waliopeleka hoja Bungeni
mwaka 1993 kutaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Hili
litazungumziwa zaidi baadae. Sababu nyengine ya sera ya Serikali tatu kwa
vyama hivyo pengine tu ni kuwa na kitu tofauti na CCM.
CCM inaamini kwamba kuanzisha Shirikisho la Serikali Tatu kutoka
Muungano wa Serikali Mbili ni kurejea nyuma na kuudhofisha Muungano.
Tendo hilo litajenga mazingira ya hata kuuvunja kabisa Muungano. Maneno
yafuatayo ya Mwalimu Nyerere yaliyomo katika Uongozi Wetu na Hatima
ya Tanzania yanatoa kwa majumuisho ujumbe huo:-
mimi nasema, ukifufua Tanganyika,utaua Tanzania. Fahali wawili
hawakai zizi moja. Yeltsin wa Tanganyika ataua Tanzania. (uk. 6)
Alipozungumzia Yeltsin, Mwalimu alikuwa akimaanisha jinsi Muungano
wa Kisovieti ulivyosambaratika. Yeltsin alipoingia katika madaraka ya
kuwa Rais wa Russia, Jamhuri iliyokuwa kubwa kuliko zote zilizokuwa
ndani ya Muungano wa Kisovieti na akaamua kujitenga, Muungano huo
ulisambaratika kwa urahisi tu. Hilo linaweza kutokea kwa urahisi pengine
zaidi ya huo kama Tanganyika inafufuliwa na kuwa na Serikali yake na
Serikali hiyo ikapata viongozi wasiotaka Muungano.
Muungano wa Serikali Mbili Ulivyoweza Kuhimili Misukosuko
Kama ilivyokwishaelezwa, Muungano, katika muundo wake huu wa Serikali
mbili umeweza kuhimili misukosuko mingi na mikubwa, na kufaulu
35
majaribu kadha. Katika sehemu hii tutajaribu kubainisha misukosuko na
majaribu hayo na jinsi Muungano ulivyoyashinda.
Kuchafuka Kwa Hali ya Hewa ya Kisiasa Zanzibar (1982 1984)
Mtikisiko uliopata Muungano katika kipindi hicho umekwishaelezewa.
Itoshe tu kueleza kwamba baada ya malumbano makali na hoja za nguvu na
jazba za kuhoji uhalali wa Muungano, Katiba za Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano zilifanyiwa marekebisho makubwa. Katiba ya Zanzibar ni kama
iliandikwa upya (kutokana na ile ya 1979) ndiyo maana inaitwa Katiba ya
1984. Katiba hiyo ilipanua upeo wa demokrasia Zanzibar na iliwiyanishwa
vizuri zaidi na ile ya Jamhuri ili kupunguza migongano. Katiba ya Jamhuri
nayo iliongezewa mambo katika orodha wa mambo ya Muungano ikiwa ni
mwelekeo wa kuimarisha Muungano.
Uchaguzi Mkuu wa 1990
Kampeni ya chini kwa chini ya kuwataka Wazanzibari wasusie Uchaguzi
Mkuu wa 1990 hadi iitishwe kura ya maoni kwanza, imekwishaelezewa.
Itoshe tu kusisitiza kwamba Wazanzibari waliipuuza kampeni hiyo na
wakajitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo na hivyo kuthibitisha imani
yao kwa Muungano.
Mjadala wa Mfumo wa Chama Kimoja Au Vingi (1991 1992)
Kufuatia upepo wa mageuzi ya kisiasa uliokuwa unavuma Duniani wakati
huo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliunda Tume ya
36
kuratibu maoni ya wananchi na hatimae kupendekeza kama Tanzania
iendelee na Mfumo wa Chama Kimoja au iingie katika Mfumo wa Vyama
Vingi. Tume hiyo imepata umaarufu wa Tume ya Nyalali kutokana na jina
la Mwenyekiti wake.
Katika kufanya kazi yake, Tume hiyo pia ilitaka na kupokea maoni ya
wananchi kuhusu muundo wautakao wa Muungano.
Kama inavyoeleweka, Tume ilipendekeza kwamba Tanzania iingie katika
Mfumo wa Vyama Vingi pamoja na ukweli kwamba asilimia 80 ya
wananchi waliotoa maoni yao walitaka Mfumo wa Chama Kimoja uendelee.
Pendekezo hilo la Tume lilikubaliwa.
Kuhusu suala la muundo wa Muungano, Tume ilipendekeza muundo wa
Shirikisho la Serikali Tatu. Pendekezo hilo lilikataliwa na CCM na baadaye
Bunge kwa sababu za kisera kama zilivyokwishaelezwa lakini pia kwa
sababu haukupatikana kabisa ushahidi kwamba watu wenyewe waliutaka
muundo huo.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume, ni Watanzania 49 (sawa na asilimia
0.13) tu kati ya wote 36,279 waliotoa maoni yao ndio waliotaka muundo huo
wa Serikali Tatu. Uchambuzi unaonekana katika Jedwali na. 3 hapo chini:
37
JEDWALI Na. 3: WATANZANIA WALIOTAKA MUUNDO WA
SERIKALI TATU
Washiriki Wote Waliotaka Asilimia
Tanzania Bara 32,279 45 0.13
Zanzibar 3,000 4 0.13
Tanzania 36,299 49 0.13
Chanzo: Kiambatanisho cha Tume ya Nyalali (Uk.i) (pamoja na makosa ya
hesabu)
Hakukuwa na maafikiano ndani ya Tume yenyewe kuhusu pendekezo hili
kwani Wajumbe tisa walipinga na wakaandika maoni yao (dissenting
opinion). Miongoni mwa hoja nyingi zenye uzito mkubwa za kukataa
pendekezo hili walizotoa wajumbe hao, ilikuwamo ifuatayo:-
Pamoja na kuelewa kuwa kwa baadhi ya mambo mengine ya kisiasa
sio lazima uamuzi wake kutegemea wingi wa watoa maoni, lakini pia
tunaona kuwa sio busara kupendekeza mabadiliko makubwa kama
haya ya mfumo wa Muungano wetu kwa kutegemea maoni ya
Watanzania 49 kati ya Watanzania 36,299 walioshiriki katika mjadala
wote ulioendeshwa na Tume ya Rais. Idadi hii ni ndogo isio na uzito
wa kitakwimu (statistically insignificant).
Hoja hiyo pamoja na nyengine za wajumbe hao waliotofautiana na wenzao
ziliwavutia Wabunge ambao kwa hivyo, walilikataa pendekezo la Serikali
Tatu mwezi wa Aprili, 1992.
Hoja ya G 55 (1993)
38
Baada ya uamuzi wa kuingia katika mfumo wa Vyama Vingi, ilibidi baadhi
ya vifungu vya Katiba vihitaji marekebisho. Rais Ali Hassan Mwinyi,
mwishoni mwa 1992, aliunda Kamati ya kupendekeza marekebisho hayo
ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mark Bomani. Miongoni mwa mambo
iliyotakiwa iyatazame ni namna ya kupata Makamu wa Rais katika mfumo
wa vyama vingi ambao utafungua milango ya uwezekano wa Rais wa
Jamhuri na yule wa Zanzibar kutoka vyama tofauti. Wakati huo wa mfumo
wa Chama Kimoja, Rais wa Zanzibar alikuwa moja kwa moja Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano. Lakini ujio wa vyama vingi ulileta hofu ya
uwezekano wa kuigawa Taasisi ya Rais (inayojumuisha Makamu wa Rais)
katika itikadi zinazopingana ikitokezea Rais na Makamu wake kutoka
vyama tofauti.
Kamati hiyo ilipendekeza kwamba Makamu wa Rais apatikane kwa
utaratibu wa Mgombea Mwenza ili kuhakikisha kuwa wote wanatoka chama
kimoja. Pamoja na pendekezo jengine kwamba kama Rais anatoka upande
mmoja wa Muungano, Makamu wa Rais atoke wa upande wa pili, utaratibu
huu ulikuwa unamwondoa Rais wa Zanzibar katika Umakamu wa Rais wa
Jamhuri.
Zanzibar ilisita kulikubali pendekezo hilo kwa madai kwamba haliendani na
dhamira ya makubaliano yaliyomo katika Hati ya Muungano ingawa baadae
iliridhia lifikishwe Bungeni ambako lilipitishwa. Wakati mashauriano
kuhusu suala hilo yakiendelea, Zanzibar ilijiunga na Umoja wa nchi za
Kiislamu (OIC).
39
Ilikuwa katika mazingira hayo lilipoibuka kundi la Wabunge walioanzia 44
hadi kufikia 55 waliowasilisha Bungeni hoja ya kutaka ianzishwe Serikali ya
Tanganyika ndani ya Muungano, Agosti, 1993. Wabunge wote hao
walikuwa wa CCM na wa kutoka Bara.
Kabla ya hapo, mjadala kuhusu Muungano na muundo wake ulikuwa zaidi
mkali Zanzibar. Makelele mengi dhidi ya Muungano yalisikika zaidi
Zanzibar kuliko Tanzania Bara. Inaelekea dhahiri kwamba msimamo wa
Zanzibar kuhusu Makamu wa Rais na OIC ndio uliochangia kwa kiasi
kikubwa kuamsha hisia na hata hasira miongoni mwa Wabunge hao wa Bara
na waliowaunga mkono. Uamuzi wa Zanzibar kujiunga na OIC ulihusishwa
na kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa vile hoja
yao ilipitishwa na Bunge, ni dhahiri kwamba Wabunge hao walipata
uungwaji mkono mkubwa. Tukio hilo ndilo lililoupa Muungano mtikisiko
wa kweli na mkubwa pengine kuliko yote ya kabla na baadae. Taifa
lilikuwa katika hatari ya kweli ya kugawanyika na Muungano kuvunjika.
Kipindi chote cha 1993-1994 kilikuwa kigumu sana kikihanikizwa na
mijadala mikali mikali ndani ya Chama na Serikali na katika jamii. Azimio
la Bunge ambalo dhahiri lilikuwa kinyume na sera ya CCM lilileta
mtafaruku mkubwa ndani ya Chama.
Baada ya mashauriano ya muda mrefu, Zanzibar ilijitoa katika OIC.
Hatimae Chama kiliamua kufanya uhakiki wa mtazamo wa wanachama
kuhusu muundo wa Muungano ili kujiridhisha kama kweli Wabunge
walizisoma kwa usahihi hisia za wanachama au la. Tarehe 12 14
Novemba, 1993, ulifanyika Mkutano Maalumu wa Pamoja kati ya
40
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Wajumbe wa Kamati ya Wabunge wa
CCM, Wajumbe wa Kamati ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa
CCM, na Mawaziri wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Mkutano huo ulifanyika Dodoma.
Mkutano huo uliamua kwamba kwa kuwa suala la kutazama upya Muundo
wa Muungano linahusu Sera ya CCM, wana-CCM waulizwe juu ya suala
hili na watoe maoni yao.
Kura za maoni za siri za wana CCM zilipigwa nchi nzima mwezi Aprili,
1994 na matokeo yalikuwa kama inavyoonekana katika Jedwali na. 4,5 na 6
hapa chini:
JEDWALI Na. 4: MATOKEO YA KURA ZA SIRI ZA WANA-CCM
WA TANZANIA NZIMA
Mtazamo Idadi Asilimia
Waliotaka Serikali moja 394,157 29.21
Waliotaka Serikali mbili 833,285 61.75
Waliotaka Serikali tatu 112,934 8.37
Kura zilizoharibika 9,115 0.67
Jumla ya Wote walioshiriki 1,349,501 100.00
Chanzo: CCM Makao Makuu
41
JEDWALI Na. 5: MATOKEO YA KURA ZA SIRI ZA WANA-CCM
WA ZANZIBAR
Mtazamo Idadi Asilimia
Waliotaka Serikali moja 452 0.52
Waliotaka Serikali mbili 85,175 98,78
Waliotaka Serikali tatu 386 0.45
Kura zilizoharibika 214 0.25
Jumla ya Wote walioshiriki 86,227 100.00
Chanzo: CCM Makao Makuu
Jedwali Na. 6: MATOKEO YA KURA ZA SIRI ZA WANA-CCM WA
TANZANIA BARA
Mtazamo Idadi Asilimia
Waliotaka Serikali moja 393,715 31.17
Waliotaka Serikali mbili 748,110 59.22
Waliotaka Serikali tatu 112,548 8.91
Kura zilizoharibika 8,901 0.70
Jumla ya Wote Walioshiriki 1,263,274 100.00
Chanzo: CCM Makao Makuu
Matokeo hayo yalionyesha kwamba asilimia 61.75 ya wanachama wote wa
CCM walioshiriki katika kura hiyo ya maoni bado walikuwa na imani na
sera ya Chama chao ya Serikali mbili, na hivyo kuithibitisha tena. Imani
hiyo kwa upande wa Zanzibar ilikuwa kubwa zaidi (asilimia 98.78).
Muundo wa Serikali Tatu waliotaka kuulazimisha Wabunge uliungwa
mkono na asilimia 8.37 tu ya wanachama na ndio uliothibitika kukataliwa
42
kabisa na wanachama ambapo ulishindwa hata na ule wa Serikali Moja kwa
pande zote mbili za Muungano.
Baada ya kura hiyo ya maoni iliyothibitisha kwamba Wabunge walienda
mchomo, Wabunge walilazimika kurudi kwenye mstari kwa kuifuta hoja
yao Bungeni. Aidha, toka wakati huo, CCM ilianza kuhakikisha kwamba
sera ya Muundo wa Serikali Mbili inaingizwa bayana katika Ilani zake za
Uchaguzi. Kabla ya hapo, ilikuwa ikilichukulia tu kuwa ni jambo
linaloeleweka.
Kabla ya CCM kuamua kuendesha kura kwa wanachama wake tu
zilikuwapo hoja kwamba kura ya maoni ilipaswa iwe ya wananchi wote.
Mwalimu Nyerere aliijibu hoja hiyo kama ifuatavyo kama alivyojinukuu
katika Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania:-
Muundo wa Muungano, pamoja na kwamba hatutaki uwe ukitibuliwa
tibuliwa mara kwa mara, ni suala la sera, si amri ya Mungu. Vyama
vya siasa mbali mbali vinaweza vikawa na maoni mbali mbali kuhusu
muundo unaofaa kwa katiba ya Nchi yetu. Muundo utakaokubaliwa
na Wananchi walio wengi ndio utakaokuwa sehemu ya Katiba ya
Nchi. Muundo wa Serikali mbili unakubaliwa na Wananchi, lakini
unatokana na sera ya TANU na ASP na kwa sasa CCM. Maoni ya
Wananchi yanaweza kukifanya Chama kibadili sera zake; lakini si
lazima. Chama chochote kinaweza kubadili sera zake bila kutafuta
kwanza maoni ya Wananchi. Siku ya Uchaguzi Mkuu maoni ya
Wananchi yatajulikana. (uk. 29)
43
Uchaguzi Mkuu wa 1995
Uchaguzi Mkuu wa 1995 ndio uliokuwa wa kwanza kufanyika ndani ya
mfumo wa vyama vingi baada ya Uhuru na Mapinduzi. Vyama vyote vya
upinzani viliendesha kampeni ya bidii kubwa ya kupinga muundo wa
Serikali Mbili na viliwaahidi wananchi kwamba kama vitachaguliwa
vitaanzisha muundo wa Serikali Tatu. Matokeo yake ni kwamba
vilishindwa vibaya na huo ni ujumbe wa dhahiri kwamba sera ya Muundo
wa Serikali Tatu ilikataliwa na wananchi. Badala yake, kwa ushindi
mkubwa wa CCM, Muungano wa muundo wa Serikali Mbili ulithibitishwa
tena na Watanzania.
Kamati Ya Kuratibu Maoni Kuhusu Katiba (1999)
Mwaka 1999, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilitoa waraka wa
mapendekezo (white paper) kuhusu mambo mbali mbali iliyokuwa inafikiria
kuyazingatia wakati wa marekebisho ya Katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa
2000. Rais aliunda Kamati ya Kuratibu maoni ya wananchi kuhusu
mapendekezo ya Serikali yaliyokuwamo katika waraka huo. Kama kawaida,
Kamati hiyo imepewa umaarufu wa Mwenyekiti wake, Jaji Kisanga.
Suala la muundo wa Muungano kwa mara nyingine tena, lilikuwa miongoni
mwa mambo yaliyotakiwa maoni ya wananchi. Lakini kwa mara nyingine
tena, Watanzania walioshiriki kutoa maoni yao walithibitisha imani yao kwa
muundo wa Serikali Mbili kwa kiwango cha asilimia 88.87, ambapo
Zanzibar ilikuwa asilimia 96.25 na Bara asilimia 84.97. Muundo wa
Serikali tatu ulipata asilimia 4.32 tu ambapo Zanzibar ilikuwa asilimia 3.48
44
na Bara asilimia 4.76. Jedwali Na. 7, 8 na 9 hapo chini zinatoa uchambuzi
wa takwimu za matokeo hayo.
JEDWALI Na. 7: MAONI YA WANANCHI WA TANZANIA
KUHUSU MUUNDO WA MUUNGANO UNAOFAA
Mtazamo Idadi Asilimia
Waliotaka Serikali moja 4,326 6.54
Waliotaka Serikali mbili 58,750 88.87
Waliotaka Serikali tatu 2,855 4.32
Waliotaka Miundo Mingineyo 174 0.26
Wote walioshiriki 66,105 100.00
Chanzo: Ripoti ya Kamati Ya Kisanga
JEDWALI Na. 8: MAONI YA WANANCHI WA ZANZIBAR
KUHUSU MUUNDO WA MUUNGANO UNAOFAA
Mtazamo Idadi Asilimia
Waliotaka Serikali moja 41 0.18
Waliotaka Serikali mbili 22,017 96.25
Waliotaka Serikali tatu 797 3.48
Waliotaka Miundo Mingineyo 19 0.08
Wote Walioshiriki 22,874 100.00
Chanzo: Ripoti ya Kamati ya Kisanga
45
JEDWALI Na. 9: MAONI YA WANANCHI WA TANZANIA BARA
KUHUSU MUUNDO WA MUUNGANO UNAOFAA
Mtazamo Idadi Asilimia
Waliotaka Serikali moja 44,285 9.91
Waliotaka Serikali mbili 36,733 84.97
Waliotaka Serikali tatu 2,058 4.76
Waliotaka Miundo Mingine 155 0.36
Wote Walioshiriki 43,231 100.00
Chanzo: Ripoti ya Kamati ya Kisanga
Kama ilivyofanya Tume ya Nyalali, Kamati hii nayo iliyaacha maoni ya
wananchi na badala yake ikapendekeza Muundo wa Serikali Tatu kwa
kutumia hoja za jazba na maneno mengi. Haishangazi kwamba na Kamati
hii nayo ilikuwa na kikundi cha wajumbe wake walioandika maoni tofauti
(dissenting opinion) kwa suala hili kama ilivyokuwa kwa Tume ya Nyalali.
Pendekezo hilo la muundo wa Serikali Tatu lilikataliwa na Serikali.
Uchaguzi Mkuu wa 2000
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2000, Muungano wenye Muundo wa Serikali
Mbili ulitiwa tena kwenye mtihani. Wapinzani waliuza tena sera ya Serikali
Tatu na CCM iliendelea kuuza sera yake ya Serikali Mbili. CCM ilishinda
kwa ushindi mkubwa zaidi kuliko hata ule wa 1995. Muungano ukapasi
tena mtihani huu.
46
MAFANIKIO YA MUUNGANO
Kama alivyosema Rais Mkapa kwenye kilele cha sherehe za kuadhimisha
miaka 40 ya Muungano, kule kudumu hadi kufikia miaka 40, pakee ni
mafanikio ya Muungano hata kama hakuna mafanikio mengine, hasa
ikizingatiwa kwamba umeruka vihunzi vingi. Lakini yapo mafanikio
mengine mengi ya msingi. Kwanza kurejesha na kudumisha umoja na
udugu wa watu waliokuwa wametenganishwa na wakoloni ni mafanikio
yasiyo kifani. Muungano umefanikiwa kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar na
uhuru wa Tanganyika, na kuhakikisha amani na utulivu wa nchi. Hali hiyo
imewezesha kushughulikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi tunayoyafaidi
hivi sasa. Muungano umesaidia kuharakisha kurejeshwa kwa demokrasia
Zanzibar na umekuwa muhimili wa utulivu (stabilizing factor) kwa siasa za
ndani za Zanzibar. Muungano umefungua milango ya fursa kwa wananchi
kujiendeleza kiuchumi bila ya kujali upande gani wa Muungano mtu
anatoka.
Muungano umekuwa muhimili madhubuti wa umoja siyo wa Tanzania
nzima tu, bali pia wa kila upande wa Muungano huo, yaani Tanzania Bara
(Tanganyika) na Zanzibar. Katika Hotuba yake ya kihistoria ya tarehe 13
Machi, 1995 kwenye mkutano wa waandishi wa habari Hoteli ya
Kilimanjaro, Dar es Salaam wakati vumbi la hoja ya Tanganyika (ya G55)
halijatulia vyema; hotuba ambayo imeandikwa katika kitabu cha Nyufa,
Mwalimu Nyerere aliifafanua dhana hiyo kama ifuatavyo:-
Watu wazima wamezungumza Muungano, kwamba tuuvunje au
uendelee. Ilikuwa ipo hatari ya kuvunjika na wala haijaisha. Watu
47
wamezungumza Uzanzibari, baadhi ya viongozi wetu! Nadhani
wengine wanafikiria hata kujitenga. Wapo, si wengi; lakini wapo.
Kujitenga maana yake ni kuvunja nchi ivunjike tusiwe na nchi moja,
tuwe na nchi mbili. Ni jambo linalozungumzwa. Tunataka kiongozi
na viongozi watakaoelewa hivyo. Huku kuzungumza Uzanzibari si
fahari. Si jambo la fahari. Hatima yake itavunjika Zanzibar. Mtu
mwenye akili hawezi kufikiri anayeona Uzanzibari ni fahari ana akili.
Hawezi akautukuza Uzanzibari kwa kujiita sisi Wazanzibar na wao
Watanganyika.
Sidhani kwamba Uzanzibari ule una usalama ndani yake. Hatima
yake Zanzibar itajitenga; na Zanzibar ikijitenga kutokana na ule tu
kuwa (sisi) Wazanzibari na wao Watanganyika, haibaki. Wakumbuke
kwamba Muungano ndio unaowafanya wanasema sisi Wazanzibari
wao Watanganyika. Nje ya Muungano, hawawezi kusema hivyo:
kuna wao Wapemba na sisi Waunguja
Watanganyika (nao) wakiwakataa Wazanzibari kwa tendo la dhambi
ile ile ya sisi Watanganyika, wao Wazanzibari, wakautukuza usisi
Tanganyika na, kwa ajili hiyo, wakawafukuza Wazanzibari,
hawatabaki salama. Hapatakuwa na Tanganyika. Wakishajitenga tu,
Wazanzibari wako kando hivi, mmewafukuza mnajidai wakubwa
nyinyi: hawa nani hawa, wao wana Rais sisi hatuna kwa nini
tusiwatimue?. Mkiwatimua mkabakia kwenu hapa, hambaki kweni
mtasemaji? Mtakuwa mmeshatoa sababu ya kusema wale ni wao na
nyinyi ni nyinyi, wao vipi Wazanzibari; halafu mbaki nyinyi?.
48
Maana kama leo wapo kabila la Wazanzibari, mmewabagua, mtaanza
vijumba vya Wapemba, vipo vijumba vya Wapemba humu. Basi
watakimbia Wapemba. Baadhi yao wamo waliokimbia wakati ulee
wa zamani. Vijumba vya kwanza mtasema Wapemba Wapemba
kama kwa sauti ya nyinyi mliokuwa mnajiita sisi Watanganyika
mtakapoanza kuchoma nyumba za Wapemba. Mnazichoma moto zile,
mtakuta eh! sisi wote si wamoja. Mbona za Wapemba tulizichoma
moto za Wachaga hatuchomi kwa nini? Maana Wachaga si wazawa
bwana! Hapa kuna wazawa, sasa mnachoma za Wapemba tu za
Wachaga mnaacha? Mtakuta hakuna watu wanaitwa Watanganyika.
Mtakuta mnajidanganya tu. Mnadhani kuna watu wanaitwa
Watanganyika. Hakuna! Kuna Wagogo, Wanyamwezi, Wasukuma,
Wazanaki, Wakuria, Wamwera eh, wengi sana siwezi kuwataja wote.
Matakuta hakuna hiki kitu kizima kinaitwa sisi Watanganyika. (uk.
9-12)
Zaidi ya kuimarisha umoja wa ndani ya nchi, Muungano pia umelijengea
heshima kubwa Taifa letu na unaendelea kudumisha shauku ya kujenga
umoja wa Afrika.
MATATIZO
Wapinzani wa Muungano na hata wanaoutakia mema wanaweza
kuorodhesha matatizo au kero nyingi kwa idadi, lakini nyingi yake zilikuwa
zisizokuwa za msingi. Kero zimekuwapo, zipo na zitaendelea kuwapo.
Zipo zinazopatiwa ufumbuzi, zipo zinazoshughulikiwa na zipo
zitazoshughulikiwa kadiri zitavyojitokeza. Kero ni sehemu ya maisha.
49
Ukiiondoa hii inazuka nyingine. Kero ziko katika nchi zisizoungana, seuze
zilizoungana kama yetu. Na kama ilivyokwishaelezewa, wakati Muungano
unaundwa, matatizo yalitarajiwa kuwa yatakuwapo na yataendelea kwa
muda mrefu. Na hata tungekuwa na muundo wa Serikali Tau au Moja,
matatizo yangekuwapo tu ingawa ya sura tofauti.
Kazi ya kuimarisha Muungano ni ya kudumu kama ilivyo kazi ya kujenga
demokrasia. Haina mwisho. Waingereza walioungana toka karne ya 18
bado hadi leo wamo katika kuimarisha. Seuze sisi wa miaka 40 tu.
Kwa bahati nzuri, malumbano mengi yanayotokea hapa Tanzania juu ya
Muungano na muundo wake aghlabu huwa zaidi baina ya viongozi wa
Serikali na wa kisiasa, kuliko baina ya wananchi wenyewe.
Hivi sasa kuna Muafaka wa Serikali zote mbili uliofikiwa kufuatia
mapendekezo ya Kamati ya Wataalamu ya Kushughulikia matatizo ya
Muungano (Kamati ya Shellukindo) ya 1992. Muafaka huo ambao
unaendelea kutekelezwa hatua kwa hatua unatoa dira ya kuondoa kero za
Muungano. Miongoni mwa hatua zilizokwisha chukuliwa hadi sasa kufuatia
Muafaka huo ni Serikali ya Muungano kuipatia Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar asilimia 4.5 ya faida ya Benki Kuu na misaada ya nje; kuondoa
paspoti kwa Watanzania kuingia Zanzibar; kutungwa kwa sheria moja ya
Uraia; kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha ambayo itashughulikia
malalamiko yote yanayohusu uchumi na fedha, n.k.
Pamoja na wingi wa kero zinazozungumzwa aghlabu kwa kutiwa chumvi na
kwa jazba, ni heri kuzungumzia kero hizo kuliko kuzungumzia historia ya
50
muungano uliovunjika kama ambavyo pengine tungekuwa tunafanya hivi
sasa kama tungekuwa na Muungano wa Serikali Tatu. Ni rahisi zaidi
kuondoa kero kuliko kufufua muungano uliovunjika.
HITIMISHO
Imedhihirika katika hoja hii kwamba uhalali wa Muungano wa Tanzania
hivi sasa si suala tena la mjadala. Mjadala uliohamishiwa kwenye kuhoji
muundo wa Serikali Mbili nao unapungukiwa nguvu kutokana na wananchi
walivyothibitisha imani yao kwa muundo huo kila walipoulizwa. Baada ya
kukosa nguvu ya hoja, wapinzani wa muundo huo sasa wanategemea tu
mbinu ya hoja ya nguvu; maneno mengi, makelele na jazba.
Muungano wenye muundo wa Serikali mbili umefaulu mtihani wa nyakati
(has stood the test of time) kwa kuhimili misukosuko mikubwa na kudumu
kwa miaka 40 sasa, ukiwa mfano wa pekee Barani Afrika.
Matatizo ya Muungano yanaweza kuwa kwa idadi kwenye orodha, lakini
hayauzidi uzani wa mafanikio yake. Na mwelekeo uliopo ni kwamba
mafanikio na uimara wa Muungano vinazidi kuongezeka wakati kero
zinapungua.
Chini ya mfumo wa vyama vingi, kila chama cha siasa kina haki ya kuwa na
sera yake ya muundo wa Muungano na kuiwasilisha kwa wananchi. Kwa
upande wa CCM, sera ya muundo wa Serikali Mbili inaendelea.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
51
REJEA
A.S.P. (1974); Maendeleo ya Mapinduzi Ya Afro-Shirazi Party; Printpak
Tanzania Ltd.; Dar es Salaam.
CCM (1994); Taarifa ya Kura za Maoni Ya Wana-CCM Kuhusu Muundo
Muafaka wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Taarifa
isiyochapishwa.
CCM (1998); Tathmini ya Miaka 20 ya CCM, 1977 1997; KIUTA;
Dar es Salaam.
Mapuri, O.R. (1996); The 1964 Revolution: Achievements and
Prospects;TEMA Publishers; Dar es Salaam.
Mkapa, B.W, (2004); Hotuba Ya Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Kwenye
Sherehe za Kuadhimisha Miaka 40 ya Muungano; Mpiga
Chapa Mkuu wa Serikali; Dar es Salaam.
Mdundo, Minael Hosanna O. (1999); Masimulizi ya Sheikh Thabit
Kombo Jecha; DUP (1996) Ltd.; Dar es Salaam.
Mwinyi, A.H. (1995); Hotuba ya Rais Ali Hassan Mwinyi Akiagana na
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mpiga Chapa
Mkuu wa Serikali; Dar es Salaam.
52
Nyerere, J.K. (1968); Uhuru na Umoja; OUP; Dar es Salaam.
Nyerere, J.K. (1994); Uongozi Wetu na Hatima Ya Tanzania; Zimbabwe.
Publishing House; Harare
Nyerere, J.K. (1995); Nyufa; Taasisi ya Mwalimu Nyerere; Dar es
Salaam.
Othman, Haroub (2004); Forty Years of The Union: Is It Withering
Away?; Unpublished
Serikali ya Tanzania (1991); Ripoti ya Tume Ya Nyalali Kuhusu Mfumo wa
Vyama Vingi au Chama Kimoja; Mpiga Chapa Mkuu wa
Serikali; Dar es Salaam.
Serikali ya Tanzania (1999); Ripoti ya Kamati Ya Kuratibu Maoni Kuhusu
Katiba (Kamati ya Kisanga); Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali;
Dar es Salaam.
Sherif, Abdul (1987); Slaves, Spices & ivory In Zanzibar; Tanzania.
Publishing House, Dar es Salaam
Shivji I.G. (1990); Tanzania The Legal Foundations of the Union;
Dar es Salaam University Press; Dar es Salaam.