Upload
independent
View
1
Download
0
Embed Size (px)
Citation preview
TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMADAR-ES- SALAAM
KOZI: SHAHADA YA ELIMU YA WATUWAZIMA NA
MAFUNZO ENDELEVU.
MSIMBO: KUCHAMBUA NADHARIA ZA UHAKIKI
MSIMBO KODI: KIU 07431
MWAKA WA MAFUNZO: 2013/2014.
MUHULA : II
MKUFUNZI : MADAM KILEO
AINA YA KAZI: KAZI YA KIKUNDIMAJINA YA WASHIRIKI
1. ISSA TWAHA 336/BACE/2012
2. KIWANGO IRENE 360/BACE/2012
3. TUZIHIRWE NIKUNDIWE 471/BACE/2012
4. MAEMBE PATRICIA 373/BACE/2012
5. NGUNGULU NEEMA 434/BACE/2012
6. PALANGYO DEBORA 445/BACE/2012
7. HAMISI RABIA 334/BACE/2012
8. LWEYEMAMU ALFRED 368/BACE/2012
9. SOWOKI DEOGRATIAS.J 462/BACE/2012
10. BARTHOLOMEW MARY 310/BACE/2012
SWALI:
Uhakiki wa maudhui katika Riwaya ya Almasi za Bandia.
MPANGO WA KAZI
A: UTANGULIZI
(i) Historia Ya Mwandishi
(ii) Muhtasari Wa Kitabu
B: KIINI CHA SWALI
(i) Nadharia Iliyotumika Katika Uchambuzi
(ii) Uchambuzi wa Maudhui na vipengele vyake mbalimbali
vikiwemo:
Dhamira
Migogoro
Msimamo wa Mwandishi
Falsafa
Ujumbe
C: HITIMISHO
(Maoni ya jumla kuhusu mchango wa kitabu mchango)
Kufanikiwa kwa mwandishi
Mapungufu ya Mwandishi
UTANGULIZI
Historia ya Mwandishi
Mwandishi wa Riwaya ya Almasi za Bandia, Marehemu Chachage C.S.L
alikuwa Mhadhiri katika idara ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar-es-
salaam baada ya kutunukiwa shahada ya P.H.D ya chuo kikuu cha
Glasgrow, Uingereza. Katika uhai wake amaeweza kuandika riwaya
nne zikiwemo Almasi za Bandia, Sudi ya Yohana , Kivuli na Makuadi wa Soko
Huria. Kwa ujumla riwaya zake hizi zimejikita katika masuala ya
historia ya nchi katika vipindi mbalimbali ikiwemo historia mara
tu baada ya Uhuru na wakati wa utandawazi na tahri zake katika
nchi ya Tanzania.
Muhtasari wa Riwaya
Riwaya ya Almasi za Bandia inazungumzia matatizo mbalimbali
yanayoikumba jamii yetu ya Afrika kwa sasa katika Nyanja za
uongozi, kisiasa, kiuchumi na katika nchi za Ulaya jinsi watu
weusi wanavyobaguliwa kutokana na rangi zao.
Mwandishi Chachage amesawiri mawazo ya kimapinduzi kwa kuichambua
jamii ya Tanzania na hali nzima ya mfumo wa uongozi katika nyanja
za serikali, uchumi na kuonyesha uozo uliomo katika jamii ambayo
viongozi kwa kutumia madaraka yao hufanya biashara za magendo
kama vile; Gordoni ambaye ni Inspekta wa polisi alivyomtumia
ndugu yake Mertoni Mpwito kumuuzia mzungu ambaye anaitwa John
Gregory na mhindi Kanjir Almasi za Bandia uk 112.
Vilevile bado ubaguzi wa rangi upo katika bara la Ulaya
umeoneshwa kwa kuonyesha jinsi Waafrika wanavyobaguliwa na
kunyanyaswa, mfano huko Ulaya waafrika walikuwa hawaruhusiwi
kuchanganyika na wazungu katika makazi na hoteli.
Katika riwaya ya Almasi za Bandia iliyoandikwa na C.S.L Chachage,
mwandishi amesawiri matukio mbalimbali ambayo yapo na yanaendelea
kujitokeza katika jamii mbalimbali hapa nchini na hata nje ya
nchi. Katika riwaya hii msanii ameonyesha/amechora mambo
mbalimbali yanayojitokeza katika jamii mfano, matumizi mabaya ya
madaraka, ubaguzi wa rangi, umaskini, rushwa, matabaka ya
walionacho na wasiokuwanacho, biashara haramu, mapenzi na ndoa,
ubakaji, migomo, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, elimu,
ujasiri pamoja na nafasi ya mwanamke katika jamii. Dhamira hizi
zimechorwa na msanii kupitia wahusika mbalimbali kama Merton
Mpwito kada wa chama na kiongozi serikalini, Yakini ambaye
alikuwa ni mfanyakazi wa shirika la Umma, Faraji ambaye alikuwa
ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kilimo na Gordon ambaye ni
askari mpelelezi.
Nadharia Zilizotumiwa katika Uchambuzi
Katika uchambuzi wa riwaya ya Almasi za Bandia nadharia tatu
zimetumika zikiwemo nadharia ya U-Marx, Ufeministi na Semiotiki.
Nadharia ya U-marx ambayo misingi yake inaonyesha uyakinifu wa
hali ya juu katika kutumia wahusika kama vipaza sauti. Tumeona
alivyowatumia akina Yakini, Zambe, Tereza na Mzee Majikondo ambao
walikuwa wanakataa mfumo kandamizi katika jamii hususani katika
nyanja za uongozi. Mwandishi amemchora Merton Mpwito na mwenzake
Gordon ambao ni viongozi katika chama na serikali na ambao
hutumia nyadhifa zao kwa kukandamiza tabaka la chini ndani ya
serikali.Wahusika wamechorwa kusawiri mabadiliko ya kimapinduzi
ya kimaendeleo. Tereza anaonekana akihamasisha wenzake katika
kufanya maandamano ya kupinga vikali suala la viongozi
kujiongezea marupurupu wakati hali ya jamii ilikuwa ni mbaya.
Nadharia ya Ufeministi, vilevile imetumika katika kusawiri yale
yanayotokea katika jamii hususani mfumo wa ugandamizaji wa
wanawake katika ya ndoa na mila, na jinsi wanawake wanavyojaribu
kujikomboa ili kuleta haki na nafasi sawa kati ya mwanamke na
mwanaume.
Nadharia ya Kisemiotiki, pia imetumika ambayo inahusu msimbo wa
kiishara na jinsi watazamaji au wasomaji wa kazi ya fasihi
wanavyogundua maana ya ishara katika kazi hiyo. Mfano, Yakini
alimgeukia Tereza na kusema huku akimbonyezea jicho kwa utani wa
mazoea (uk 62).
Vilevile Merton Mpwito alivyotumbua macho yaliyoashiria mshangao
mkuu akiwa ametabasamu kwa dharau ya wazi kabisa (uk 77). Pia
tunamwona Yakini akichorwa na mwandishi katika (uk 75) kuwa
“Yakini aliduwaa. Hakuamini kabisa kile kilichotaka kutokea
dakika moja iliyopita”.
Dhamira Kuu
Dhamira kuu katika riwaya hii ni unafiki wa viongozi wa Kiafrika
na taswira hasi aliyovishwa Mwafrika kutokana na mtazamo wa
Wazungu huko Ulaya. Katika riwaya hii ya Almasi za Bandia, Mwafrika
anavishwa taswira hasi kama kujihusisha na uuzaji wa madawa ya
kulevya, wanawake weusi kujihusisha na ukahaba, Waafrika kupenda
starehe na mapenzi kuliko kufanaya kazi, Waafrika kuwa tabia za
ubakaji Hii inaonesha unafiki ambao unawagusa Wazungu kuhusu
mtazamo wao juu ya Waafrika waishio huko Ulaya pamoja na viongozi
wa Kiafrika wanaofuata nyayo za Wazungu badala ya kusaidia
Waafrika wenzao. Kwa ufupi mtazamo wa Wazungu kuhusu Waafrika ni
mtazamo hasi kwani Waafrika waliojaliwa kufika Ulaya wamekuwa
wakidharauliwa na kuvishwa sifa mbaya kama watu wanaojali sana
mapenzi kuliko kazi na watu wasiokuwa na maendeleo. Pia Mwafrika
mwenyewe amejivika sura ya bandia (Almasi za Bandia) kwa kufanya
mambo ambayo yanamwaibisha Mwafirika na kuwafanya Wazungu kuwa na
mtazamo hasi kuhusu Mwafrika. Kwa mfano ubakaji na uuzaji wa
madawa ya kulevya, ukahaba na kupenda starehe ni sifa walizovikwa
Waafrika kuwa ndiyo wanaofanya mambo hayo na siyo Wazungu. Kwa
mfano, tunaona Wazungu wakiamini kwamba Waafrika ndio wanaofanya
biashara ya madawa ya kulevya na ndio sababu iliyopelekea Yakini
na Chaupele wakamatwe na askari polisi pale uwanja wa ndege wa
Amsterdam. “Basi wote waliochukuliwa hapa ni Waafrika watupu. Kisa? Kwa kawaida
wanawashuku watu weusi kuwa ndio wauza bangi na madawa ya kulevya. Hakuna
hata mzungu mmoja aliyechukuliwa…” (uk.48).
Waafrika pia wanachukuliwa kuwa ni watu ambao hawajasoma, kwa
mfano pale Muhindi anaposema Fanya kaji mingi African hapana soma na iko
vivu. Hapana kuwa kama European.” (uk 19). Hapa alikuwa akiongea kwa
lafudhi ya Kihindi akimaanisha kuwa Waafrika wanastahili kulipwa
ujira mdogo na sio sawa na Wazungu kwa sababu hawajasoma. Bara la
Afrika pia linachukuliwa kuwa ni sehemu yenye shida nyingi,
umasikini, magonjwa njaa kwa mf…………………. .
Suala la Uongozi Mbaya
Kwa upande wa viongozi wa Kiafrika ni kuwa, Almasi za Bandia
zinawakilisha viongozi ambao si wakweli yaani walaghai na
matapeli ambao huyatafuta madaraka kwa udi na uvumba kwa
kuwaahidi wananchi mambo ya uongo ambayo hawayatekelezi. Hali
hii huonesha uongozi mbaya na matumizi mabaya ya madaraka kwani
viongozi hawa hutumia madaraka waliyopewa kinyume cha sheria kwa
kukandamiza, kunyonya, kuonea na hata kudharau walioko chini
yako. Msanii amewachora viongozi wa chama na serikali wakitumia
ovyo madaraka yao kwa kufanya mambo ambayo ni kinyume cha miiko
ya kazi zao. Viongozi hawa wa Kiafrika wanaonekana hata
wakiwatishia Waafrika wenzao kama inavyojidhihirisha katika nukuu
ifuatayo. Merton Mpwito, msanii amesawiriwa akitumia wadhifa wake
na kuwatishia wenzake kwa kujivunia madaraka yake.
Tunathibitishiwa na mwandishi anaposema “…………Mwache atakuja
tambua madaraka yangu siku moja” (uk 58), “……………… basi
tutakaporudi nyumbani ninyi wote hapa mtanikoma! Nimemaliza! Na
sina mchezo!”................ (uk 76)
Msanii amemchora Merton Mpwito ambaye alikuwa ni kiongozi katika
chama na serikali akiwatishia wenzake Yakini na Zambe ili tu
wasiseme ukweli juu ya tabia na mienendo mibaya ya kiongozi huyo.
Msanii amemchora Faraji Changamoto ambaye ni Afisa Utawala wa
Shirika la Uhuduniaji wa miradi ya kilimo akitumia madaraka yake
vibaya, pale alipomlinda mfanyakazi mwenzake Yakini kwa kutomkata
mshahara baada ya kubainika kwamba ana kesi mahakamani kama
sheria zinavyoagiza. Yakini alikuwa ni rafiki yake na Faraji
Changamoto. Alitumia urafiki wao kuvunja sheria, rejea uk 26,
mwandishi anasema, “………kwa kawaida kama ninavyotegemea kwamba
unaelewa, mfanyakazi akiwa katika hali kama hiyo, hubidi
asimaishwe kazi na kukatwa nusu mshahara hadi idhihirike kwamba
hana hatia. Naona ugumu sana kukutendea jambo hili. Wengi wetu
tunatambua na kuithamini kazi yako na msaada uwapao wafanyakazi
wenzako kikazi. Sitafanya hivyo, japo natambua kwamba navunja
sheria. “Sitafanya hivyo kwako” (uk.26)”.
Pia tunamwona Gordon askari mpelelezi ambaye amechorwa na
mwandishi akitumia vibaya nafasi yake ya uaskari. Gordon anafanya
biashara haramu ya kuuza Almasi za Bandia. Pia anamlazimisha
Yakini kusaini hati ya maelezo bandia ili atiwe hatiani kwa
makosa ambayo hakuyafanya (uk .86).
Kwa ujumla katika ujenzi wa jamii mpya tabia hizi za utumiaji
mbaya wa madaraka hazipaswi kuvumiliwa. Jamii inabidi iamue na
kujitoa mhanga kupambana na hali hii. Rejea (uk 106-107). Msanii
amechora jamii inapambana na viongozi wanaohujumu rasilimali za
nchi. Msanii anasema “…………….. hapa kulikuwa na mamia ya watu
waliokasirika, kulikuwa na wengine zaidi waliokuwa wanakuja pale
kwa nguvu na hasira za kifaru………..” (uk 107). Hii dalili ya watu
kukataa tabia mbaya za viongozi wetu na kuamua kufanya mapinduzi
katika harakati za ujenzi wa jamii mpya.
Saula la Uonevu na Ukiukwaji wa haki za binadamu (Injustice)
Dhamira hii imejidhihirisha kwa kuangalia jinsi vyombo vya dola
vianvyokiuka haki za binadamu kwa kuwaonea wananchi ambao
wanapigania haki zao. Kwa mujibu wa (Wamitia K.W, 2003: 347),
vyombo kandamizi vya dola vinahusishwa na mtaalam Lous Althusser
kueleze vyombo vinavyotumiwa na tabaka linalotawala kudhulumu na
kukandamiza tabaka tawaliwa. Vyombo kndamizi vya dola ni asasi
ambazo hutumia njia za kukandamiza ili kuwafanya watu na hasa
wafanyakazi kulitii tabaka tawala. Vyombo hivi ni kama polisi,
magereza na majeshi.
Katika riwaya ya Almasi za Bandia Mwandishi ameonesha jinsi vyombo
vya dola vilivyokuwa vinawakandamiza watu wa tabaka la chini,
akina Yakini ambao walikuwa wanapigania haki za wafanyakazi.
Wafanyakazi hao walikuwa wakifanya migomo kwa kutetea maslahi ya
wakulima pamoja na wafanyakazi wadogo lakini tunaona kuwa nguvu
za dola zinatumika ili kuwagandamiza badala ya kuwasaidia.
“…. Polisi Polisi! Watoto wa wakulima wanawapiga virungu.
Watoto wa wenzao wa wakulima wanaotetea maslahi ya wakulima! Polisi! FFU! FFU!....
Suala la Matatizo ya Kiuchumi
Hali mbaya ya uchumi ni hali ambayo jamii inashindwa kupata
mahitaji muhimu kutokana na kipato chao kuwa kidogo. Hali hii
imejitokeza pale wanafunzi walipokuwa wanakula chakula chenye
wadudu na huku wengine wakikosa kabisa hata hicho chenye wadudu.
“………. Siku zilivyozidi kwenda ndivyo maisha yalivyozidi kuwa
mabaya. Watoto walikosa matunzo kutokana na wafanyakazi kupata
kipato kidogo watoto walizagaa wakiwa matumbo wazi” (uk .20).
“Baadhi walidai kuwa wanafunzi ndio wanaoonewa kwa kupewa chakula
chenye wadudu na wengine wakadai ilibidi wavumilie chakula hicho”
(uk.12).
Wahusika mbalimbali walichorwa katika riwaya hii wanaonekana
kutegemewa mfano Zambe alitegemewa na mama Sadiki pia mwanae
Sadiki. Pia Yakini alitegemewa na watoto wake na Tereza alipokuwa
chuoni. Pia Tereza alikuwa anampelekea mama yake pesa kidogo ya
kujikimu kimaisha inadhihirishwa na mwandishi anaposema,
“… Tereza Mtweza mtoto pekee kwa wazazi wake naye alikuwa ni
tegemeo kubwa kwa mama yake” (uk. 63).
Pia tunaona wanafunzi wakipanga kuandamana hadi ofisi ya magazeti
ya serikali kupinga kitendo cha viongozi kujipa marupurupu wakati
hali ya uchumi ilikuwa ni mbaya (uk.13). Vilevile njaa ilitawala
kila mahali nchini inadhihirishwa na mwandishi.
“…..Hali ya maisha ilikuwa mbaya sana nchini gharama ya maisha
ilikuwa imepanda maradufu na sehemu nyingine za nchi zilikuwa na
njaa si Dodoma, si Moshi” (uk.18).
Tukiangalia maisha ya sasa ya Tanzania elimu inayotolewa
haimwezeshi mwanafunzi kujitegemea hivyo jamii kuendelea kuwa na
hali mbaya kiuchumi hata wale waliopata elimu.
Suala la Rushwa na Ulaghai
Rushwa ni hali ya kutoa/kupokea fedha au kitu cha thamani ili
kutoa huduma Fulani. Rushwa inaweza ikawa kati ya mtu aliye
kwenye nafasi fulani au mtu aliye kwenye madaraka ya jambo fulani
ili mtoaji apewe upendeleo. Pia tunaona jinsi rushwa ilivyotawala
katika sehemu za kazi tunamwona Yakini akiwa Uwanja wa ndege
akielekea Londoni lakini walinzi wanamtaka alipe fedha za kigeni
kama ushuru wa uwanja kinyume na maelekezo ambayo yalikuwepo.
Baada ya kutokuwa na fedha za kigeni analazimika kulipa sh 500/=
badala ya 200/= ambazo alitakiwa alipe.
“… Kwa hiyo unatakiwa kulipa ushuru wako wa fedha za kigeni na si
za Tanzania. Wewe si rushwa bado ni tatizo katika maeneo mengi
nchini Tanzania mfano Jeshi la polisi, askari wa barabarani
wanaomba rushwa na kuwaachia dereva wazembe, mahakamani na
hospitalini pia.
Suala na Migomo
Migomo ni hali ya kukataa kufanya jambo fulani kutokana na
kutoridhishwa na mwenendo mzima wa utendaji wa jambo hilo na
kipatikanacho kutokana na jambo hilo. Katika riwaya ya Almasi za
Bandia.Vilevile tumeona migomo mbalimbali ikifanywa na wanafunzi
pamoja na wafanyakazi walikuwa wakifanya migomo kwa kutetea
maslahi ya wakulima pamoja na wafanyakazi wadogo.
“…. Polisi Polisi! Watoto wa wakulima wanawapiga virungu.
Watoto wa wenzao wa wakulima wanaotetea maslahi ya wakulima!
Polisi! FFU! FFU!....
“Japokuwa waajiri walitukubalia, lakini walikuwa
wamechelewa.Tayari tulikuwa tumeshaanza mgomo. Hatukwenda kazini
uk 2”. Pia katika uk 13, mwandishi ananukuu kwa kusema kuwa:
“Na wengine wakaona kwamba migomo ndiyo njia mojawapo ya
kurekebisha hitilafu katika jamii uk 13”. Hata katika jamii yetu
ya sasa, tumeona migomo mbalimbali ya walimu, madaktari na hata
wabunge wa upinzani katika bunge la Tanzania ambayo inatokana na
kunyimwa haki za msingi za makundi mbalimbali katika jamii.
Suala la Mapenzi na Ndoa
Mapenzi ni hali ya kuingiwa moyoni na kuthamini mtu au kitu zaidi
ya mwingine au kingine. Ni hisia zinazohusiana na mahaba au hisia
za ndani kati ya mume na mke au kwenye familia.
Ndoa ni muunganiko wa mume na mke kutengeneza familia.
Mwandishi anamwonyesha Yakini pamoja na Tereza jinsi walivyokuwa
na mapenzi ya kweli toka wakiwa chuoni hadi pale walipooana.
Tereza alikuwa na mapenzi ya dhati kwa mumewe na Yakini alimpenda
Tereza pia. Tunaona pale jinsi Tereza alivyokuwa akifuatilia
jinsi mume wake alivyopelekwa pale uwanja wa ndege na akaenda
kulipa ushuru aliotakiwa kulipa. Tunadhihirishiwa na mwandishi
anaposema
“…. Tereza mkewe Yakini alizitoa hizo shilingi mia tano.Yakini
aliondoka pale hima huku mzee masharubu akimtakia safari njema”.
(uk 6)
Vilevile tunamwona Tereza alivyomtafuta mtu wa kumwekea dhamana
mumewe Yakini pale alipokuwa amekamatwa na polisi. Mwandishi
anatudhihirishia kwa kusema,
“…. Ilikuwa awekwe chini ya ulinzi, lakini kwa bahati njema,
Tereza alikuja hima na mtu wa kumwekea dhamana…” (uk 11)
Suala la Ngono Zembe na Ukahaba
Ngono zembe ni hali/ kitendo cha kufanya mapenzi yasiyo salama na
kiholelaholela bila kutumia zana za msingi, yaani kufanya mapenzi
na mtu asiye mumeo au mkeo wakati. Ukahaba ni hali ya mwanamke
kufanya biashara ya ngono au kuuza mwili wake kwa ajili ya
kujipatia pesa/fedha au kipato. Mwandishi anaonyesha suala la
ngono zembe pale tunapomuona Merton akishiriki ngono na Jane
ambaye si mkewe na mkewe Gloria anafumania. “……naye Gloria
alimtazama kisha akatazama kitandani Merton alikuwa amemlalia
Jane akimbusu kwa mapenzi motomoto..” (uk 97). Pia wanawake
wakubwa weusi walivyokuwa wakijihusisha na ngono zembe na vijana
wadogo. ukahaba ulivyokuwa ukifanyika ambapo wanaume wazee
walikuwa wakitembea na watoto wadogo kama binti zao wa kuwazaa
lakini ni katika hali ya kutaka kupata raha ya kijinsia. Vilevile
wanawake wakubwa nao pia kuchukua wavulana wadogo kwa lengo la
kutimiza raha zao kijinsia. Inadhihirishwa na mwandishi pale
anaposema;
“…. Unakaona kale kajamaa kafupi kale? Basi kanatoka Malawi. Sasa lile limama lizee,
nene na refu vile sijui katalipeleka wapi? Katamezwa na hilo jike” (uk 36)
Tunaona jinsi wanawake walivyofanya ukahaba kama ni biashara. Mwandishi
anasema;
“…. Waliwapa bei za huduma mbalimbali, kama ni kwenye maficho ya mlemle mitaani
bei ilikuwa nafuu, na kama ilibidi waende wote nyumbani basi bei iliongezeka zaidi” (uk
40).
Starehe
Hii inajidhihirisha pale ambapo akina Yakini wanaonekana
wakipenda mambo ya starehe kama kunywa pombe na kwenda kucheza
dance katika baa ya Western ambapo kuna mijimama ya Kiafrika
inayofanya mapenzi na vijana wadogo. Hii inajidhihirisha pale
wanapoonekana katika sehemu za starehe, Yakini na wenzake wakiwa
masomoni Uingereza ambapo kulikuwa na sehemu za starehe za
wazungu peke yao na Waafrika peke yao, kama vile mabaa. Hii pia
ianonesha jinsi Wazungu walivyokuwa na mtazamo hasi kuhusu
Waafrika. Kwa mfano pale wanapoambiwa na mtu mmoja, “Kwanini
hamkwenda kwenye baa ambazo zinatembelewa na watu weusi, badala yake mkaja
hapa?” (uk.41).Mbali na starehe ya kucheza dansi na kunywa, Yakini
na rafiki zake walioneakana kujihusisha na masuala ya kimapenzi
na wanawake waliikuwa wakijiuza baa. Kwa mfano pale
Suala la Ubakaji
Ubakaji ni kitendo cha kulazimisha kufanya mapenzi au ngono kwa
nguvu bila ridhaa ya mhusika. Katika riwaya hii tunaona jinsi
Vilevile mhusika mwingine Merton Mpwito anaonekana akimbaka binti wa Kihindi
aitwaye Patricia Tereza, ambapo alimfanyia tendo hilo bila ridhaa yake. Mwandishi
anadhihirisha hayo pale anaposema;
“….. Usinisogelee! Ukinisogelea nitapiga kelele! Merton alicheka kwa ufedhuli na
kumjibu, unapoteza wakati wako bure. Hakuna atakaye kuamini. Hukuja hapa kwa
kulazimishwa, wewe mwenyewe umejileta!!”….aliivuta chupi yake yule msichana na
kuichanilia mbali bila ya huruma wala kujali. Alikuwa anahema kama faru na kutoka
udenda wa uchu” (uk 70-71)
Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii
Kwa kuangalia nafasi ya mwanamke katika jamii, msanii amemchora
mwanamke katika nafasi mbalimbali ndani ya riwaya hii ya Almasi za
Bandia chanya na hasi. Kwa kiasi kikubwa katika riwaya ya Almasi
za Bandia, mwanamke amechorwa katika nafasi hasi.
Kwa upande wa nafasi hasi, mwanamke amesawiriwa kama kiumbe
kinachonyanayaswa ambapo hali hii huletelezea ukatili na
unyanaysaji wa kijinsia kama inavyojidhihirisha katika maelezo
yafuatayo:
Kwanza mwanamke amechorwa kama kiumbe duni kinachokandamizwa
katika jamii katika kipengele cha mapenzi. Hii inaonyesha kwamba
mwanamke amechorwa katika nafasi hasi. Tunaona jinsi Patricia
alivyokamatwa kwa nguvu na kunajisiwa na Merton Mpwito (uk 3)
Pia tunaona kitendo alichofanyiwa Patrisia kwa kubakwa na Merton
Mpwito (uk 62).
“…. Umesema Merton Mpwito alikukamata kwa nguvu na kukunajisi?”
Pia jamii ilimnyanyapaa Tereza baada ya kufukuzwa chuo kikuu
aliposhiriki kwenye maandamano, kwahiyo jamii ilimwona kuwa ni
dhalimu maradufu katika jamii kule kijijini kwao (uk 63).
Pili msanii anaendelea kuonyesha jinsi wanawake wanavyokandamizwa
na kunyanyaswa katika jamii, katika asasi ya kiutamaduni wa
kiafrika. “…. Lo! Wanawake duniani ni kundi moja kubwa la watu
wanaoonewa! Yaelekea jamii zote zimejaa ngono za kuhalalisha
uonevu….” (uk 62)
Tatu, msanii amemchora mwanamke kama chombo cha starehe (uk 40)
tunaona wanawake wakiuza miili yao mitaani. Msanii anasema “…..
wanawake waliuliza kama wanataka biashara? Pia katika (uk 28)
tunamuona mwanamke akigombaniwa na wanaume ili aende
kuwastarehesha kimapenzi (uk 36-37) Msanii anasema “….. kijana
alipigwa hadi kung’olewa meno kwa sababu ya kugombea hawa
wanawake.
Kwa upande chanya mwanamke amechorwa kama mtu anayeweza kuleta
maendeleo. Kwa mfano, mwanamke amechorwa kama kiongozi na
mwanamapinduzi na mtu shujaa anayeweza kuongoza jamii yake katika
kupambana na maovu. Pale tunapomuona Tereza akiongoza na
kuhamasiha maandamano ya wanafunzi wenzake pale chuo kikuu cha
Dar-es-salaam, wakitetea haki za wakulima na wafanyakazi.
Wakipinga kitendo cha viongozi kijipa marupurupu wakati ilikuwa
wazi kwamba hali ya nchi kiuchumi ilikuwa mbaya…” (uk 16) …..
huyu msichana aliitwa Tereza. Alikuwa amemuona usiku wa jana yake
wakati alipokuwa amejitokeza jukwaani kutoa maoni yake na
mawaidha kuhusu mbinu za kutumia katika maandamano….. (uk 16).
Pia mwanamke amechorwa kama mshauri mzuri wa wanaume na mwenye
upendo. Msanii amemuonyesha Tereza kama mwanamke jasiri
mfuatiliaji wa haki na mwenye upendo kwa Yakini amabaye ni mume
wake, pale alipotafuta mtu wa kumwekea mumewe dhamana (uk 116)..“
tereza alikuja hima na mtu wa kumwekea dhamana”.
Sita, msanii amemuonyesha mwanamke kuwa ni mtu mwenye msimamo,
pale Patricia alipokataa kwenda ugenini, “….. Patricia alisema
sikujua kama ninyi mna mawazo ya ubabe wa kiume, kwamba kuna kazi
fulani za wanawake tu. Karne ya ishirini hii! (uk 68)
Hata leo katika jamii zetu mwanamke anachukuliwa kwa namna chanya
na hasi mfano mwanamke ana chukuliwa kama mlezi, mchapakazi,
jasiri na mshauri katika jamii. Pia amechukuliwa kwa namna hasi
kwani anatumiwa kama chombo cha starehe, kufanya kazi ndogondogo
kama vile kupika, kufua na kuangalia watoto.
Suala la Ukatili na Unyanyasajiwa Kijinsia
Ukatili na unyanayasaji wa kijinsia ni masuala ambayo yana uhusiano
wa karibu. Suala la unyanyasaji wa kijinsia ni suala ambalo linatokea
sana katika jamii zetu za sasa na limekuwa ni chanzo na tatizo la
kuleta mifarakano katika jamii. Katika jarida la FEMA (2010, Des),
linaeleza kuwa unyanayasaji wa kijinsia ni tendo lolote lenye mtazamo
wa jinsia linaloweza kumsababishia mtu adha au kero, madhara na mateso
ya kimwili, kisaikolojia na kingono. Unyanayasaji wa kijinsia unatokea
kwa watu wengi hasa wasichana na wanawake kupewa mimba na kutelekezwa,
kupigwa, kudhulumiwa haki zao za msingi. Mifano ya unyanayasaji wa
kijinsia ni kama ifuatavyo: Kwanza, unyanaysaji wa kimwili kwa kumpiga
mtu au kumtishia mtu wa jinsia tofauti kwa silaha. Pili, unyanyasaji
wa kisaikolojia kwa kumdhalilisha mtu, kumtishia kumwacha na kumnyima
mahitaji mtu anayekutegemea. Tatu, unyanayasaji wa kingono kwa kumbaka
mtu, kufanya ngono na watoto wadogo na kumshikashika mtu bila ridhaa
yake. Hii yote ni sehemu ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Suala la Ubaguzi wa Rangi
Ni kitendo cha kutowathamini au kuwatenga binadamu kwa misingi ya
rangi za ngozi zao.
Katika dhamira hii ndogo pia msanii Chachage ameonyesha jinisi
wazungu walivyokuwa wakiwabagua watu wengine wakiwaita weusi,
mfano waafrika na wahindi. Waliwadharau na kuwanyanyasa kwa
kuwalipa ujira mdogo.
“ bwana mkubwa, kwanini mnaendelea kuwalipa Waafrika ujira mdogo na wazungu
ujira mkubwa pamoja na marupurupu mengi!” (uk 18-19)
“ ndio kijana, iko tambua ninyi ishi hali ngumu. Lakini kila mutu nalipwa kwa jinsi yake.
Fanya kaji mingi African hapana soma na iko vivu. Hapana kuwa kama European.” (uk
19)
“ hapana kataa iko jusi African kuwa tofauti na European’’ (uk 19)
Ubaguzi wa aina hii makazini/maofisini bado upo katika jamii zetu
za sasa, kwa mfano katika mabenki hapa nchini yanayomilikiwa na
wazungu au wahindi nafasi zote za juu zinashikiliwa na wao na
waafrika wanaishia kuwa makeshia, wafagizi na walinzi. Hii pia
tunaiona katika makampuni ya uwekezaji kama Tigo, Airtel, Vodacom
na migodini nafasi zote za juu ni za wazungu na wahindi wakati
waafrika wanafanya kazi ngumu kwa ujira mdogo.
“Penye kituo cha magari moshi yapitayo chini ya ardhi alikutana
na mashabiki wa mpira wa timu ya Rangers, wacha wamzomee,
wakimwita mtu wa Katanga, Nignog ambalo ni tusi maarufu la
wazungu kwa waafrika linalomaanisha mwanaharamu mweusi!Rudi kwenu
we mwanaharamu mweusi. Yakini alikasirika sana” (uk 32)
Hata sasa bado ubaguzi huo upo katika nchi za Ulaya katika
viwanja vya michezo, mashabiki wa kizungu na wachezaji wa kizungu
wanapowazomea na kuwatukana wachezaji wa kiafrika. Mfano,
Balotelli mchezaji wa taifa la Italia alipotupiwa ndizi kiwanjani
kwa kuashiria yeye ni nyani mweusi na John Terry alivyotoa lugha
chafu kwa Fednand wa uingereza na Suarez alivyomkashifu Patrick
Evra wa Ufaransa kwa kuwa wanarangi/ ngozi nyeusi, hayo yote
yanaonyesha jinsi ubaguzi wa rangi ambavyo bado upo katika baadhi
ya watu huko Ulaya.
Pia ubaguzi wa rangi unaonekana katika sehemu za starehe pale
kina Yakini na wenzake wakiwa masomoni Uingereza ambapo kulikuwa
na sehemu za starehe za wazungu peke yao na waafrika peke yao,
kama vile mabaa. Hii pia ianonesha jinsi Wazungu walivyokuwa na
mtazamo hasi kuhusu Waafrika.
“Kwanini hamkwenda kwenye baa ambazo zinatembelewa na watu weusi, badala yake
mkaja hapa?” (uk. 41).
“Baada ya muda mfupi Yule kijana aliwaasa tena kwamba ile baa haikuwafaa, ilifaa
waende kwenye baa ya watu wa aina yao” (uk. 42).
Ubaguzi wa aina hii pia bado upo katika baadhi ya nchi hapa
Afrika na hata Ulaya. Kwa mfano Afrika ya Kusini.
Katika kipengele kingine cha ubaguzi wa rangi tunaona wazungu
wakiamini kwamba waafrika ndio wanaofanya biashara ya madawa ya kulevya na ndio
sababu iliyopelekea Yakini na Chaupele wakamatwe na askari polisi pale uwanja wa
ndege wa Amsterdam.
“Basi wote waliochukuliwa hapa ni waafrika watupu.Kisa? Kwa kawaida wanawashuku
watu weusi kuwa ndio wauza bangi na madawa ya kulevya. Hakuna hata mzungu
mmoja aliyechukuliwa…” (uk 48)
Hali hii ipo hata sasa kutokana na matukio mengi ya hivi karibuni
ya baadhi ya waafrika wengi kukamatwa katika nchi za ughaibuni
wakiwa na madawa ya kulevya. Chanzo ni umaskini unaosababisha
watu kutamani/kutaka utajiri wa haraka kwa uvivu wa kufanya kazi
halali na kutumiwa katika usafirishaji wa madawa hayo kwa maslahi
ya wafanyabiashara wakubwa wa mataifa makubwa.
Suala la Elimu
Ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo
wa kimaumbile wa mtu binafsi. Katika dhana ya kiufundi, elimu ni
njia ambayo hutumiwa kimakusudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi
na maadili kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine.
Msanii anawachora wahusika kama Yakini, Tereza, Zambe na wengineo
ambao walikuwa masomoni Chuo Kikuu ambapo waliweza kuandaa migomo
ya kupigania haki za watu wa kipato cha chini. Elimu yao
iliwawezesha kujiamini na kuandaa mipango hiyo kwani kile
walichokuwa wanakipigania kilikuwa na faida kwa jamii nzima.
Tunathibitishiwa na mwandishi anaposema;
“ Jumapili ya tarehe tano mwezi wa tatu, wanafunzi walionekana
wakiteremka mjini, wakiwa wamebeba mabango na nyoyo zao zikiwa
zimejaa hamasa za kimapinduzi” (uk 14)
Hali hii bado inaendelea kujitokeaza katika jamii yetu ya sasa,
wasomi wa vyuo vikuu hugoma kutokana na hali ya kutotimiziwa haki
zao za msingi, kama vile Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu
kuwacheleweshea mikopo yao yaani kutowapa kwa wakati. Mfano mwaka
jana tuliona Chuo Kikuu cha Dodoma. Pia walimu na madaktari
waligoma kwa kutotimiziwa maslahi yao na vitendea kazi.
Msanii anaelezea kuhusu elimu kwamba, kiwango kikubwa cha elimu
kinaweza kusababisha mtu apate kipato kikubwa ili hali elimu
ndogo inafanya mtu apate kipato kidogo.
“Aliajiriwa katika bandari ya Dar-es-salaam kama mnyampara.
Alikuwa na kipato kikubwa kuliko mamia ya vibarua walioajiriwa
pale, lakini kwa madarasa yake mawili aliyosoma hakufua dafu kwa
makarani waliosoma kuliko yeye’’ (uk 18)
Hali hii inasawiri hali halisi ya muktadha wa waajiriwa katika
sekta mbalimbali serikalini na hata katika mashirika, taasisi na
makampuni mbalimbali nchini.
Imani na Itikadi za Kichawi na kishirikina
Msanii ameelezea suala la imani katika pande mbili, imani ya dini
na imani za kishirikina. Anaelezea imani ya dini kwamba ni
kumtegemea Mungu pale anaposema,
“Hawa wakristo walipinga kabisa imani ya kwamba iliwezekana watu kujilinda kama
jumuiya, kwani walidai kwamba ulinzi ilikuwa ni kazi ya Mungu na si ya binadamu.
Kwa hiyo wakakataa kushiriki katika migowe, shughuli za jumuiya na matambiko
yaliyowahusisha wahenga”. (uk 64). Pia mwandishi kwa upande mwingine
anaongelea imani za kishirikina jinsi zilivyopigwa vita pale
anaposema,“Baba yake Tereza hakuepukana na matatizo hayo, kwani
wakati wa uhuru na baada ya hapo kulikuwa na vita vikali dhidi ya
ushirikina na matibabu ya mitishamba…” (uk 65),“mara kukatokea
wimbi la imani kwamba kuna mtu aitwaye Chikanga huko Nyasaland
aliyeweza kuwatoa watu tunguri zao”.
Hii pia inadhihirisha hali halisi ya muktadha wa maisha ya sasa,
wasomi wengi hawaamini na wanapinga ushirikina, wao wanaamini na
kumtegemea Mungu peke yake ambapo jamii ya watu wasiosoma wengi
wanaamini sana ushirikina.
Suala la Kuiga Utamaduni na Mambo ya Kigeni
Utamaduni ni uzoefu wa kimaisha wa kundi la watu au jamii fulani
Utamaduni hujumuisha michakato ya kijamii ambayo huiwezesha jamii hiyo
kujielezea, kujitambulisha na pamoja na kufanya shughuli zakila siku,
(Wamitila, 2003:330). Mara nyingi vijana huwa wa kwanza kufuata
mienendo na matendo mipya ya maisha kwa kuwa huwa hawajazama katika
mfumo maalum wa maisha na wana matamanio makubwa ya kujaribu mienendo
mipya. Kwa hiyo ni rahisi kwa vijana kubadilika kwa vile imani zao za
kimsingi huwa zinaendelea kujengeka, (Wafula,1999: 18). Utamaduni ni
uzoefu wa kimaisha wa kundi la watu au jamii fulani Utamaduni
Katika riwaya ya Almasi za Bandia, mwandishi ameonyesha jinsi ambavyo
wanajamii imevamiwa na kuiga mambo ya Kizungu ikiwemo utamaduni wa
kigeni na masuala mengine hasa mambo ya usasa. Katika kuchambua
dhamira hii utamaduni wa kigeni na wa vipengele kama lugha, shughuli
za kiuchumi, matendo ya wahusika, uongozi, siasa na mtindo wa maisha
kwa ujumla kama vile mavazi, vyakula, mila na desturi vitaangaliwa.
Kwa mfano, Yakini na wenzake walivyokuwa Ulaya walikuwa wakienda
kucheza madansi ya Kizungu kwenye hoteli za kizungu. Almasi za Bandia
inaashiria/inawakilisha Waafrika Weusi wanaoiga tamaduni na mambo ya
Ulaya hususani pale wanapopata nafasi za kwenda Ulaya. Waafrika hawa
wameacha utamaduni wao na kuiga utamaduni wa Kizungu ambao
umefananishwa na Almasi za Bandia. Mfano, mhusika Merton na Wazungu.
Almasi za Bandia pia inawakilisha Wazungu wanaojifanya kuonea huruma
Bara la Afrika na kutoa misaada kumbe mioyoni mwao na katika hali ya
ukweli wanataka kuendelea kuwanyonya Waafika.
Motifu
Katika riwaya ya Almasi za Bandia, motifu zinazojitokeza ni motifu ya
safari na motifu ya msako. Hii inajidhihirisha kwa kumwangalia mhusika
Yakini anavyofunga safari toka Tanzania kwenda kusaka elimu nchini
Glasgow, Uingereza ambapo alifanikiwa kumaliza elimu yake ya Chuo
kikuu lakini alipata changamoto nyingi sana kuanzia alipoanza safari
yake pale Airport ya Dar es Salaam kwenda Ulaya. Yakini kule Ulaya
anakutana na kundi la vijana wa Kiafrika ambao wamejiingiza katika
matendo mbalimbali kama starehe na mengineyo, ambao kwa matendo yao na
vitu wanavyovifanya wanaibua dhamira mbalimbali kama elimu, starehe,
uuzaji wa madawa ya kulevya n.k Motifu hizi za safari na msako wa
elimu zinaibua dhamira na migogoro mbalimbali kama vile unyanyasaji wa
kijinsia, ubakaji Merton kumbaka Patricia ambayo hivi vinaibuliwa na
Yakini ambaye anaamuuliza Partricia mweneyewe.
Suala la Migogoro
Migogoro ni kipengele kimojawapo kinachotumika kuelezea maudhui.
Kutokana na mivutano inayotokea katika kazi ya fasihi, yanazuka
matukio ambayo yanasaidia katika kupata maudhui. Wamitila (2003)
anaeleza kuwa mgogoro hutumiwa kurejelea mvutano unaokuwako kati ya
mhusika mmoja na mwingine katika kazi ya fasihi au katika akili ya
mhusika mmoja. Migogoro ni sehemu muhimu katika msuko wa kazi ya
fasihi na huchukua sehemu kubwa ya kazi hiyo. Mgogoro hujitokeza kwa
njia mbalimbali. Senkoro ( 1982:4 ) anaeleza kuwa katika kazi ya
fasihi kuna migogoro kati ya wahusika, ama vikundi vya wahusika,
familia zao, matabaka yao na kadhalika. Migogoro yaweza kuwa ya
kiuchumi, kiutamaduni au kisiasa. Halikadhalika kuna migogoro ya
kinafsia ambayo inatokea katika nafsi ya mhusika.
Katika riwaya ya Almasi za Bandia ipo migogoro mingi ambayo imejitokeza.
Migogoro hiyo yaweza kuwa kati ya makundi ya watu na migogoro ndani
ya mhusika mwenyewe yaani migoggoro nafsia. Ifauatayo ni aina ya
migogoro iliyojitokeza kwenye riwaya ya Almasi za Bandia:
Migogoro ya watu wawili
Mgogoro kati ya Patricia na Merton
Chanzo cha mgogoro wao ni Merton kutaka mapenzi kwa Patricia.
Suluhisho ni Merton kumbaka Patricia. Je kulikuwa na suluhisho la
mgogoro?
Mgogoro kati ya Yakini na Merton
Chanzo chake ni kusingiziwa kwa Yakini kwamba, alimtumia
majambazi wakampiga. Suluhisho ni Merton kusema ukweli kwamba
alipigwa na wahindi kwa ajili ya kuwauzia almasi za bandia.
Mgogoro kati ya Gloria na Merton
Chanzo ni Gloria kumfumania Merton akiwa na Jeni. Suluhisho ni
Merton na Gloria kusuluihishwa na mjumbe wa nyumba kumikumi.
Mgogoro kati ya Zambe na Merton Mpwito
Chanzo chake ni Merton anadai Zambe anamchafulia jina lake.
Suluhisho ni barua ya wasafirishaji mizigo ambayo iliarifu kwamba
mizigo imefika salama.
Migogoro ya makundi
Mgogoro kati ya wanafunzi wa chuo kikuu na serikali
Chanzo ni wanafunzi kupinga kitendo cha viongozi kujipa
marupurupu wakati hali ya uchumi ilikuwa mbaya. Suluhisho ni
wanafunzi kuandamana kupinga kitendo hicho.
Mgogoro kati ya wananchi na viongozi kina inspekta Gordon.
Chanzo ni kumgonga mtu kwa gari la akina inspekta Gordon.
Suluhisho ni wananchi wenye hasira kali kuwapiga mawe na kuwauwa
kina Inspekta Gordon na Athuman.
Falsafa
Katika riwaya hii ya Almasi za Bandia, msanii anaamini kuwa kuna
unafiki/ ubandia katika nyanja au nafasi mbalimbali zinazoshikwa
na watu mbalimbali katika jamii ndani na nje ya Tanzania kwa
ujumla si kitu kizuri. Kwa mfano, ubandia wa viongozi ambao
wanaahidi kuwahudumiwa wananci lakini mwisho wa siku wanaenda
kinyume na maagano ambayo huletezea kuwa na uongozi mbaya.
Ubandia/ unafiki wa Wazungu kujifanya kuwa wanawapenda Wafrika
kwa kuwapa misaada na kufungua vitega uchumi mbalimbali kumbe nia
yao kubwa si kuwasaidia Waafrika bali kuwanyonya kiuchumi.
Pia msanii anaamini na kuonyesha kuwa ili kuweza kuondoa Almasi
hizi za Bandia, inabidi kuwe na ushirikiano mzuri katika jamii
ambao ni jambo muhimu kukuza jamii katika nyanja zote kisiasa,
kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Tena anaamini kuwa palipo
mvutano kati ya wema na ubaya lazima wema utashinda na kwamba
haki ya mtu haipotei hivihivi. Mwisho wa ubaya ni aibu.
( Ubaya alioufanya Merton kuuza madini bandia na baadae kupigwa.
Kisha akamsingizia Yakini kwamba ndiye aliyetafuta watu wampige
baadae tunamwona akiaibika baada ya kosa lake kugundulika).
Ujumbe katika Riwaya ya Almasi za Bandia
Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, wananchi walijiunga na
wanachuo kwenye maandamano wakiwa wamebeba mabango yaliyopinga
unyonyaji na kuunga mkono ujamaa huku yakilaani kitendo cha
viongozi kujiongezea maslahi (uk 14).
Mwanamke katika jamii ni lazima athaminiwe, aheshimiwe na
kushirikishwa katika maamuzi, Yakini alimshirikisha Tereza katika
mabo yote wakiwa bega kwa bega mfano ni pale wakati Yakini
alipoambiwa alipe shilingi mia tano mkewe Tereza alimlipia, pia
Tereza alionekana akimleta mtu wa kumwekea dhamana Yakini
(mumewe) (uk 5-6), (uk.11)
Uongozi mbaya ni adui wa maendeleo. Merton na Inspekta Gordoni
wanaonekana wakitumia vibaya dhamana zao za uongozi kwa kufanya
biashara haramu ikiwa ni pamoja na kutishiana kutokana na
madaraka waliyokuwa nayo (uk.110).
Kusingiziana si tabia nzuri kwa watu kwani inawezekana kutia watu
katika hasara, majonzi na sintofahamu, pia na kuleta utengano
mkubwa. Hali hii inaonekana pale Merton Mpwito akimsingizia
Yakini kuwa ndiye aliyemvamia na kumjeruhi. Usemi huu
unadhihirishwa na Merton Mpwito pale alipokiri mwenyewe alipokuwa
hospitali kuwa alipigwa na mzungu Gregory na Yule mhindi Kanjir,
aliendelea kueleza kuwa kaka yake Gordon na Athumani walikuwa
wamenipa Almasi za kumpelekea Gregory hotelini kwake. (uk 110-
111).
Hali ya kuwa na ubaguzi katika jamii sio kitendo kizuri kwani
huweza kukwamisha maendeleo na kuleta vita vikali. Hali hii
inaonekana pale ubaguzi wa rangi unapofanyika kati ya weupe dhidi
ya weusi na kuleta ugomvi wa mara kwa mara na vifo
visivyotarajiwa (uk.42).
Mbio za sakafuni huishia ukingoni, Merton na kaka yake Inspekta
Gordon walijitafutia utajiri wa haraka haraka kwa kuuza almasi za
bandia na wakaishia kufa.
Msimamo
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi kwa kuyatolea macho matatizo
yanayoikabili jamii katika kujikomboa kutokana na ukandamizaji
unaofanywa na viongozi wa Kiafrika na unyonyaji na ukandamizwaji
toka kwa Wazungu. Kwa mfano, Yakini ametumiwa na mwandishi kama
kipaza sauti cha kuleta mapinduzi haya na hatimaye anakamatwa na
kutiwa mbaroni bila kosa lolote. Mfano, Yakini anatengenezewa
kesi, anakamatwa, anateswa bila kosa lolote, viongozi wanakaa
kikao Wete Pemba cha kujiongezea maslahi wakati jamii inateseka.
Mwisho kunatokea maandamano/migomo kwa wanafunzi, wakulima na
wafanyakazi ambayo inaashiria kupinga hali za kionevu ili kuleta
mapinduzi.
Hitimisho
Almasi za Bandia ni riwaya inayosadifu mifumo ya siasa, uongozi na
masuala mbalimbali ya kijamii kama uchumi siasa na utamaduni na
kuonyesha jinsi watu wanvyopambana ili kukabiliana na kubadilisha
mifumo hiyo kandamizi katika nchi ya Tanzania na Afrika kwa
ujumla. Hivyo mwandishi ameonesha mapambano kati ya makundi
mbalimbali ya kijamii ili kuleta mapinduzi hayo hususani uongozi
na tabaka la chini la makabwela.